Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young Africans leo imetuma salaam kwa timu ya Azam ambayo watakutana siku ya jumamosi katika mchezo wa Ngao ya Hisani baada ya kuichapa Sports Club Villa ya Uganda mabao 4-1.
Ikiwa na wachezaji wake wapya Yanga iliingia uwanjani kwa lengo la kuhakikisha inaendeleza wimbi lake la ushindi, ikizingatia ndio timu yenye kikosi bora kabisa kwa sasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mshambuliaji aliyerejea Yanga akitokea klabu ya Azam FC, msimu uliopita akichezea Simba SC Mrisho Ngassa aliipatia timu yake bao la kwanza dakika ya saba ya mchezo kwa shuti kali la kimo cha mbuzi lililomshinda mlinda mlango wa SC Villa Elugant Martin akiduwaa asijue la kufanya.
Dakika ya 18 ya mchezo mshambuliaji Ndaula Moses aliipatia SC Villa bao la kusawazisha kwa kichwa kufuatia krosi iliyopigwa na Ronald Muganga kumkuta mfungaji na kuukwamisha mpira wavuni huku walinzi wa Yanga wakitegeana na kumtazama mfungaji.
Nahodha wa timu ya Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' aliipatia timu yake bao la pili kwa mkwaju mkali kufuatia mpira wa adhabu aliosogezewa na Haruna Niyonzima kumshinda mlinda mlango wa SC Villa akiwa amesimama na mpira kujaa wavuni na kuhesabu bao la pili kwa watoto wa Jangwani.
Dakika tatu baaadaye dakika ya 30, mshambuliaji Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao tatu akimalizia mpira uliopigwa na Jerson Tegete kugonga mwamba wa juu na kumkuta Kavumbagu aliyeukwamisha wavuni mpira huo.
Mpaka timu zinakwenda mapumziko, Young Africans 3- 1 SC Villa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na katika dakika ya 62 ya mchezo kiungo Haruna Niyonzima aliipatia Young Africans bao nne kwa ustadi wa hali ya juu akiitumia vizuri pasi aliyopewa na mshambuliaji Huseein Javu na kuufanya ubao wa matanagazo usomeke 4-1.
Yanga ilifanya mabadiliko amabapo waliingia Rajab Zahir, Hussein Javu, Bakari Masoud, Said Bahanuzi na Oscar Joshua kuchukua nafasi za Kelvin Yondani, David Luhende, Athuman Idd 'Chuji', Jerson Tegete na Haruna Niyonzima.
Hussein Javu nusura aiipatie Young Africans bao la dakika ya 72 ya mchezo baada ya mpira alioupiga kugonga mwamba wa juu kabla ya kuokolewa na walinzi wa SC Villa ya Uganda.
SC Villa ilijaribu kusaka mabao lakinu umakini wa walinzi wa Yanga ulikuwa kikwazo kwao muda wote wa mchezo huku golikipa Ally Mustapha 'Barthez' akikoa mabao mawili ya wazi kutoka kwa mshabuliaji Ronald Muganga.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 4 - 1 SC Villa.
Mara baada ya mchezo wa leo kikosi cha Young Africans kitaendelea na mazoezi kesho asubuhi katika viwanja vya shule ya sekondari Loyola kujiaanda na mchezo wake wa Ngao ya Hisani dhidi ya wana lambalamba timu ya Azam FC mchezo utakaochezwa tarehe 17.08.2013 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
Young Africans: 1.Ally Mustapha 'Barthez', 2.Juma Abdul, 3.David Luhende/Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub 'Cannavaro' 5.Kelvin Yondani/Rajab Zahir, 6.Athuman Idd 'Chuji/Bakari Masoud, 7.Mrisho Ngassa, 8.Salum Telela, 9.Jerson Tegete/Hussein Javu, 10.Didier kavumbagu, 11.Haruna Niyonzima/Said Bahanuzi
Source:www.youngafricans.co.tz
إرسال تعليق