Kesi
inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa
Ponda, jana ilitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro bila
mshitakiwa kuwako mahakamani, hali iliyoibua hisia kuwa serikali
imekwepa gharama za kumsafirisha mtuhumiwa kutoka Dar es Salaam kwenda
Morogoro na kurejea kama ilivyofanya mara mbili.
Ponda wakati anasomewa mashitaka yake kwa mara ya kwanza mahakamani hapa Agosti 18, mwaka huu alisafirishwa kwa helikopta ya polisi na kurejeshwa Dar es Salaam, huku viunga vya mji wa Morogoro vikiwa vimetanda polisi waliojihami kupambana na ghasia.
Ponda wakati anasomewa mashitaka yake kwa mara ya kwanza mahakamani hapa Agosti 18, mwaka huu alisafirishwa kwa helikopta ya polisi na kurejeshwa Dar es Salaam, huku viunga vya mji wa Morogoro vikiwa vimetanda polisi waliojihami kupambana na ghasia.
Agosti 28, mwaka huu, serikali pia iliingia katika gharama kwa mara ya pili kwa kumsafirisha Sheikh Ponda kwenda mahakamani mjini Morogoro kwa kutumia basi la Jeshi la Magereza kutoka jijiji Dar es Salaam ambako anashikiliwa katika gereza la Segerea kwa ajili ya kesi hiyo na kumrejesha tena Dar es Salaam.
Jana kesi hiyo baada ya kutajwa bila Sheikh Ponda kuwapo mahakamani iliahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu, itakapotajwa tena.
Sheikh Ponda anashitakiwa kwa uchochezi, kuharibu imani za watu wengine na kushawishi kutendeka kwa kosa.
Wakati kesi hiyo ikitajwa na Mwanasheria wa Serikali, Gloria
Rwakibarila, mbele ya Hakimu Agnes Ringo, na kuahirishwa hadi Jumanne
ijayo, mahakama hiyo itakapotoa uamuzi wa kumpa dhamana au la, baadhi ya
wafuasi wa Sheikh Ponda waliokuwa nje ya uzio wa mahakama walikuwa
hawajui kilichokuwa kikiendelea dhidi ya kiongozi wao kwa kuwa
ilifanyikia katika chemba.
Hali hiyo ilimlazimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard
Kabate, kutoka nje ya ofisi yake na kwenda kuwaeleza wafuasi hao sababu
za kutofikishwa kwa kiongozi wao huyo mahakamani hapo jana.
Hakimu Kabate aliwaambia kuwa kesi hiyo haikutajwa katika mahakama ya
wazi kwa sababu ilikuwa inatumika kuendesha vikao vya Mahakama Kuu.
Aliwataka wafuasi hao kuondoka mahakamani hapo mpaka wiki ijayo kiongozi
wao atakapofikishwa mahakamani kwa ajili ya kujua hatma ya dhamana
yake.
Baada ya Hakimu huyo kutoa ufafanuzi huo, wafuasi hao walitawanyika kwenye viwanja vya mahakama.
Waandishi wa habari walipomuuliza hakimu huyo sababu za Sheikh Ponda
kutofikishwa mahakamani kusikiliza kesi yake ikitajwa, alisema
hakukuwapo na umuhimu wa kuwapo mahakamani kwa kuwa ilikuwa ni kwa ajili
ya kutajwa tu. Hata hivyo, Hakimu Kabate alisema kuwa mshitakiwa huyo
atalazimika kuwapo mahakamani Jumanne ijayo kesi hiyo itakapoitishwa kwa
ajili ya kuamua hatma yake ya dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Ponda anayetetewa na mawakili watatu
wakiongozwa na Wakili Juma Nassoro, anadaiwa kutenda makosa hayo Agosti
10, mwaka huu jioni eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na mawakili wake wamewasilisha
ombi la dhamana na mahakama itatoa maamuzi Jumanne ijayo baada ya
kupitia vifungu vya sheria.
NIPASHE jana lilipomuuliza Wakili Nassoro sababu za kutokwenda Morogoro
wakati kesi ya mteja wake ikitajwa, alisema kuwa jana ilienda kwa ajili
ya kutajwa kwa hiyo hakukuwa na umuhimu sana wa kwenda mahakamani.
Hata hivyo, aliongeza kuwa hajui sababu ya Sheikh Ponda kutopelekwa mahakamani pengine kwa sababu ilikuwa kwa ajili ya kutajwa.
SOURCE: NIPASHE
إرسال تعليق