TAARIFA YA SERIKALI KWA VYOMBO VYA HABARI


utalii
TAARIFA YA SERIKALI
Ndugu Wananchi,
Jana majira ya saa moja usiku, nchi yetu imekutwa na tukio la kusikitisha sana la kushambuliwa kwa kumwagiwa tindi kali watalii vijana wawili raia wa Uingereza Kate Gee na Kirstie Trup wwote wakiwa na umri wa miaka 18. Shambulizi hilo lilifanyika katika eneo la Shangani. Tukio hilo ni kubwa na linashitua sana kwani limeanza kuchukua sura mpya kutokana na tindi kali kuanza kumwagiwa wageni.
Kumwagiwa vijana hao tindikali hakuwezi kuachiwa hata kidogo kwani kitendo hicho kinajaribu kuiondoshea nchi sifa iliyojijengea ya Zanzibar kuwa ni eneo la Amani na Utulivu. Mbali hayo, tendo hilo halikubaliki katika mazingira ya kibinadamu kwani kila binadamu ana uhuru wa kuishi na kutembea akiwa ana uhakika na usalama wake. – Sisi wenyewe Wazanzibari, tunatembea na kuishi nchi mbali mbali za kigeni.
Kuachwa kuendelea kwa vitendo vya aina hii kunaweza kuwajengea hofu wageni na raia wetu. Aidha, kitendo hicho kinaweza kuathiri sana sekta ya utalii ambayo ni sekta kiongozi katika muhimili wa uchumi wetu.
Katika kuhakikisha jambo hilo halipewi nafasi kuendelea tena, serikali imekusudia kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuendesha uchunguzi mkali wa kuwasaka wahusika ili kuweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.Vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi kwa pamoja kuwatafuta wahal;ifu hao na mara watakapokamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria. Katika kufanya kazi hiyo Serikali inawaomba wananchi kutoa ushirikiano utakaopelekea kuwakamata na kuwafikisha katika vyumba vya sheria wote waliohusika na tukio hilo. Serikali ya Zanzibar kwa upande wake inaahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayesaidia kukamatwa kwa watu waliofanya uhalifu huo.
Ndugu Wananchi,
Kwa vile bidhaa ya tindi kali katika siku za hivi klaribuni imeanza kutumika vibaya, Seikali inachukua kila hatua kudhibiti matumizi ya bidhaa hiyo kwa kudhibiti uingizaji, usambazaji, upatikanaji na utumiaji wa tindi kali na inazitaka taasisi zote zinazohusika zitimize wajibu wake kwatika matumizi ya tindikali kwa kutumia sheria iliyopo na kwa haraka kutunga kanuni za kuthibiti uuzaji na matumizi ya tindikali.
Katika kuhakikisha vitendo vya uhalifu haviendelei na hasa katika maeneo ya utalii yakiwemo maeneo ya Mji Mkongwe na kwenye maeneo ya fukwe, Serikali inachukua hatua za makusudi za kuweka ulinzi utakaosaidia wageni wetu kuja nchini na kutembea bila ya bughudha.
Kupitia kauli hii, Serikali inaomba wananchi wote kutoa ushirikiano mkubwa katika kulinda sekta ya utalii kama ndio chanzo kikubwa cha uchumi wa nchi yetu.
Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunatoa pole kwa waliojeruhiwa na familia zao na tunawaombea waliojeruhiwa wapate nafuu haraka. Aidha, tunatoa pole kwa ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania na kuuomba watupelekee masikitiko ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Serikali ya Uingereza kwa tukio hilo na kwamba tutafanya kila jitihada matukio kama haya yasitokee tena.

Post a Comment

أحدث أقدم