Grant aachiliwa kwa kosa la wizi

Jermaine Grant ameachiliwa baada ya viongozi wa mashtaka kukosa ushahidi wa kutosha dhidi yake
Raia Muingereza anayeshukiwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini Somalia, ameachiliwa kwa kosa la wizi wa mabavu kutokana na tukio lililoripotiwa mwaka 2008.
Viongozi wa mashtaka walikosa kuthibitisha kuwa mshukiwa huyo Jermaine Grant kutoka Mashariki mwa London alitenda kosa hilo.
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani mnamo tarehe 23 Septemba kwa makosa mengine ya ugaidi.
Polisi wa Kenya wanadai kuwa Grant alifahamiana na mkewe mwanachama wa Al Shabaab aliyehusika na mashambulizi ya London mwaka 2008.
Grant tayari amehudumia kifungo cha miaka miwili na nusu kwa kuwa nchini Kenya kinyume na sheria.
Aidha Grant alihukumiwa katika mahakama mjini Nairobi, kwa madai ya kushambulia kituo cha polisi karibu na mpaka wa Somalia mwaka 2008.
Genge linaloshukiwa kuwa wanachama wa Al shabaab, lilishambulia kituo cha polisi na kumwachilia huru bwana Grant baada ya kukamatwa na polisi akijaribu kuingia nchini Somalia.
Genge hilo lilidaiwa kuiba bunduki na gari la polisi huku wakiwajeruhi polisi kadhaa wakati wa shambulizi lao.
Polisi wanadai kuwa wakati walipovamia nyumba ya Grant , walimkuta na vifaa vya kutengeza maguruneti, ikiwemo gesi za hydrogen peroxide na ammonium nitrate, pamoja na betri , madai anayokanusha Grant.
Mwaka jana mwendesha mashtaka Jacob Ondari alidai kuwa Grant alishirikiana na Samantha Lewthwaite, mjane wa mlipuaji aliyefanya mashambulizi mjini London Jermaine Lindsay kuhusu mpango wa kufanya mashambulizi.
Bi Lewthwaite anasakwa na polisi wa Kenya kwa madai ya kutumia stakabadhi bandia za usafiri.
- Bbc

Post a Comment

Previous Post Next Post