Chadema yaipiga bao CCM

MAHAKAMA ya Rufaa imeombwa kutupilia mbali rufaa ya kesi ya ubunge, inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kutokana na mlalamikaji wa kwanza, Shaaban Itemba, kuhamia Chadema. Rufaa hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa leo katika Mahakama ya Rufaa mjini Dodoma na Jopo la Majaji watatu, ambao ni Jaji Salum Massati, Jaji Engela Kileo na Natalia Kimaro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, wakili aliyekuwa anasimamia rufaa hiyo, Godfrey Wasonga, alisema tayari ameshatoa notisi kwa Msajili wa Mahakama ya Rufaa kuomba kuondolewa kwa kesi hiyo.

Wasonga alisema, mlalamikaji huyo ameonyesha kutokuwa na nia ya kuendelea na rufaa hiyo na ametoa siri zote za jinsi kesi hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa,” alisema Wasonga.

Lissu aliwashinda mlalamikaji huyo pamoja na wenzake wawili katika kesi ya kupinga ubunge wake katika Jimbo la Singida Mashariki.

Wakazi wawili wa Kijiji cha Makiungu mkoani Singida, Shaaban Itemba na Paskali Hallu, ambao walifungua kesi ya msingi kupinga ubunge wa Lissu, tayari walikwishabainisha kuwa wapo tayari kukubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Aprili, mwaka huu.

Mara kadhaa wananchi hao wamekuwa wakinukuliwa katika vyombo vya habari wakimlalamikia Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuwa anawashinikiza kuendelea na rufaa hiyo licha ya kuwa walikwishajitoa. 

Awali kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo, mahakama ilikuwa ianze kwa kusikiliza pingamizi zilizotolewa na upande wa walalamikiwa, ambao ni Lissu na Jamhuri, za kupinga rufaa hiyo na jopo hilo la majaji litatoa uamuzi.

Upande wa wakatiwa rufaa ulikuwa na hoja saba za kupinga rufaa hiyo, ikiwemo hiyo ya mlalalamikaji namba moja, Seleman kupinga kwamba hajakata rufaa kwa Hati ya Kiapo ya Mei 24, mwaka huu.

Hoja nyingine ni notisi ya kiapo kutopelekwa kwa mujibu wa rufaa kinyume na masharti ya 84 (1) ya Kanuni ya Adhabu za Mahakama ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.

Vilevile nakala zote rekodi ya rufaa hazijathibitishwa usahihi wao na wakala au wakili kinyume na masharti ya Kanuni ya 96 (5) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.

Rufaa hiyo pia imepitwa na muda wake kwa sababu hati ya ucheleweshaji iliyotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu haijasainiwa, haina tarehe wala muhuri kinyume na Kanuni ya 90 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania za mwaka 2009,” alisema Lissu.

Walalamikaji walitakiwa kukata rufaa siku sitini baada ya notisi ya rufaa kutolewa na kwamba tarehe ya mwisho ya kukata rufaa ilikuwa Julai 3 mwaka jana na kwamba rufaa hiyo ilikatwa Mei 7, mwaka huu.

Hoja nyingine ni kwamba rufaa hiyo si halali, kwa kuwa imeacha nyaraka muhimu, ikiwemo maombi ya mwenendo wa shauri wa kusamehewa gharama za dhamana.

Pia katika rufaa hiyo, amri iliyomshindisha kesi si halali, kwa kuwa haionyeshi tarehe ambayo amri hiyo ilitolewa kinyume na kanuni ya 9 ya Kanuni za Masijala za Mahakama Kuu za mwaka 2005.

Wakata rufaa pia wameshindwa kuwasilisha mahakamani hoja za maandishi za kuunga mkono hoja za rufaa yao ndani ya siku 60 au kuomba muda wa kuziwasilisha.

Post a Comment

Previous Post Next Post