Habari
iliyoko katika ukurasa wa mbele wa gazeti la MTANZANIA la leo
(September 10) ni kuhusu ripoti mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya
Kupambana na Mihadarati na Uhalifu (UNODC), inayosema Tanzania ni kinara
wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo, imesema jumla ya tani 64 za dawa za kulevya aina ya
Heroine, zilisafirishwa bila kukamatwa kwenda au kupitia Afrika
Mashariki, ikiwamo Tanzania kati ya mwaka 2010 na 2013.
Ripoti hiyo, imesema nchini Tanzania mji wa Tanga, ndio kinara na
njia kuu ya kusafirishia dawa hizo kwani tangu mwaka 2010, ukamataji
uliongezeka kutoka kilo 145 hadi kilo 813 mwaka huu.
“Tanga ni njia kuu ya usafirishaji wa dawa hizi, kumekuwa na
ongezeko kubwa mno tofauti na miji mingine katika ukanda wa Afrika
Mashariki,” ilisema ripoti hiyo. Wastani wa ukamataji wa shehena za
dawa za kulevya eneo hilo, uko katika kilogramu 1,011 mwaka 2013 kutoka
145 kilo za awali.
Takwimu zinaonyesha kwa pamoja Watanzania na Wakenya, wanaongoza kwa
utumiaji na usafirishaji dawa za kulevya aina ya Cocaine, huku wakitumia
dola milioni 160 kila mwaka. Lakini katika kipindi cha miaka mitatu
iliyopita, kati ya mwaka 2010 na 2013, shehena zilizokamatwa na maofisa
husika nchini Tanzania, Kenya, Shelisheli na Mauritius zilikuwa tani 1.6
tu.
Takwimu hizo za kushtusha, zinatoa picha kwamba sehemu kubwa ya
shehena za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au kukamatwa na
vyombo vya dola. Eneo la Afrika Mashariki, linaonekana kuwa kimbilio la
wasafirishaji kutoka Asia hususani wa Afghanistan, Iran na Pakistan.
Ripori hiyo, imesema Pwani ya Mashariki mwa Afrika imekuwa kitovu cha
biashara na upitishaji dawa za kulevya, kwa sababu ya kukua kwa
mahitaji ya ndani na kuchagizwa na hatua zilizochukuliwa kudhibiti dawa
hizo katika eneo la Balkan, lililokuwa likiongoza kwa biashara hiyo.
Kwa mfano mwaka 2011, kilogramu 102 za dawa za kulevya zilikamatwa
mjini Mombasa, lakini kufikia mwaka 2013, kiwango hicho kiliongezeka
kuwa kilo 194.
Ripoti ililinganisha ukanda huo na njia ya Balkan, ambayo
inaunganisha nchi za Pakistan, Iran na Uturuki kabla ya kuvusha kwenda
kusini mashariki mwa Ulaya. Katika njia hiyo, ukamataji ulishuka hadi
kilogramu 679 mwaka 2010, kutoka kilogramu 1,804 mwaka 2006 ikichangiwa
pamoja na mambo mengine na kupungua kwa soko la Heroine barani Ulaya.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema wasafirishaji wamebuni njia
nyingine ambazo bado hazijulikani kuingia Ulaya. “Mtiririko wa biashara
mashariki mwa Afrika kwa hakika umeongezeka, kutokana na ukuaji wa
mahitaji ya ndani au ukuaji wa matumizi katika ukanda huo kama soko au
eneo la kupitisha mihadarati.
Iwapo mashariki mwa Afrika itakuwa ‘Balkan mpya’ athari zake kwa
ukanda huo, zitakuwa kubwa kama zile zilizoikumba Afrika Magharibi,
ripoti ilionya.
“Hatua ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa dawa za kulevya,
zinachukuliwa uzito kimataifa, lakini pia ongezeko la matumizi ndani ya
mashariki mwa Afrika si jambo la kupuuza.”
Wakati dawa za kulevya zinapoondoka Afghanistan, husafirishwa kwa njia ya barabara hadi Pwani ya Makran, ukanda wa jangwani uliotambaa kutoka Pakistan hadi Iran katika mwambao wa Bahari ya Arabu na Ghuba ya Oman ambako wakazi wake wengi ni Waafrika Magharibi na Waasia.
Wakati dawa za kulevya zinapoondoka Afghanistan, husafirishwa kwa njia ya barabara hadi Pwani ya Makran, ukanda wa jangwani uliotambaa kutoka Pakistan hadi Iran katika mwambao wa Bahari ya Arabu na Ghuba ya Oman ambako wakazi wake wengi ni Waafrika Magharibi na Waasia.
Wasafirishaji hao wana watu wao Mashariki mwa Afrika, ambao wengi wao ni Watanzania na Wakenya wanaoendesha shughuli mpakani.
Mwaka 2011, kwa mfano, Nyakiniywa Naima Mohamed maarufu kama Mama
Lela, msafirishaji maarufu wa biashara hiyo raia wa Kenya kutoka
kitongoji cha Majengo mjini Nairobi, alikamatwa nchini Tanzania baada ya
Rais wa Marekani, Barack Obama kumtaja kuwa mmoja wa vigogo wa ‘unga’.
Vigogo wa ‘unga’, hata hivyo huajiri watu wanaowabebea kutoka mataifa
mbalimbali yakiwamo Waafrika Kusini na Waafrika Magharibi.
Inaelezwa wabebaji huhusika wa kusafirisha dawa za kulevya, hupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole nchini Ethiopia. Lakini imekuwa
kawaida kwa Waafrika Magharibi kutumia hati za kusafiria za Afrika
Kusini, wanazopata kwa njia ya kuhonga au kufunga ndoa na raia.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, baada ya Watanzania na Wakenya, raia
wa Nigeria wanashika nafasi ya pili kama wabebaji maarufu zaidi, huku
idadi yao kubwa wakiishi nchini Kenya. Mmoja wa Wanigeria hao, Anthony
Chinedu kutimuliwa kwake nchini Kenya, kidogo kusababishe mgogoro wa
kidiplomasia baina ya Kenya na Nigeria.
Source: Mtanzania
Post a Comment