Raia wa Rwanda
amejinyonga kwa kamba chumbani kwake, tukio linalohusishwa na zoezi
linaloendelea hivi sasa nchini la kuwasaka wahamiaji haramu na
kuwarejesha makwao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio,
marehemu anatajwa kuwa ni Francis Mathias (75), ambaye alikuwa mkazi wa
kitongoji Kikukuru kata Kikukuru, tarafa Mabira wilayani Kyerwa mkoani
Kagera.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kikukuru, Joseph Leo, jana
alilithibitishia NIPASHE kutokea kwa tukio hilo na kuwa alipata taarifa
hizo kutoka kwa binti wa marehemu juzi saa 3:00 asubuhi.
“Baada
ya kupata hizo taarifa niliongozana na mgambo, tulipofika mlango wa
chumba chake ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukafanikiwa kuuvunja
tukaingia ndani na kukuta amejitundika kwa kamba,” alisema Leo na
kuongeza kuwa marehemu alikuwa mfugaji na mkulima.
Alisema kuwa kabla ya kujiua, mzee huyo alichana fedha za Kitanzania zinazokadiriwa kufikia Shilingi
milioni saba zikiwamo noti za Sh. 5,000 na za Sh. 10,000, ambazo zilikutwa ndani ya chumba chake.
Leo
alisema baada kushuhudia alipiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kata
Kikukuru ambaye alifika na kupiga ngoma na watu walikusanyika kushuhudia
kilichotokea na baadaye kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi.
Alipotakiwa
na NIPASHE kuthibitisha kama kweli mwananchi wake aliyejinyonga alikuwa
raia wa Rwanda, Leo alithibitisha na kufafanua kuwa tayari alikwisha
kumuorodhesha kwa lengo la kurejeshwa kwao katika opereshani iliyoanza
Jumamosi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu wanaoishi mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa aliwahi kumhoji marehemu Mathias ambaye alimweleza kuwa alikuja Tanzania kutoka Rwanda tangu mwaka mwaka 1976.
Naye
Ofisa Tarafa ya Mabira, Nicolaus Rugemalira, alisema uchunguzi wa awali
wa kimazingira umeonyesha kuwa kulikuwa na mgogoro wa familia baada ya
marehemu kutaka wauze mali zao zote warudi Rwanda, lakini familia yake
haikukubaliana naye kutokana na mkewe kuwa raia wa Tanzania.
“Mke
wake ni Mtanzania, inaonekana baada ya familia yake kukataa uamuzi wake
wa kuuza mali zote ili waondoke, aliamua kuchukua uamuzi huo,” alisema
Rugemalira.
Akizungumzia tukio hilo, binti wa marehemu, Melania
Francis, alithibitisha kuwapo ugomvi kati ya baba yake na mama yake hali
iliyosababisha mama yao kuondoka bila kufahamika alikoelekea.
Alisema
siku ya tukio aliamka na kuwaandaa wadogo zake kwenda shuleni na baada
ya hapo alikwenda shambani kuona kama vibarua wameanza kazi ya kulima,
lakini aliporudi nyumbani alishangaa kuona mlango wa chumba cha baba
yake bado umefungwa wakati haikuwa kawaida yake kulala hadi saa moja.
Melania
alisema alibisha hodi bila majibu, akajaribu kufungua ikashindikana na
alipochungulia aliona fedha nyingi zimetapakaa ndipo alipokimbia kutoa
taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji.
“Nafahamu baba alikuwa na uwezo wa kumiliki fedha hizo, lakini sikufahamu anazihifadhi wapi,” alisema binti huyo wa marehemu.
Alisema
wamezaliwa watoto watano katika familia hiyo na kwamba ndugu zake
wawili walitoweka na kubakia watatu na kuongeza kuwa kuwa anatambua kuwa
baba yake alikuwa raia wa Rwanda.
Alipotakiwa kueleza kama
anafahamu alikoelekea mama yake, binti huyo alidai kuwa hafahamu ingawa
anafahamu kuwa ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.
Kutokana
na kutoweka kwa mama huyo pamoja na wanafamilia wengine, uongozi wa
eneo hilo unaendelea na ufuatiliaji ili kujua wanafamilia wengine
wamekwenda wapi.
-NIPASHE
Post a Comment