TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARYPRESS RELEASE
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitahidi kuimarisha
uchunguzi wa matukio ya watu kumwagiwa tindikali ili wahusika wapelekwe
kwenye vyombo vya sheria.
Dk. Shein ametoa wito huo leo huko hospitali la Mnazi Mmoja mjini Unguja
alipokwenda kumjulia hali Padri Anselmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki,
Machui Unguja, ambae amelazwa katika hospitali hiyo kufuatia kumwagiwa
tindikali jana jioni.
“hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee... ni lazima Jeshi la Polisi
lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake”
alisisitiza Dk. Shein.
Amekieleza kitendo hicho kuwa ni cha kikatili na kisichovumika na
kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Dk. Shein amesema amesikitishwa na kitendo hicho na kumpa pole Padri
Mwang’amba na kumuomba Mwenzi Mungu ampe nafuu haraka apone ili endelee
kuitumikia jamii.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo nje ya Wodi alipolazwa Padri huyo
Dk. Shein aliwataka waumini hao kuwa na subira wakati Serikali ikichukua
hatua kukabiliana na kitendo hicho.
“Ni jambo la kusikitisha kumfikisha binadamu wenzako katika hali kama
hii ya majonzi. Hakuna anayeyataka haya. Tuwe wastahamilivu Serikali
tunachukua hatua”aliwaambia waumini hao.
Akizungumzia hali yake, Padri Mwang’mba alimueleza Rais kuwa hali yake
ni nzuri na anaona vizuri lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya
uvimbe kupungua sehemu za machoni.
“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri
zaidi” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake
hakuathirika sana.
Amefafanua kuwa tukio hilo lilitokea eneo la Mlandege jioni wakati
akitoka katika ofisi moja inayotoa huduma za intaneti/mtandao katika
eneo hilo ndipo akatokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi
akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk. Jamala Adam Taibu
amesema alipofikishwa katika hospitali hiyo Padri Mwang’amba alipatiwa
huduma zote muhimu za matibabu zinazostahiki.
Kuhusu majeraha aliyopata Dk. Jidawi alieleza kuwa kwa ujumla asilimia
30 ya mwili wa Padri Mwang’amba umeathirika na kidogo sehemu za macho.
Chanzo - ZanziNews
Post a Comment