YANGA IUKUBALI MKATABA WA AZAM TV ILI KUZIOKOA KLABU ZINGINE



SIKUTAKA kukurupuka kutoa maoni yangu kuhusiana na sakata la Azam TV mpaka nilivyofikiria kwanza. Nimezingatia sababu zifuatazo, kwanza; Sipo tena katika uongozi wa klabu, pili; Nilishajiuzulu umakamu Mwenyekiti wa klabu za ligi.

Tatu; Sikuwa nimeona rasimu ya udhamini wa Azam  na nne; Sikuwa Dar es Salaam, hivyo kukosa baadhi  ya dondoo muhimu kuhusu masuala hayo.

Kutokana na kuwa miongoni  mwa waanzilishi wa mchakato wa kupigania ligi huru, nimeona bado nina wajibu wa kutoa maoni na kueleza kile ninachokijua kwa faida ya waliouliza na mpira wetu kwa ujumla. Lengo langu si kuwahukumu wadau kwamba huyu amekosea au huyu hajakosea. Lengo hapa ni kujenga kile ambacho wadau wa mpira na umma kwa ujumla umekuwa ukipigania.

Sheffield FC, Nots County, Stoke City, Nottingham Forest, Sheffield Wednesday, Chesterfield, Rhotheram, Reading, Aston Villa na Birmingham City (Smallheath FC).

Hiyo juu ni orodha ya klabu kongwe katika Ligi ya England. Lakini ikumbukwe kwamba Sheffield FC ndiyo klabu kongwe kuliko zote duniani inayotambuliwa na Fifa, bahati mbaya inacheza ligi ya chini isiyo ya kulipwa. Stoke City ndiyo klabu kongwe kuliko zote katika England. Kwa mashabiki wa mpira wa Waingereza watashangaa kutosikia majina ya timu wanazozishabikia.

Napenda kutolea mfano Waingereza kwa namna wanavyouendesha mpira wao na ndiyo maana ligi yao ni maarufu kuliko zote dunianai. Mfumo wa Waingereza unajali sana kuwepo kwa klabu hizo za  soka kama sehemu ya urithi wao.Watafanya kila wawezalo kuhakikisha timu hazifi.

Na hata zinapofilisika wataziweka chini ya uangalizi mufilisi (administration) kama ilivyowahi kutokea kwa Chelsea, Leeds na Portsmouth ili kuhakikisha zinakuwa hai. Kitu kimoja wasichofanya ni kuzitafutia timu nafasi katika ligi au daraja husika. Hakuna mwenye nafasi  au daraja la kudumu.Uwezo wako na ubunifu wako utakubeba.

Ni mpira wa ushindani na hii ni mojawapo ya siri ya umaarufu wa Ligi Kuu England (EPL). Pamoja na hayo yote, wenzetu wanatambua sana mchango wa klabu zenye uchumi mdogo katika maendeleo. Hivyo miradi mingi inayoibuliwa na Chama cha Soka (FA) pamoja na udhamini uhakikisha kwamba maslahi ya timu zilizo chini hayapuuzwi.

Wanajua kwamba huko chini ndilo chimbuko la vipaji na mafanikio ya walio chini ni sehemu ya mafanikio ya ligi nzima. Ndiyo maana timu inayoshuka daraja Uingereza hupewa fedha za mwavuli (parachute money) ili kuendana na maisha katika daraja la chini.

Hapa kwetu, kuna klabu za kihistoria kama Yanga, Simba, African Sports (Zanzibar na Tanga),Coastal Union na zingine ambazo kwa bahati mbaya au makusudi zimekufa au yamebaki majina tu. Katika hizo ni Young Africans (Yanga) na Simba (zamani Sunderland) ambazo zimekuwa na nafasi za kudumu katika ligi ya juu.

Hali hii ambayo yawezekana imetokea kiasilia au imetengenezwa, imezipa klabu hizi mbili mashabiki unazi (cult fans) kiasi cha kuwa kama dini mbili kuu za mpira wa Tanzania.

Wakati tunasherehekea hili kama sehemu ya urithi wetu, tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba hatulewi  (obsession) utamaduni huu kiasi cha kukwamisha maendeleo. Tunatakiwa kuzilinda klabu hizi kongwe bila kuzifunga mbeleko kimchezo na tunatakiwa kuzidhibiti bila kuzifunga gavana kimchezo. Huu ni mpira, na siku zote utabaki kuwa mchezo unaotoa fursa sawa kwani hauchezewi gizani.

Kama nilivyosema hapo juu, hali ya mpira wetu kutawaliwa na klabu mbili inaweza kuwa matokeo ya bahati mbaya na makusudi. Inaweza kuwa matokeo ya kimchezo au matokeo ya kibiashara na hata kisiasa.Yote kwa yote na bila kunyoosheana vidole, Chama cha soka na klabu kongwe zina wajibu wa kuweka mazingira sawia ya kiushindani  badala ya kuendeleza tofauti kubwa wakati mchezo unabaki ni mmoja.

Niliposikia kuhusu malalamiko dhidi ya Azam TV, nilijua yatakuwa yanatoka kwa klabu zingine si Yanga au Simba kwani klabu hizo ndizo zimekuwa zikilia ukata kila mara  wakati watani wa jadi wakiwa na hali nzuri (kwa viwango vya Tanzania).

Klabu hizi zimekuwa zikiibua vipaji lakini wanachokipata hakiendani na juhudi zao. Na wakati mingine hupoteza vipaji (kiubabe) bila ya kupata malipo yoyote.

Baada ya kuung’oa ubaguzi wa rangi (Apartheid) pale Afrika ya Kusini, zilifanyika juhudi za makusudi za kupunguza tofauti. Ilikuja miradi kama BEE (Black Economic Empowerment), mradi huu ulitoa upendeleo maalum kwa biashara zilizomilikiwa na watu weusi na wa rangi mchanganyiko ambao kwa kipindi kirefu waligandamizwa na weupe.

Lengo halikuwa kuwamaliza weupe lakini  kuwasaidia waliobaki kupata fursa zilizopotezwa (Lost advantage). Hivyo hivyo, Shirikisho na klabu za Yanga na Simba wana wajibu na deni kwa klabu nyingine na maendeleo ya mpira kwa ujumla. Wanasema aliye na kingi ana wajibu mkubwa zaidi, kwani kupata kwake kumechangiwa na wengi.

Mchakato kuelekea kuwa na chombo cha kuendesha ligi haukuwa rahisi. Kama klabu tulishaona fursa na ufanisi unaoweza kupatikana katika uendeshaji wa ligi iwapo chombo huru kitafanya kazi hiyo moja badala ya TFF ambayo ina majukumu mengi. Mimi na Mwenyekiti wangu (Geofrey Nyange Kaburu) na viongozi wa  klabu tulikuwa na vikao vingi (rasmi na visivyo rasmi) na Mwenyekiti Leodegar Tenga na makamu wake kuhusu suala hili.

Tulifanya mahojiano mengi na vyombo vya habari na kujaribu kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa chombo huru cha kuendesha ligi. Tulifika mahali hata tukaandaa rasimu (draft) ya makubaliano (Memorandum and Articles) ya kutengeneza kampuni ya ligi nje ya utaratibu wa TFF. Baadaye tulifikia muafaka na Rais wa TFF na kamati ya Utendaji juu ya kuweka utaratibu wa mpito kuelekea bodi huru ya Ligi.

Katika utaratibu huu iliundwa kamati ya ligi ambayo kazi yake ya kwanza katika masuala ya udhamini ilikuwa kujadili mkataba wa Vodacom huku kila mara ikirudi kwa klabu kueleza maendeleo. Pamoja na kuteuliwa na Rais wa TFF, kwa kiasi kikubwa iliundwa na wawakilishi wa klabu. Mojawapo ya mambo yaliyokuwa yanatupa msukumo ni kuona kuna klabu ni maskini kiasi cha hata kutosafiri kwenda kutimiza majukumu yao ya ligi.

Haikupendeza kuona kuna timu zinapata pointi si kutokana na uwezo wao wa kucheza mpira bali uwezo wao wa kulipia nauli. Yote kwa yote ilikuwa ni vigumu kupata kampuni  ya kimataifa ya kujitosa kudhamini ligi nzima.

Mkataba wa Azam TV, iwapo utatiwa katika vitendo ni mwanzo mzuri na chachu ya ushindani katika ligi yetu. Bila shaka, hakuna zuri lisilo na kasoro, Bodi ya Ligi itakapokuwa imeanza itaangalia maeneo ya kuboresha kwa manufaa ya ligi yenyewe na mpira kwa ujumla. Tutake tusitake, udhamini wa TV kwa ligi za nchi zinazoendelea unahitaji kujitoa muhanga.

Hakuna mwenye ukweli 100% kuwa miaka mitatu ya udhamini itamtengenezea Azam Media  faida. Ni ukweli usiopingika kwamba kama makubaliano yatatekelezwa kwa ukamilifu  udhamini huu utakapokamilika utakuwa umeitangaza ligi na eneo ilo la uwekezaji. Na yawezekana Azam asishinde zabuni itakayofuata baada ya miaka mitatu na hivyo kuifaidisha kampuni itakayoshinda.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba ligi ikionyeshwa moja kwa moja wako wadhamini wengine (co-sponsors) wa ndani na nje watakaoingia kuwekeza katika mpira wetu.Nina imani klabu zetu za kihistoria hapa Afrika Mashariki (Yanga na Simba) zinaweza kupata udhamini binafsi (exclusive) ikiwa ni matokeo ya kuonekana katika Azam TV.

Walichokifanya kamati ya ligi ni sawa na hadithi ya kijana ambaye baada ya kushinda juani akiuza maembe yake bila kupata mteja, kwa vile aliamini katika ubora wa maembe yake, aliamua kula embe moja. Baada ya kuanza kula kila aliyepita alivutiwa na harufu nzuri ya embe na kununua kisha ukawa umati mkubwa kiasi cha kijana kulazimika kwenda nyumbani kuangua mengine ili kukidhi kiu ya wateja wake.

Ligi yetu ni bidhaa ambayo inahitaji mtu wa kujitoa muhanga kudhamini kwani pamoja na yote haijatangazwa vya kutosha. Udhamini huu utaipa bodi ya ligi kiburi na kujiamini wakati wa kujadiliana na wawekezaji huko mbele maana bidhaa itakuwa ipo (real) imeshafanyiwa majaribio na si ya kufikirikia

Wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, ulifanyika mkutano wa Tanganyika African National Union pale Tabora. Kulikuwa na pendekezo la uchaguzi kufanyika katika misingi ya rangi yaani Wazungu, Waasia na Waafrika. Suala hili liliwagawa sana Tanu kwani lingeamua wawe au wasiwe sehemu ya serikali ya madaraka ya ndani ambayo ingekuwa nafasi kubwa ya kupewa uhuru kamili hapo baadaye.

Lakini Rais wa Tanu, Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere alikuja na busara moja kwamba kuwemo katika uchaguzi kuna mengi (ingawa si yote) ya kupata na kutoshiriki ni kupoteza yote. Mara nyingi ni vizuri ukawa na pa kukanyaga kwanza kabla ya kuruka.

Kwa busara hii ningeshauri klabu kuingia udhamini huu huku wakiendelea kusaka njia nyingine za kujipatia riziki.

Haki za matangazo si dhahabu ardhini kwamba usipoitumia haiozi. Ni bidhaa ambayo inahesabika kwa muda,usipoitumia (kwa kwenda hewani) imepotea na ya kesho haina uhusiano na ya leo. Si rahisi udhamini wowote (hata ule tunaoutolea mifano) ukawa timilifu. Matatizo ya klabu nyingi yanahitaji utatuzi wa leo na baada ya hapo kuweka mikakati ya mbele. Bila shaka ligi ya msimu wa 2013/14 itakuwa na msisimko wa aina yake.

Katika kila mwendo hakukosi msuguano, ninaamini klabu zina mengi ya kufanana kuliko kutofautiana katika suala la matangazo ya mechi. Na mara nyingi kitu kipya (hata kama ni kizuri) huleta mashaka,wasiwasi na woga lakini hayo yote yakipewa mtazamo chanya yatakuwa na faida mbeleni. Hii ni fursa ya kihistoria kwa mpira wa Tanzania iwapo pande zote zitatimiza wajibu wake.

(Mwandishi wa makala hii Selestine Mwesigwa ni Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga na Makamu Mwenyekiti wa klabu za Ligi Kuu (VPL) wakati wa harakati za kuunda kampuni ya ligi)

Post a Comment

أحدث أقدم