SIMBA SC YAIPIGA GOLI 4 - 3 MAFUNZO YA ZANZIBAR WAKATI AKIFUNGUA AKAUNTI YA MABAO

Nararua kama Simba; Tambwe Amisi akishangilia na Ramadhani Singano 'Messi'
 

MSHAMBULIAJI mpya Mrundi wa Simba SC, Amisi Tambwe leo amefungua akaunti ya mabao katika klabu hiyo, baada ya kufunga mawili katika ushindi wa 4-3 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii. Pamoja na kufunga mabao mawili, Tambwe pia alitoa pasi ya bao la pili- hivyo kuwaonyesha Simba SC kwamba hawakukosea kumsajili.   Mchezaji huyo kutoka Vital’O ya Burundi na mfungaji bora wa Klabu Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka huu, aling’ara katika mchezo wa leo sawa na beki Kaze Gilbert waliyesajiliwa naye wote kutoka Vital’O. Hadi mapumziko, tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Mafunzo wakitangulia kupitia kwa Ally Juma dakika ya 32 na Amisi Tambwe akiisawazishia Simba SC dakika ya 45. Mafunzo walipata bao lao kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja umbali wa mita 24, lililomshinda kipa Andrew Ntalla na kutinga nyavuni.   Simba ilisawazisha baada ya Tambwe kuuwahi mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia yeye mwenyewe kupiga kichwa akiunganisha krosi ya Rashid Ismail kutoka upande wa kulia wa Uwanja.  Kipindi cha pili, Simba SC iliingia na moto na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 47 tu mfungaji Sino Augustino aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Rashid Ismail kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Amisi Tambwe.  Mafunzo ilisawazisha bao hilo dakika ya 52 mfungaji Jaku Juma aliyeunganisha pasi nzuri ya Ally Juma baada ya mabeki wa Simba SC kuchanganyana.  Dakika ya 72, Juma Jaku aliifungia Mafunzo bao la tatu, akiunganisha krosi ya Heri Salum ikiwa ni dakika moja tu tangu kipa Abbel Dhaira aingie kuchukua nafasi ya Andrew Ntalla. Tambwe aliifungia Simba SC bao la kusawazisaha dakika ya 81, akiunganisha krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’.  Nahodha Nassor Masoud ‘Chollo’ aliifungia Simba SC bao la nne dakika ya 83 baada ya gonga safi, mpira ukianzia kwa Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyempa Said Ndemla ambaye akampasia mfungaji aliyewainua vitini wana Msimbazi. Simba SC; Anderw Ntalla/Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Miraj Adam, Gilbert Kaze, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’/William Lucian ‘Gallas’, Ramadhani Singano ‘Messi’, Said Ndemla, Amisi Tambwe, Rashid Ismail/Sino Augustino na Ramadhani Chombo ‘Redondo’/Zahor Pazi.
Salamu zenu Jangwani; Tambwe Amisi leo amefungua akaunti ya mabao Simba SC

Mafunzo; Abdul Suleiman, Hamadi Hajji/Hajji Abdi, Abdul Abdallah, Heri Salum, Said Mussa, Juma Othman/Haji Mwambe, Mohamed Abdul, Masoud Hamad/Wahid Ibrahim, Juma Jaku, Ally Othman/Sadick Habib na Ally Juma.

Post a Comment

أحدث أقدم