Mshikamano
wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya Bunge na sasa vyama hivyo
vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla
ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Jana
wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe
(Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) walikutana na waandishi wa
habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada huo kuwa sheria,
hadi pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Walisema
muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi
wa kunusuru walichokiita “utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa
wananchi” hivyo wanaitaka Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza
katika mchakato huo.
Akitoa tamko
la pamoja kwa niaba ya viongozi wenzake, Profesa Lipumba alisema
wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma,
kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Rais
Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho
yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa
mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona ila aurejeshe
bungeni,”alisema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato
huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya,
ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii
ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko,
migogoro na hata machafuko.”
Mwenyekiti
huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya watu, hivyo mchakato huo haupaswi
kuhodhiwa na chama kimoja, badala yake unapaswa kuwa shirikishi na
jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa Katiba katika msingi wa maridhiano.
Kuna madai
kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika
kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu mamlaka ya Rais
kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.
Madai
mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia
majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa
na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa
wajumbe husika.
Itakumbukwa
kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia wingi wao kupitisha
muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha
Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge
kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Katika
tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na
maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa
Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Mbowe na Mbatia
Kwa upande
wake, Mbowe alisema: “Amani itavurugwa kama mchakato wa Katiba Mpya
utahodhiwa na chama kimoja cha siasa, ikiwa hivyo sisi hatutakubali kuwa
kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani
ni lazima haki iwepo.”
Alisema
fursa ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na watu wachache ndani ya CCM, na
kwamba wapinzani watatumia kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania
kinachoendelea, ili washiriki katika kuidai Katiba iliyotokana na mawazo
yao.
Mbowe alisema wapinzani hawatarudi nyuma na hawatakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa Katiba ya sasa.
“Mwalimu
Nyerere aliwahi kuandika katika kitabu chake kwamba, ‘kuna siku wananchi
watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa makini’. Amani itaharibiwa na
wale wenye dola, sio vyama vya upinzani” alisema Mbowe.
Kwa upande
wake, Mbatia alisema: “CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania
kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini
Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo. CCM inaweza kufa,
lakini Tanzania itaendelea kubaki.”
“CCM
wakisema wapinzani tunafanya vurugu wanakosea, katika taifa hili
Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao. Katiba
Mpya ni tendo la maridhiano na kisiasa sio kisheria, sisi tuna tofauti,
lakini tumeziweka pembeni.”
Mbatia
alimtaka Rais Kikwete kusimamia kikamilifu mchakato wa Katiba ili
historia isije ikamhukumu. “Yeye ndio ameanzisha mchakato huu wa kupata
Katiba Mpya, aweke masilahi ya taifa mbele sio masilahi ya chama chake
cha siasa, CCM haiwezi kuwa juu ya dola na Serikali, asisaini
marekebisho ya Katiba yaliyofanyika bungeni,”alisema Mbatia na kuongeza:
“Mkono wa Rais usilitumbukize taifa la Tanzania katika machafuko,
kwanza hagombei tena urais wala uongozi ndani ya chama chake, sasa
anamwogopa nani.”
Vyama hivyo
pia vimetangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la
kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa ni ‘hujuma dhidi ya
upatikaji wa Katiba Mpya’.
Mikutano
hiyo itaanzia Septemba 21 mwaka huu, katika Viwanja vya Jangwani, Dar es
Salaam na baadaye viongozi hao watakutana na makundi mbalimbali
yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa,
wasomi na taasisi za elimu.
Makundi
mengine ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima,
wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu wenye ulemavu, jumuiya za
wanawake, vijana na wastaafu.
Post a Comment