Wateja wa maji Moshi kulipa ankara kwa mtandao; Namba zatolewa kuripoti matatizo

 
PictureCyprian Luhemeja
ZAIDI ya wateja 21,000 wa mamlaka ya majisafi na taka mjini Moshi (MUWSA), wanatarajiwa kuanza kulipia Ankara zao za maji kwa kutumia mitandao ya Tigo Pesa, M-PESA, Airtel Money na Easy Pesa kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.

Mamlaka kuingia katika mitandao hiyo imelenga kuwarahisishia wateja wake muda wa kukaa katika foleni kwenye ofisi za mamlaka na sasa watapata fursa ya kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuongeza uzalishaji mali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, mkurugenzi mtendaji wa MUWSA, Cyprian Luhemeja alisema mpango huo aliouita wa 'dijitali' upo katika hatua za mwisho na ni sehemu ya uboreshaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi katika shughuli za maendeleo.

Alisema pamoja na mpango huo, hautaathiri nafasi za ajira kwa watumishi wake bali wanachofanya kwa sasa ni kusimamisha ajira mpya na waliopo kuhamishiwa katika ofisi ndogo ya Himo ambayo ni sehemu ya mamlaka itakayokuwa ikitoa huduma.

Mapema wakati wa ziara yake ya siku nane mkoani Kilimanjaro, Naibu

Waziri wa maji Dk Binillith Mahenge aliitaka MUWSA kusaidia usambazaji huduma ya maji katika mji mdogo wa Himo ikiwa ni baada ya kutoridhishwa na usambazaji unaofanyika sasa.

Akizungumzia mgawo wa maji, Luhemeja alisema umefutwa baada ya mamlaka kufanikiwa kupunguza upotevu wa maji wa asilimia 39 hadi kufikia asilimia 28 mapema mwezi uliopita huku lengo likiwa kufikia asilimia 9 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

“Chini ya mpango wa matokeo makubwa sasa ‘Big result now’ hakuna tena mgawo wa maji kuanzia Agosti 1, tumefungua call center, wateja watatupigia simu kupitia namba ya bure 0785 555555, nyingine 02755045 au 0275500021 saa 24, kueleza matatizo ya maji katika maeneo yao,” alisema Luhemeja.

Aidha mkurugenzi huyo alisema bado kuna upungufu wa maji kwani kiasi kinachozalishwa sasa ni lita za ujazo 27,000 huku mahitaji ni uzalishaji wa lita 38,000 na kwamba lengo ni kuzalisha lita za ujazo 40,000.

Alisema kiwango cha maji kitaongezeka mara baada ya kukamilika kwa Visima vya Lunguo, KCMC na tanki la Kilimanjaro, huku pia mamlaka ikitenga zaidi ya Mil 46 kwa ajili ya usambazaji maji maeneo ya Kiborloni, Rau na KDC.

Kwa upande wake,afisa uhusiano wa mamlaka hiyo,Dora Killo alisema mamlaka hiyo ina zaidi ya wateja 21,000 katika manispaa ya Moshi, sehemu ya weruweru na Shirimgungani wilayani Hai na baadhi ya maeneo wilayani Moshi vijijini huku lengo likiwa kufikisha wateja 50,000 ifikapo Juni mwaka 2014.

--- Imeandikwa na Dixon Busagaga wa globu ya Jamii Moshi

Post a Comment

أحدث أقدم