Micheweni.
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Mkoa
wa Kaskazini Pemba, wametoa mapendekezo ya pamoja wakitaka mambo matano
yaondolewe kwenye Muungano, yabaki kwenye Serikali washirika.
Waliyopendekeza yaondolewe ni Mambo ya Nje, Uraia na Uhamiaji, Sarafu
na Benki kuu, usajili wa vyama vya siasa pamoja na ushuru wa bidhaa
wakisema kwamba kama yataendelea kuwepo kwenye Muungano kama
ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yatasababisha Serikali
shirikishi kuwa dhaifu.Wakizungumza baada ya kuwasilishwa kwa kazi za
makundi yaliyopewa jukumu la kujadili suala la mihimili, wajumbe hao
walisema mambo hayo matano ndiyo yanayoweza kuzipa nguvu Serikali
shirikishi ambazo zitakuwa Tanganyika na Zanzibar.
Walitolea mfano wa mambo ya nje na kusema kuwa ikiwa Rais wa Serikali
ya Tanganyika au Zanzibar ataondolewa jukumu la kuteua mabalozi na hata
kuiwakilisha nchi nje ya nchi atakuwa ameondolewa meno. “Nchi washirika
ziachiwe masuala ya mambo ya nje,”alisema Kassim Mohamed Kassi, mkazi
wa Chimba akiwakilisha vijana.
Kuhusu Sarafu na Benki Kuu, walisema sababu za kupendekeza iondolewe
katika muungano ni kuwa itadhoofisha uchumi wa nchi washirika.
Aidha kwa upande wa uraia na uhamiaji, walisisitiza kuwa kila nchi
watu wake wana utamaduni usioingiliana na nchi nyingine washirika, hivyo
kila upande uwe huru.
Ushuru wa bidhaa, wajumbe hao walipendekeza ubaki kwenye nchi
washirika na siyo Muungano kama inavyopendekezwa kwa sababu ikiwa
itaachwa hivyo sehemu kubwa ya kodi na ushuru kutoka nchi washirika
zitashindwa kuwanufaisha watu wake.
Kuhusu usajili wa vyama vya kisiasa, wajumbe hao walisema hiyo ni
moja ya kero za muungano iliyojitokeza baada ya kuingia kwa mfumo wa
vyama vingi. Sheria ya chama ili kisajiliwe sharti kipate wanachama wa
mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar. Walitaka mambo ya muungano yabaki
mawili tu ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
pamoja na Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano.
Mwananchi
Post a Comment