RAIS Jakaya Kikwete amesema wale wote wanaombeza
kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula wake 2015 huku
akiwananga baadhi ya wanaCCM kwa kushindwa kuyaelezea mafanikio ya
Serikali chini ya chama hicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika
mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia
(MCC), Rais Kikwete alisema: “Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini
sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa
ahadi zangu.
“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika
vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na
nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima.
“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji
vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali yetu ya
barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba naomba
niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili.
“La umeme leo nazindua nataka kuwaeleza walionibeza waje waone sasa
ahadi zangu…hayo yote niliyasema kwenye ahadi zangu 2010,” alieleza
Kikwete huku akishangiliwa na wananchi.
Mradi huo umegharimu Dola za Marekani 15.54 milioni sawa na Sh24.87
bilioni kwa Mwanza na Geita pekee, fedha ambazo ni asilimia 25 ya Dola
za Marekani 62.6 milioni sawa na Sh103.24 bilioni zilizotengwa kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi 225 ya upanuzi wa njia za kusambazia umeme
katika mikoa kumi nchini.
Rais Kikwete alisema Serikali inajipanga kusambaza umeme na kufikiwa
vijiji vyote na kubainisha kuwa mpango huo unakwenda sambamba na
uanzishaji wa vyanzo vya umeme ili viweze kuzalisha megawati 3,000
ifikapo 2015 na kwamba ziada itauzwa nje ya nchi.
Septemba 2 mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
ilitangaza kuanza kwa awamu ya pili ya usambazaji wa umeme vijijini,
mpango ambao utagharimu Sh881 bilioni na kukamilika Juni 2015.
Katika utekelezaji wa mradi huo, huduma za jamii zitakazopewa
kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ni shule, zahanati, misikiti,
makanisa na visima vya maji.
Mpango huo unatarajiwa kuinufaisha mikoa 24 ya Tanzania Bara, huku
wateja 250,000 wa awali wakiunganishwa pamoja na kuhusisha kazi ya
usambazaji umeme kwenye makao makuu ya wilaya 13 zisizokuwa na umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Ami Mpungwe alisema tayari mikoa 14
imepata makandarasi na ujenzi wa vituo sita vya usambazaji umeme,
wakati mchakato wa kuwapata wajenzi katika mikoa 13 iliyokosa
wakandarasi awali, unaendelea.
Awananga viongozi wa CCM
Rais Kikwete amewananga baadhi ya viongozi wa chama chake na kusema kuwa ni dhaifu katika uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio ya Serikali chini ya CCM.
Rais Kikwete amewananga baadhi ya viongozi wa chama chake na kusema kuwa ni dhaifu katika uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio ya Serikali chini ya CCM.
“Baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na wanachama wamezubaa kiasi cha
kushindwa kuzungumzia mafanikio ya Serikali inayoundwa na CCM, lakini
wamekuwa mahodari wa kujadili wanapobezwa na wapinzani.
“Tatizo lenu CCM mmezubaa, huo ndiyo udhaifu wenu mkubwa, kupata maji
ya bomba ni hatua kubwa na maendeleo, lakini viongozi wa CCM nyie
mmezubaa na ni dhaifu, hamuwezi kueleza mafanikio haya, lazima niliseme
hili na ujumbe uwafikie,” alieleza na kuongeza.
“Kwa nini mnasubiri mimi nifike hapa ndipo mje kwenye miradi kama
hii, mimi nikija huku siji nikiwa nimebeba miradi hii mgongoni, kwa nini
mmekuwa dhaifu wa kuyasema haya na badala yake mmekuwa hodari wa
kushupalia dosari zinazosemwa na wapinzani na kuacha mazuri haya?”
alisema Kikwete. Alisema Tanzania ni nchi kubwa kuliko nchi zingine za
Afrika Mashariki, lakini ina mtandao mkubwa wa barabara kuliko nchi kama
Kenya, lakini akawalaumu watu wanaoisifia nchi hiyo jirani na kubeza
mafanikio ya Serikali yake.
Azungumzia Elimu
Wakati huohuo, Rais Kikwete amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha kila sekondari ya kata inakuwa na maabara zenye vifaa viliyokamilika na kwamba atakayeshindwa kufanya hivyo atamwajibisha.
Wakati huohuo, Rais Kikwete amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha kila sekondari ya kata inakuwa na maabara zenye vifaa viliyokamilika na kwamba atakayeshindwa kufanya hivyo atamwajibisha.
Alisema vijana lazima wasome katika shule zenye vifaa na kusisitiza
kuwa, kwa sasa Serikali imekamilisha mpango wa kusambaza walimu ili
kukabiliana na uhaba uliopo. Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali
inajiandaa kukamilisha mpango wa Tehama kwa shule zote nchini kutokana
na kuwapo kwa mtandao wa mawasiliano kupitia mkongo wa taifa.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz
إرسال تعليق