Mara
kadhaa nimesikia malalamiko fulani kutoka wa watayarishaji wa muziki wa
bongo hususani watayarishaji wachanga, uchanga kwa maana kwamba hawana
muda mrefu kwenye hii tasnia lakini pia wenye muda mrefu lakini
hawajapata fursa ya kuwa miongoni watayarishaji wanaofuatwa sana na
superstars na pia majina yao kutotajwa na kuzungumziwa sana katika
vyombo vya habari hapa nchini.
Malalamiko ama niyaite manung’uniko yanayotawala zaidi vinywa vyao ni
kusahauliwa na wasanii waliofikishwa mbali na nyimbo walizozitayarisha
wao, kama ilivyo mara nyingi watayarishaji hawa ndio huwaomba
superstars kuingiza maneno yao kwenye beats zao, hili limetawala zaidi
mikoani pindi wasanii wafikapo kwa ajili ya matamasha.
“Palipo na ulaji hapakosi maneno”…huu ni msemo wa kale lakini
usiozeeka kwakuwa nguvu yake yaonekana katika kila nyanja ihusishayo
‘chochotekitu’, zungumzia siasa, zungumzia biashara, lakini pia
zungumzia muziki (nyanja ambayo mimi nimeshawishika kuidadavua hapa).
Muziki kwa kiasi kikubwa hivi leo umekuwa na fursa nyingi sana
tofauti na zamani, wapo wanaotumia fursa hizo vizuri lakini pia wapo
ambao mpaka leo wako nyuma kimawazo, hii inamaanisha kupoteza nafasi
nyingi ambazo laiti kama wangezizingatia mapema basi wangeyaona na
kuyatafuna matunda ya kazi zao.
Naamini kinachokuwa kichwani mwa mtayarishaji wakati anafanya beat ya
wimbo ni kufanikiwa kwa wimbo huo tunasema ana “visualize” mafanikio.
Kubwa ambalo analiweka kichwani kwa wakati ule ni wimbo kupigwa na
kupendwa kisha yeye kujulikana zaidi, nimekaa na watayarishaji wengi wa
aina hii na kwa kuwasoma mind zao nikaona kabisa kwamba fedha si kitu
wanachowaza kwa wakati ule.
Wimbo unatoka na unapendwa (kama mtayarishaji alivyotamani) lakini
anakosa kuzungumziwa sana kwenye vyombo vya habari pindi wimbo
uzungumziwapo (tofauti na matarajio yake), maneno yanaanza chinichini
kuwa kafanya ngoma lakini hasikii kuzungumziwa yeye pindi wimbo na
msanii wazungumziwapo, naambiwa kwenye soko kila mtu anatakiwa kufanya
lake ili kupata publicity.
Msanii yeye sifa yake inaimarika, anapata shows na matangazo ya
kufanya, anaingiza wimbo kwenye makampuni ya simu na hatimaye labda
anakuwa awarded kutokana na wimbo huohuo (vitu ambavyo mtayarishaji
hakuvifikiria awali), na hapo ndipo manung’uniko yanapoanza kupamba
moto, producer anakosa morali ya kufanya kazi na anaishia tu kuingiza
mamoshi na vinywaji vikali mwilini mwake.
Pesa haijawahi kutosha hata siku moja ndio maana matajiri wadunia
bado wanazisaka, mtayarishaji usitegemee Msanii akupe pesa baada ya
mafanikio hayo kwakuwa naye anamatatizo yake kibaaaoo!!! Wachache sana
wanaweza kukukumbuka wakati wanazivuna.
Kuanzia leo mtayarishaji nataka nikufungue macho ya upeo wako ili
uone ambavyo havionekani kwa macho ya kawaida, ukishaona basi uchukue
hatua lakini pia utafute vingine ambavyo mimi sitokuonyesha.
UNGEanza kukithamini kiti unachokalia, kipe heshima
kwakuwa ofisi yako ndio kiwanda cha kutengenezea fedha za kuendeshea
maisha yako. Ni wazi ukiipa heshima ofisi yako basi kila mtu anayetia
mguu atakuheshimu lakini pia ataheshimu kazi ya mikono yako.
UNGEpata ushauri kisheria ya namna gani unaweza kuwa
na haki ya kila kazi unayofanya hususani zile unazofanya bure. Bure
yako iwe bure kwa muda ule tu nikimaanisha kuwa uwe umewekeza.
Tengenezewa mikataba ambayo wewe na msanii unayemfanyia wimbo bure
mtasaini, walau kuwe na asilimia fulani ambayo utaipata pindi wimbo huo
uingizapo hela kwa namna yoyote (wanasheria watakueleza vizuri).
Hii itapoteza manung’uniko yako ambayo naweza sema ni makosa yako
mwenyewe from the first place. Nina mfano mzuri wa wimbo wa Kala
Jeremiah ambao aliutengeneza Deey Classic ambaye kipindi hicho alikuwa
studio za rock town Mwanza. Wimbo umemuibua Kala kutoka alipokuwepo na
nathubutu kusema ndio wimbo uliompa mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi
kuliko nyimbo zake zote, lakini vipi kuhusu mtayarishaji??? Malalamiko
tu.
Rafiki yangu Sappi ni producer mdogo kiumri lakini ameshafanya
makubwa nchini Kenya yeye akiwa ni Mtanzania pekee kwenye studio za
HomeBoys. Yeye nilimuuliza mambo yalivyo huko akanijibu “Game ya huku ni
professional hakuna mtu anaye record bure unless producer ametaka
mwenyewe but mnasign contract before kazi ianze.” Nilimdodosa kidogo
kuhusu asilimia ngapi producer ananufaika kwa mikataba ya aina hiyo
akaniambia 60%…nikashtuka kidogo.
UNGEweka nguvu katika kutoa kazi nzuri zitakazoiweka
cv yako vizuri. UNGE ya hapo juu haitokuwa na nguvu kama wewe ndio
unambembeleza msanii. Hakika ni ngumu kumbembeleza ufanye nae kazi kisha
kumpa mikataba asaini. Lakini ubora wa kazi zako ndio silaha yako kubwa
ya kumshikisha Msanii kalamu na kusaini.
Niliona mkwaruzano wa Lucci na Chidi Benz kwenye swala hilihili
katika mitandao, kwa waliousikia wimbo alioufanya chidi kwa lucci
wanasema ni boonge la ngoma, lakini inaonekana Lucci akaintroduce swala
la kisheria baadae kabisa kitu ambacho Chidi anasema si sahihi kwakuwa
Lucci ndiye aliyemuita studio kwake na mpaka anafanya wimbo hakuambiwa
kuhusu masuala ya kusaini. Lucci did the right thing ila alikosea
procedures.
UNGEhifadhi kazi zako vizuri, sio wimbo
haujakamilika ushatoa demo zaidi ya saba. Kwanini usiwe na msimamo hata
kama ni msanii ndio anataka. UNGEmwambia utaratibu wa ofisi yako ni
kutotoa wimbo kabla haujakamilika, hakika atasikiliza na kuheshimu.
Nasema hili kwasababu mara kadhaa imetokea beat uliyofanya wewe msanii
anaenda kuirudia kwa mtu mwingine na kufanya sauti upya.
Lakini pia mazingira tofauti kidogo ya hali hii ni kumpa msanii wimbo
kabla hamjamalizana, somo hili alilifaulu sana Hermy B wa BHitz, sijui
ni wangapi mlifuatilia sakata lake na AY na FA? Mambo hutakiwa kuwa
vile, unataka chako basi twende nionavyo ni sahihi kwangu kama
mtayarishaji, lakini kama angekuwa ni mtu wa kugawagawa tu nyimbo ni
wazi kuwa ingekula kwake.
UNGEtanua wigo wa kazi zako kusikilizwa. Mtandao
umerahisisha mambo mengi sana siku hizi, na kama unavyojua ni ngumu sana
kuwafikia watu muhimu ili wasikie ufanyacho, ni wakati sasa wa
kujihusisha na mitandao kama soundcloud, hulkshare, revernation, myspace
na mingine mingi ambayo unaweza ukashare kazi zako na kupata nafasi
zaidi.
UNGEhakikisha una identity, sizungumzii sauti
unayoweka mwanzo na mwisho wa nyimbo unazofanya lah, nazungumzia
utofauti wa midundo yako na ya watayarishaji wengine. Nampenda
mtayarishaji huyu wa nje anaitwa Liam Geddes, yeye ni mchanga lakini ana
ushauri mzuri kwako, anasema “keeping positive is essential, things
take time to be released which can be a pain. Always try to make
something original and different to the last track you made. Practice
really makes perfect as well!”
Kama nilivyosema awali, nayafungua tu macho yako na kukuonyesha
vichache, nakushauri kutazama mengine ya kukunufaisha kutokana na kile
ukifanyacho, utalalamika mpaka lini? Kila la kheri na Mungu aendelee
kuibariki mikono yako.
Imeandikwa na Kinye: Kinye42@gmail.com
@kinye42
@kinye42
Post a Comment