Majibu ya Dk Reginald Mengi kuhusu hoja ya vitalu vya gesi, mafuta

Picture
Reginald Mengi
Septemba 7, 2013 nilipokea barua pepe (email) yenye kichwa cha habari kisemacho “ubinafsi/ufisadi wa MENGI na Chuki/Fitina kwenye Maendeleo”.

Aliyetuma email hiyo alijitambulisha kama “CCM TANZANIA” na email ilisambazwa kwa vyombo vya habari, waandishi na watu wengine wengi wakiwamo wanasiasa. Kabla ya hapo nilifowadiwa nakala ya ujumbe (SMS) na watu ambao walitumiwa na Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge inayosema;

“Ambieni Watanzania: Kampuni za Mengi zimeshikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa mita za mraba 3,752.37 (sq km) Amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza. Watanzania wanakosa mapato na ajira! Sasa 
anataka vitalu vya gesi na mafuta. Je huu ndio uzawa?”

Na

“Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali wa vitalu vya raslimali zetu. Waelezeni Watanzania ukweli huu.”

Vile vile Septemba 5, 2013 Profesa Muhongo akijibu swali la Mwandishi wa habari lililouliza;

“Mhe. Waziri tunataka ufafanuzi kuhusu kauli yako ya hivi karibuni kwamba waTanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika uwekezaji wa gesi asilia. Kwanza kauli hii ni kweli? Pili kauli kwamba   Watanzania wanaweza kuwekeza kwenye sekta ya machungwa tu huoni kwamba si kwamba unawavunja moyo bali unadhalilisha wewekezaji wazalendo?”

Na Profesa Muhongo akajibu:

“Kila mtu alitoa mawazo ya sera ya gesi wakiwemo TPSF. Mengi na wenzake wanataka vitalu wafanye ulanguzi wa gesi na mafuta yetu. Tutatoa orodha ya vitalu vya madini vilivyoko mikononi wa Mengi ambavyo anafanya ulanguzi. Ukweli utaonyesha ubabaishaji na ulanguzi wa Mengi wa genge lake.”

Nimeona ni vyema nitumie haki yangu ya kujibu (right of reply), lakini kwa wale wanaohusika kusambaza taarifa hizo kuchafua jina langu wajue kwamba kujibu kwangu hakuondoi haki yangu ya kuchukua hatua za kisheria.

Kuingizwa kwa vitalu vya madini katika hoja ya gesi

Huo ni upotoshwaji wenye lengo la kututoa kwenye hoja ya msingi ya rasilimali yetu ya gesi. Sijawahi kufanya udalali kwenye vitalu vya madini. Huu ni uongo wa hali ya juu.

Tamko la TPSF na majibu ya Profesa Muhongo

Siku ya Agosti 28, 2013 Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ilifanya kikao chake cha Bodi na baadaye kufanya mkutano na waandishi wa habari. Mambo mengi yalizungumzwa katika kikao hicho ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa Watanzania (Economic Empowerment).

Kuhusu uwezeshaji Watanzania, mambo muhimu matatu yalijadiliwa na kutolewa mapendekezo. Mambo hayo ni 1) Manunuzi ya Umma (Public Procurement); 2) Ardhi na uvuvi; na 3) suala la gesi asilia.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, mimi nikiwa Mwenyekiti wa TPSF, niliwasilisha maoni ya TPSF kuhusiana na Manunuzi ya Umma, wakati Makamu Mwenyekiti wangu, Salum Shamte, aliwasilisha maoni yetu kuhusiana na sekta ya ardhi na uvuvi na mwishoni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliwasilisha maoni TPSF kuhusiana na gesi asilia.

Katika maoni yake TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi na kushauri kusitishwa ugawaji wa vitalu vya gesi hadi hapo sera ya gesi itakapokua tayari. Mwisho Bwana Simbeye alisema kwamba TPSF itaomba kukutana na Profesa Muhongo kuwasilisha mawazo na mapendekezo ya taasisi hiyo.

Siku chache baada ya TPSF kutoa maoni yake mambo mawili yalitokea. Kwanza Profesa Muhongo alijibu kupitia vyombo vya habari kwamba mpango wa kugawa vitalu vya gesi na kuingia mikataba utaendelea.

Profesa Muhongo pia alisema wazi kwamba hana mpango wa kukutana TPSF, kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda.

Matokeo yake Profesa Muhongo hajajibu hoja kuhusiana na barua aliyoandikiwa na TPSF. Binafsi nilishitushwa na msimamo wa Profesa Muhongo kwani Serikali ya awamu ya nne imepiga hatua kubwa katika kudhihirisha kuwa ni “serikali sikivu”. Ingemgharimu nini Profesa Muhongo kukaa na kutusikiliza? Hakuna ambacho angepoteza zaidi ya dakika chache za muda wake.

Jambo la pili ambalo lilitokea ni mimi binafsi kushambuliwa kana kwamba maoni yaliyotolewa kuhusiana na gesi ni maoni yangu binafsi na si ya TPSF.

Mifano ya mashambulizi dhidi yangu ni kama nilivyoonyesha hapo juu katika email na ujumbe mfupi wa simu (SMS).

Msimamo wa Profesa Muhongo katika gesi ni upi?

Msimamo wa Profesa Muhongo mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ulikuwa ni kutaka kupitishwa kwanza kwa sera ya gesi asilia kabla ya kuendelea na ugawaji wa vitalu vya gesi.

Septemba 2012, Profesa Muhongo alisema;

“Some of the agreements are really shoddy and they need to be revoked” and “I can’t tolerate agreements which are not in the country’s interests but they benefit a few individuals”.

Tafsiri yake ni:

“Baadhi ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa” na “Sitovumilia mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi na inawanufaisha wachache”. http://www.energy-pedia.com/news/tanzania/new-151679

Baada ya hapo, Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi ambao ulipangwa kufanyika mwezi Septemba 2012 na kupitia upya mikataba yote. Profesa Muhongo alinukuliwa akisema:

‘Earlier this month, the state-run Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) delayed a licensing round for nine deep-sea oil and gas blocks previously set for this month until a parliamentary vote on a new gas policy in October. "Right now as a country, we are in the gas boom and we don't have gas policy in place.”

[…]

Recent gas strikes off east Africa's   seaboard have led to predictions the region could become the third largest exporter of natural gas on the planet.

"Our country is reviewing its policy. Is that something new?" he said. "We want both the companies that are investing in the country and Tanzanians to benefit from the oil and gas projects."

[…]

"This is completely new business to us. We are learning," Muhongo said.’

Tafsiri yake ni:

‘Mwanzoni wa mwezi huu TPDC ilihairisha mchakato wa ugawaji wa vitalu tisa vya gesi asilia vilivyoko baharini hadi hapo Bunge litakapopitisha sera mpya ya gesi iliyowasilishwa bungeni mwezi Oktoba;

"Kwa sasa kama Taifa, tuko katika mazonge ya gesi na hatuna sera ya gesi.

"Nchi yetu inaandaa sera (ya gesi). Hicho ni kitu kipya?..."

"Tunataka kampuni zote, kampuni zinazowekeza nchini mwetu na Watanzania tunufaike na miradi ya gesi na mafuta."

"Hii  ni biashara mpya kabisa kwetu. Tunajifunza."

http://www.reuters.com/article/2012/09/18/tanzania-exploration-idUSL5E8KIPEJ20120918

Zoezi wa la kugawa vitalu vya gesi asilia lilisitishwa lakini hadi sasa matokeo ya kupitia upya mikataba hayajatolewa hadharani.
Picture
Miezi michache baadaye, Februari 26, 2013, Profesa Muhongo alisisitiza msimamo wake wa kutaka Tanzania kuwa na sera ya gesi kabla ya kugawa vitalu zaidi. Aliyasema hayo alipokua akihutubia mkutano uliofanyika Chatham House, mjini London. Mkutano huo uliopewa jina “Tanzania: An Emerging Energy Producer”. Ulikuwa na madhumuni ya:

“Tanzania is drawing growing attention as a pivotal country in East Africa for oil and natural gas exploration, having led the region in terms of new discoveries of natural gas in 2012. With known gas reserves of approximately 7.5 billion cubic feet, the potential to transform Tanzania's international standing and domestic electricity production is considerable. However, recent protests against the construction of a pipeline to Dar es Salaam highlight the challenges that Tanzania faces in ensuring that the benefits of its natural resources are widely felt.

Tafsiri yake ni:

“Tanzania inaonyesha kuja juu katika Afrika Mashariki kwa uvumbuzi wa mafuta na gesi asilia baada ya kuongoza kwa uvumbuzi wa gesi asilia mwaka 2012. Ikiwa na wastani wa futi za ujazo bilioni 7.5, ni dhahiri itasaidia Tanzania kupaa katika anga za Kimataifa na kusaidia uzalishaji wa umeme kwa matumizi ya ndani. Hata hivyo, vurugu za hivi karibuni kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam inaashiria changamoto mpya ambazo Tanzania sasa inakabiliana nazo kuhakikisha kwamba manufaa ya gesi asilia yanawafikia watu wengi zaidi wa chini.”

Alichowasilisha Profesa Muhongo katika mkutano huo kwa ufupi kinapatikana katika tovuti hii;
http://www.chathamhouse.org/events/view/189235

Kama inavyonekana kwenye kiambatanisho, moja ya nyaraka aliyowasilisha Profesa Muhongo inaonyesha kwamba mchakato wa kuanza ugawaji wa vitalu ungeanza baada ya kupitishwa kwa sera ya gesi.

 Hadi sasa hatuna sera ya gesi asilia.

Lakini jambo la kushangaza, Profesa Muhongo amebadilika na anataka vitalu vigawiwe kabla ya kuwapo kwa sera gesi.

Sababu za kubadilika kwa Profesa Muhongo hazina mashiko

Profesa Muhongo amenukuliwa na gazeti la Daily News la Agosti 31, 2013 akieleza sababu zake za kutaka vitalu vigawanywe kabla ya kupitishwa kwa sera ya gesi. Sababu kuu alizozisema ni tatu; (1) Ushindani wa soko na majirani zetu akitolea mfano wa Msumbiji (2) Sheria ya mwaka 1960 iliyoanzisha TPDC na Sheria ya Petroli ya mwaka 1980 kwamba zinatosha kusimamia ugawaji wa vitalu akimaanisha sera na sheria mpya zitafuata baada ya ugawaji wa vitalu; na (3) Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika sekta hii akimaanisha waachiwe wageni peke yao.

Maelezo kwamba tunashindana na Msumbiji haya halalishi ugawaji vitalu kabla ya sera. Utafiti wa gesi asilia ni jambo linachokua muda mrefu, ndio maana TPDC wanaingia kwenye mikataba ya muda mrefu (isiyozidi miaka 11 kwenye utafiti na miaka 25 kwenye uchimbaji). Kwa hiyo kusubiri miezi michache ili Bunge letu liidhinishe sera, haiwezi kuathiri ushindani wa kibiashara. Hata nchi Msumbiji anayoizungumzia hivi sasa inapitia upya mpango wake wa uwekezaji katika gesi asilia na kuingiza sera na sheria mpya zitakazo simamia rasilimali hiyo. Katika mahojiano yaliofanyika na jarida la Africa Report mwezi Julai mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati wa Msumbiji, Mh. Abdul Razak Noormahomed, alisema madhumuni ya mabadiliko hayo ni kuwapa kipaumbele wananchi wa Msumbiji.

Mohojiano haya yanapatikana katika anuani ifuatayo: 
(http://www.theafricareport.com/Interview/extractive-industry-the-goal-is-to-give-an-edge-to-mozambicans-noormahomed.html). 

Kama nilivyoeleza hapo juu, mara baada ya Profesa Muhongo kuingia wizarani alisema kinaga ubaga kwamba sheria iliyopo haikidhi mahitaji ya sekta ya gesi asilia ndiyo maana akasimamisha ugawaji wa vitalu vya gesi na kuamrisha mikataba ipitiwe upya na sera ipatikane. Leo tunashuhudia Profesa Muhongo akila matapishi yake na kusema kwamba sheria zile zile alizoziponda sasa zinafaa.

Kauli ya Profesa Muhongo kwamba wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza tu kushiriki biashara ya juisi na soda na hawana uwezo wa kushiriki katika biashara ya gesi yao ni dharau.

Kigezo gani Profesa Muhongo anatumia kutoa kauli ya jumla yenye kutawaliwa na hisia? Amefanya utafiti gani kupima uwezo wa kifedha wa wafanyabiashara wa kitanzania? Kwa taarifa yake, wapo wafanyabiashara wengi ambao wanaweza kupata fedha kwa ajili ya kuchimba visima vya gesi. 

Ni dhahiri kwamba Profesa Muhongo anathamini tu kampuni za kigeni, anasahau kwamba kuna mifano ya kuwapo kampuni za kigeni ambazo zimekua zikifanya udalali hapa nchini kwa miaka mingi kwenye rasilimali za nchi yetu ikiwa ni pamoja na madini na gesi.

Uzalendo wangu:

Ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi si mzalendo Wantanzania wanafahamu ukweli. Vile vile ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi ni mbinafsi na sipendi maendeleo ya Watanzania wenzangu kwa hili pia Watanzania wanafahamu ukweli

Kuhusu Kilimanjaro Hoteli na mgogoro na Yussuf Manji n.k, mtizamo wako unategemea wewe upo katika kundi lipi kati ya kundi safi la waadilifu au kundi chafu la wala rushwa. Watanzania wanafahamu msimamo wangu kwenye hili.

Mimi sipingi kuwepo kwa wawekezaje wageni katika sekta ya gesi lakini kuna mambo mawili napigania. Kwanza Watanzania wanufaike na rasilimali yao ya gesi na pili iwepo sera ya gesi inayotoa kipaumbele kwa Watanzania

Mimi napenda maendeleo ya nchi yangu; kwa hiyo hata siku moja siwezi kupinga uwekezaji ama ubia na wawekezaji. Ninachosimamia ni manufaa kwa nchi yangu.

Tuhuma kwamba nafanya kampeni dhidi ya Wizara

Tuhuma kwamba nimeandaa kongamano kwa ajili ya vijana wa Chadema si za kweli. Huu ni uzushi usio na kichwa wala miguu. Vile vile madai kwamba naitumia vibaya vyombo vya habari vya IPP Media si ya kweli hata kidogo ikizingatiwa kwamba hata mahojiano ya Profesa Muhongo kwa simu akiwa Austria, yalirushwa na kituo cha redio cha Radio Stereo kinachomilikiwa na kampuni yangu ya ITV-Independent Television Limited.

Hitimisho

Julai mwaka huu, Rais wa Marekani Barack Obama, alihitimisha ziara yake ya Kiserikali nchini Tanzania, kwa kusema;

“Ultimately the goal here is for Africa to build Africa for Africans.”

Akimaanisha kwamba, Hatimaye Lengo ni Africa kujenga Africa kwa ajili ya Waafrika                                 

Profesa Muhongo asipingane na ushauri huu mzuri.

Nimalizie kwa kuwahakikishia Watanzania kwamba mashambulizi binafsi dhidi yangu yenye nia mbaya ya kunishushia heshima hayatakaa yafanikiwe.

Wenu,

Dk. Reginald A. Mengi

Post a Comment

Previous Post Next Post