RAIS TENGA AIPONGEZA KAMATI YA LIGI
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita.
Amesema
TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa lengo la kutaka klabu
zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta
mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa na
makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
“Fedha
za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya Ligi. Ni
matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani tumeanzisha jambo hili
kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema Rais Tenga
wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya
habari.
Rais
Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala bora watu wanakuwa na
imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa kampuni kuwekeza
kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.
Amesema
ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika ukanda huu wa Afrika Mashariki,
Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo yenye udhamini mkubwa
kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya televisheni.
Pia
amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu hazitaruhusiwa
kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za mapato na
matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika zijiandae
kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.
Kuhusu
tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema bado linafanyiwa kazi na CRDB
ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko katika hatua nzuri, kwani
nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka iwezekanavyo.
“Tiketi
za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika,
lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika karibu viwanja vyote.
Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za kuchapia),
zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system
(mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia
uwezekano wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa
una system yake tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala
lisitucheleweshe,” amesema.
WACHEZAJI 620 WATHIBITISHIWA USAJILI FDL
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya 624 wa
timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza kutimua vumbi kesho
(Septemba 14 mwaka huu).
Wachezaji
wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka watakapokamilisha taratibu ni
Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon, Godfrey Bonny Namumana
(Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth Chukwu wote wa Mwadui
FC ya Shinyanga.
Darlington
na Chukwu ambao wote ni Wanigeria wamezuiwa mpaka watakapowasilisha
vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji wakati Namumana
aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC).
Nayo
African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA Academy ambayo Namwando
anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia mchezaji huyo.
Klabu
ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili katika FDL ni Friends Rangers
FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya Shinyanga wakati iliyosajili
wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu hiyo ya Morogoro
imesajili wachezaji 19 tu.
Vilevile
Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili wa wachezaji wanane wa klabu
za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika hatua ya pili ya
usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.
Wachezaji
hao ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United), Robert Machucha na
Said Ndutu (Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani (Coastal
Union U20), Ramadhan Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba)
ambaye tayari Hati yake Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.
YANGA YAPEWA SIKU 14 KUWALIPA AKINA NSAJIGWA
Yanga
imepewa siku 14 kuanzia leo (Septemba 13 mwaka huu) kuwalipa waliokuwa
wachezaji wake msimu uliopita, nahodha Shadrack Nsajigwa na Stephen
Mwasika wanaoidai klabu hiyo jumla ya sh. milioni 15.5.
Uamuzi
huo umefanywa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Septemba 12 mwaka
huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilisikiliza madai ya wachezaji hao.
Fedha
hizo ni ada ya usajili ambayo klabu hiyo ilikubaliana na wachezaji hao
wakati ikiwasainisha mikataba. Yanga imeshawalipa sehemu ya fedha
walizokubaliana na kiasi hicho ndicho bado hakijalipwa. Nsajigwa anadai
sh. milioni 9 wakati Mwasika ni sh. milioni 6.5.
SIMBA UWANJA WA TAIFA, YANGA IKO MBEYA VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu kesho (Septemba 14 mwaka
huu) kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio ya washabiki wengi
yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na ile kati ya
Mbeya City na Yanga.
Simba
inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika
mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na kijani,
sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A
itakuwa sh. 20,000.
Pia
Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya mazoezi (broadcast training)
kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo haitarekodiwa au kuoneshwa moja
kwa moja.
Katika
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, shughuli itakuwa kati ya
mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC. Mwamuzi Andrew
Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna wa mechi
hiyo James Mhagama kutoka Songea.
Mechi
nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na Tanzania Prisons (Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting (Uwanja wa Mabatini
mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja wa
Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex,
Dar es Salaam).
MJINI MAGHARIBI KUCHEZA FAINALI COPA
Mjini
Magharibi imepata tiketi ya kucheza fainali ya michuano ya Copa
Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 upande wa wavulana
baada ya kuing’oa Temeke kwenye nusu fainali iliyochezwa leo (Septemba
13 mwaka huu) asubuhi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es
Salaam.
Ushindi
wa mabao 2-0 yaliyofungwa dakika za 30 na 63 kupitia Juma Ali Yusuf
ndiyo yaliyoipa Mjini Magharibi tiketi ya kucheza fainali itakayofanyika
kesho (Septemba 14 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia
saa 9 alasiri.
Mjini
Magharibi itacheza fainali hiyo na mshindi wa nusu fainali ya pili
inachezwa leo jioni kwenye uwanja huo huo kati ya mabingwa watetezi
Morogoro na Ilala.
Kwa
upande wa wasichana Ilala imetinga fainali baada ya kuifunga Kinondoni
mabao 2-0 katika nusu fainali ya kwanza. Mabao ya washindi yalifungwa
dakika ya 27 na Fatuma Bahau wakati Happiness Lazoni alifunga la pili
dakika ya 39.
Nusu fainali ya pili kwa wasichana itakuwa kati ya Mwanza na Mbeya.
30 WAITWA KAMBINI TWIGA STARS
Kocha
Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage ameita kambini kikosi cha
wachezaji 30, wengi wao wakiwa vijana ikiwa ni mwendelezo wa programu ya
kujenga timu hiyo.
Kambi
hiyo itakuwa jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 15 hadi 26 mwaka
huu. Vijana wengi wamejumuishwa ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kuandaa timu
itakayocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 20.
Kaijage
amesema pamoja na malengo hayo kwa timu ya vijana, bado maana kubwa
inabaki kuandaa Twiga Stars iliyo imara kwa ajili ya mashindano
mbalimbali ya kimataifa.
Amesema
Twiga Stars haikabiliwi na mashindano yoyote mwaka huu, hivyo lengo ni
kuijenga upya ndiyo maana haichezi michezo ya kimataifa ya kirafiki hadi
itakapofika wakati wake.
Utaratibu
huo ulianza kuanzia kambi ya Machi mwaka huu, na ndio umezaa timu ya
vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambayo sasa itashiriki mashindano ya
Kombe la Dunia.
Wachezaji
walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden, Pwani), Asha Rashid (Mburahati
Queens, Dar es Salaam), Belina Julius (Lord Barden, Pwani), Donisia
Daniel (Lord Barden, Pwani), Esther Chabruma (Sayari Queens, Dar es
Salaam), Eto Mlenzi (JKT, Dar es Salaam) na Evelyn Sekikubo (Mburahati
Queens, Dar es Salaam).
Fatuma
Bushiri (Simba Queens, Dar es Salaam), Fatuma Hassan (Mburahati Queens,
Dar es Salaam), Fatuma Issa (Evergreen, Dar es Salaam), Fatuma Mustafa
(Sayari Queens, Dar es Salaam), Fatuma Omari (Sayari Queens, Dar es
Salaam), Flora Kayanda (Tanzanite, Dar es Salaam) na Gerwa Lugomba
(Umisseta, Kanda ya Ziwa).
Hamisa
Athuman (Marsh Academy, Mwanza), Maimuna Hamisi (Airtel Rising Star,
Ilala), Maimuna Said (JKT, Dar es Salaam), Mwanahamisi Omari (Mburahati
Queens, Dar es Salaam), Mwapewa Mtumwa (Sayari Queens, Dar es Salaam),
Pulkeria Charaji (Sayari Queens, Dar es Salaam) na Rehema Abdul (Lord
Barden, Pwani).
Sabahi
Hashim (Umisseta, Zanzibar), Semeni Abeid (Tanzanite, Dar es Salaam),
Sharida Boniface (Makongo Sekondari, Dar es Salaam), Sofia Mwasikili
(Sayari Queens, Dar es Salaam), Tatu Idd (Lord Barden, Pwani), Therese
Yona (TSC Academy, Mwanza), Vumilia Maarifa (Evergreen, Dar es Salaam),
Yulitha Kimbuya (Marsh Academy, Mwanza) na Zena Khamis (Mburahati
Queens, Dar es Salaam).
Post a Comment