ALISIMAMA kutoa hoja, hakupewa fursa; akaambiwa akae chini. Hakukaa.
Akaambiwa atoke nje; hakutoka. Wakaitwa askari kumtoa kwa nguvu, ukazuka
mzozo uliozaa masumbwi bungeni.
Ni kauli gani ambayo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitaka kutoa?
Vyanzo vyetu vya habari vilivyo karibu na Mbowe vilimnukuu jana akisema alichotaka kusema, akazuiwa na Naibu Spika, Job Ndugai, ni hiki hapa:
“Kwanza, nilichotaka kusema ni kutoa hoja ya kuomba shughuli za Bunge
zisitishwe kwa muda ili Kamati ya Uongozi ya Bunge ijadili makandokando
yote ambayo yalikuwa yametokea juu ya muswada huo, ukiwamo uongo wa
mwenyekiti wa kamati ya Bunge, uongo wa serikali bungeni na masuala
mengine yote, ili sasa Bunge lipate mwelekeo chanya juu ya muswada huo
na mchakato mzima wa Katiba Mpya kwa masilahi ya wananchi.
“Hivyo hoja yangu ilikuwa muhimu sana kusikilizwa, ili viongozi wakutane
kuokoa jahazi na kuondoa sintofahamu ambayo hatimaye imesababisha
mjadala mkubwa na muswada mbovu kupitishwa bungeni kwa masilahi ya
upande mmoja wa CCM,” Mbowe alikaririwa akisema.
Vyanzo hivyo vilisema kuwa kama Ndugai angemsikiliza Mbowe, hakuna fujo
ambazo zingeibuka bungeni. Badala yake, naibu spika huyo alitumia ubabe
kumlazimisha Mbowe akae chini, na baadaye akamwitia askari wamtoe, jambo
ambao wabunge wengine wa upinzani walilikataa, wakajitoa mhanga
kumlinda Mbowe.
Katika sakata hilo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi,
alivuliwa viatu na askari wapatao watano, wakambebea mzobemzobe hadi
nje, huku mmjoa wao akisemekana kumuumiza kwa ngumi, jambo ambalo
lilisababisha hasira za mbunge huyo naye akathubutu kumpiga konde askari
huyo.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kama Ndugai angemsikiliza
Mbowe, viongozi wa Bunge wangekutana na kuweka mazingira ya mjadala
wenye hoja zenye afya kwa ajili ya masilahi ya Watanzania.
Vyanzo hivyo vinasema suala la Kiongozi wa Upinzani Bungeni kupewa
nafasi kusema anaposimama hufanyika kwa mujibu wa kanuni ya 5(1)
inayosema:
“Katika kutekeleza majukumu yake, yaliyotajwa katika ibara ya 84 ya
Katiba, Spika ataongozwa na kanuni na pale ambapo kanuni hazikutoa
muongozo, basi Spika
atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi, kanuni zingine
zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi
za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu
wa Bunge la Tanzania.”
Kwa kuzingatia kanuni hii, na kwa kuwa Bunge letu linafuata utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola (Westminster Model)
ambao unatoa nafasi ya pekee kwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali na
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani anaposimama kutaka kusema jambo
bungeni, makundi kadhaa ya wananchi yamekuwa yakimlaumu Ndugai kwamba
alipaswa kumhukumu Mbowe baada ya kusikiliza hoja yake.
“Angempa nafasi ya kusema au kusikilizwa kwanza ili ajue kiongozi
mwenzake alitaka kusema nini au alikuwa na jambo gani zito au la dharura
ambalo lingeweza hata kusaidia Bunge zima, hivyo wananchi kunufaika,”
kilisema chanzo kimoja cha karibu na Mbowe.
Mbowe alisema kuwa Ndugai anapaswa kuelewa kuwa bungeni ni mahali ambapo
panapaswa kuheshimiwa kwa mijadala mikali, yenye hoja za afya kwa ajili
ya masilahi ya wananchi, kwani moja ya kigezo muhimu katika uvumilivu
wa kujadiliana ni kusikiliza, lakini hakutoa fursa hiyo kwa sababu
anazozijua.
Duru za siasa zinaeleza kuwa Ndugai alilifanya kwa makusudi kumzuia
Mbowe kwa sababu ya maelekezo yaliyotokana na vikao vya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) vilivyoketi hivi karibuni jijini Dodoma.
Rais Kikwete njia panda
Wakati muswada huo uliopitishwa kwa maoni ya upande mmoja wa wabunge wa
CCM ukisubiri kusainiwa ili kuwa sheria, Rais Jakaya Kikwete amewekwa
katika wakati mgumu kusaini muswaada huo.
Ugumu huo unatokana na malalamiko mengi kutoka nje na ndani ya nchi
ambayo yameelekezwa kwa CCM, kwamba imekusudia kuhakikisha inatengeneza
Katiba itakayolinda masilahi yao badala ya kujali masilahi ya taifa.
Wakati wabunge wa kambi ya upinzani wakisusia mjadala na kutoka nje,
wabunge wa CCM walipitisha muswada huo bila kuujadili, na bila
kuzingatia hoja ya ushirikishwaji wa Wazanzibari.
Hatima ya muswada huo iko mikononi mwa Kikwete ambaye anakabiliwa na
wakati mgumu kama ataamua kuusaini au kulitaka Bunge litimize kwanza
hitaji hilo lililoleta sokomoko inayoweza kudhuru mchakato mzima huko
mbeleni.
Kama Rais Kikwete atatumia busara kama za awali, upo uwezekano mkubwa
muswada huo ukarejeshwa bungeni ili ujadiliwe baada ya kutimiza vigezo.
Ugumu huo unatokana na dhamira yake ya wazi kwamba anataka kuweka
historia ya kuandika Katiba upya wakati CCM inamzunguka kwa kufanya
njama za kisirisiri, kuhujumu mchakato wa Katiba Mpya kama njia ya
kumkomoa Mwenyekiti wao, Rais Kikwete.
chanzo:daima
Post a Comment