TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Awataka
viongozi wawashauri wananchi wafuge kisasa
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda amesema idadi kubwa ya mifugo katika bonde la mto Mara ni
mojawapo ya changamoto zinazokabili utunzaji endelevu wa bonde na amewataka
viongozi wa mkoa watoe elimu ya kutosha kwa wananchi ili wafuge kisasa na
kuepusha uharibifu wa mazingira.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Septemba 15, 2013) wakati akifunga maadhimisho
ya Siku ya Mara (Mara Day Celebrations) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine
mjini Mugumu, wilayani Serengeti mkoani Mara. Maadhimisho hayo yalianza
Septemba 12, mwaka huu.
“Changamoto
iliyopo ni kuainisha, matumizi bora ya ardhi iliyopo kwa kuzingatia uwiano
baina ya ardhi na mifugo iliyopo. Tunawajibika kupima ardhi yetu kuanzia ngazi
ya vijiji ili kuepusha athari zinazotokana na kuzidisha mifugo katika maeneo
tuliyonayo ikiwemo eneo la Mto Mara.
“Kupima
ardhi kutasaidia kuepusha migogoro inayoweza kutokea baina ya wakulima na
wafugaji. Tutaendelea na mikakati ya kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili
wafuge kisasa na kupunguza idadi ya mifugo ili kuepuka uharibifu wa mazingira,”
alisema.
Alisema
bonde la mto Mara ni rasilmali kwa wakazi wa Mara na kwamba kama bonde hilo
likitumiwa vizuri lina fursa kubwa ya kiuchumi na hasa kwenye kilimo cha
umwagiliaji maji.
Alisema
wastani wa pato la mwananchi wa Mara liko chini ikilinganishwa na mikoa jirani
ya Mwanza, Manyara na Shinyanga na kwamba kilimo cha umwagiliaji kwa mazao kama
mpunga na mbogamboga kitasaidia kuinua pato la wananchi wa mkoa huo.
“Ili
kulitunza bonde hili ni lazima tuache kazi za kilimo umbali wa mita 60 kutoka
kingo za mto huu kwa mujibu wa sheria. Tuache kuchoma misitu, tuache kukata
miti hovyo, na kama mnataka kufanikiwa, nawashauri mfuge nyuki. Mkiwa na
mizinga yenu kwenye misitu hamtachoma moto, ni lazima mtajizuia kuchoma moto
ili msiwadhuru nyuki wenu,” alisema.
Alisema
bonde la mto Mara ni fursa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hivyo wakazi wa
bonde hilo wa pande zote mbili hawana budi kulitunza kwa faida ya kizazi cha
sasa na cha baadaye.
Aliwaomba
viongozi wa Tanzania na Kenya kushirikiana kulitunza bonde hilo na kuhakikisha
kwamba Mto Mara unadumu.
“Mto Mara
ni mto wenye historia, ni mto wa kumbukumbu, ni mto wa shughuli za kiuchumi na
shughuli za maendeleo. Lakini zaidi ya yote, mto Mara unaunganisha jamii za
pande zote mbili Kenya na Tanzania. Tutumie mto Mara kama alama (Symbol) ya
chanzo cha umoja wetu, mshikamano, udugu na upendo kati ya wananchi wa Kenya na
Tanzania na hata nchi zote za maziwa makubwa zinazotumia Ziwa Victoria,”
alisema.
Maadhimisho
hayo yalihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa Maji, Maliasili na Utalii na TAMISEMI
pamoja na viongozi kadhaa kutoka Serikali ya Kenya. Pia wakuu wa mikoa ya
Arusha, na Manyara, na wakuu wa wilaya
mbalimbali.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, SEPTEMBA 15, 2013.
Post a Comment