Sheikh Ponda, UAMSHO watuhumiwa kuhamasisha shambulio la tindikali kwa mabinti wa Kiingereza

Victims Kirstie Trup and Katie Gee
Gazeti la kila siku la Telegraph la hapa Uingereza linaripoti kuwa baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam visiwani Zanzibar wanaamini kuwa shambulio la tindikali dhidi ya mabinti wawili wa Kiingereza, Kirstie Trup na Katie Gee lilifanywa na wafuasi wa kikundi cha UAMSHO, ambacho kinataka Zanzibar ijitenge na Tanzania Bara na kisha kuanzisha sheria kali za Kiislam.

Huko nyuma kumeshatokea mashambulizi dhidi ya viongozi wa dini ya Kiislam na Kikristo, ikiwa ni pamoja na mashambulio ya tindikali na mauaji.

"Ofkoz, itakuwa kazi ya Uamsho," alinukuliwa Sheikh Fadhil Soraga, aliyeshambuliwa kwa tindikali Novemba mwaka jana, na anaamini wahusika katika tukio hilo dhidi yake walikuwa UAMSHO.

Wiki mbili zilizopita, vipeperushi vya vyenye wito mkali wa uchochezi dhidi ya Wakristo vilisambazwa sehemu mbalimbali huo Zanzibar, tukio linalohusishwa na harakati za UAMSHO.

"Siku 10 tu zilizopita, walikuwa wanasema wanaandaa kitu kikubwa. Tukio hili, ambalo Waislamu wote twapaswa kulilaani, ni kazi ya kundi hilo (UAMSHO)," alisisitiza Sheikh Soraga.

Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Zainzibar, Padri Cosmas Shayo naye alikuwa na mtizamo kama huo wa Sheikh Soraga. Mtangulizi wa Padri huyo, Padre Evaristus Mushi, aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi Februari, na hisia zimekuwa kwamba UAMSHO walihusika na tukio hilo.

"Hawa watu wamedhamiria kuzusha vurugu  ili kufikia malengo yao," alisema.

"Wanataka kuifanya Zanzibar iwe ya Waislam pekee, na walianza kwa kuwatisha Wakristo na sasa wanataka kuwatisha watalii ambao wanawaona kama Wakristo pia."

Kabla ya shambulio hilo la tindikali, mmoja wa mabinti hao, Katie, alizabwa kibao na mwanamke mmoja mtaani wakati wa mfungo wa  Mwezi wa Ramadhan.

Katie na Kirstie, walikuwa Zanzibar wakifanya kazi kwa kujitolea, baada ya kumaliza masomo yao ya sekondari. Wote wanatoka katika familia zinazojiweza kimaisha. Baba ya Katie ni chartered surveyor,moja ya ajira inayolipa vizuri hapa Uingereza, huku Kirstie alisoma sekondari ambayo ada yake ni pauni 3,375 (zaidi ya Sh milioni 13)  kwa muhula.

Mabinti hao walikuwa Zanzibar kwa mwezi mmoja wakijitolea katika shule ya chekechea ya Mtakatifu Monica, iliyopo Stone Town, kupitia shirika la kujitolea la Art in Tanzania.

Siku moja kabla ya shambulio hilo la tindikali, ali-tweet kwa furaha baada ya kukutana na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, alipozuru Zanzibar hivi karibuni kuhamasisha vita dhidi ya malaria kupitia Clinton Health Access Initiative.

Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph, mmoja wa masapota wakubwa wa UAMSHO ni Sheikh Ponda Issa Ponda, anayedaiwa kutumia wiki tatu zilizopita kuhamasisha Waislam Zanzibar 'kuamka kama huko Misri.'

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Elieza Feleshi alinukuliwa akisema kuwa Serikali itafanya kila jitihadakumkamata Sheikh Ponda.

Wakati huo huo, gazeti la kila Jumapili la Sunday Mirror lina habari ndefu kuhusu Sheikh Ponda, iliyobeba kichwa cha habari: "Shambulio la tindikali Zanzibar: Mhubiri wa chuki Sheikh Ponda Issa Ponda apigwa risasi na polisi, akamatwa"

Gazeti hilo limeeleza kuwa polisi walimpiga Ponda risasi ya machozi begani kabla ya kumkamata, na sasa yupo mahututi hospitalini.

Habari hiyo inaeleza kuwa Ponda alikwenda Zanzibar kuhamasisha maandamano dhidi ya serikali, na kukiunga mkono kikundi cha UAMSHO, kwa malengo ya kutimua wageni Zanzibar na kuanzisha sheria za Kiislam

Post a Comment

أحدث أقدم