Taarifa ya Mazishi ya Meja Khatib Shaban Mshindo Kijiji kwao Fujoni Unguja.
Press Release:-
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Meja Khatibu Shaaban
Mshindo aliyefariki Dunia akiwa katika shughuli za ulinzi wa amani
katika kikosi cha umoja wa Mataifa kwenye jimbo la Goma Nchini Jamuhuri
ya Kidemokrasia ya Congo amezikwa kwa heshima zote za Kijeshi.
Meja Shaaban ambaye alijeruhiwa vibaya kwa bomu katika eneo lake la kazi
na kusababisha kuvuja damu nyingi na hatimae kusababisha kifo chake
akiwa njiani kupelekwa Hospitali alizikwa kijiji kwao Mangapwani Wilaya
ya Kaskazini B, Mkoa Kaskazini Unguja.
Makamanda na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania , askari
wengine wa vikosi vya ulinzi, wananchi , ndugu wa marehemu walishiriki
kwenye mazishi hayo wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed.
Marehemu Meja Khatib Shaaban Mshindo alizaliwa Tarehe 29 Septemba 1972
katika Mtaa wa Rahaleo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi na
baadaye kupata elimu yake ya msingi na kuhitimu mwaka 1986.
Alijiunga na Skuli ya Sekondari uchama na kuhitimu kidato cha Nne mwaka
1990 ambapo baadaye akajiunga na kidato cha tano na sita katika skuli ya
sekondari ya Alharamain na kumaliza mwaka 1993.
Meja Khatib Shaaban Mshindo alijiunga na Jeshi la wananchi wa Tanzania {
JWTZ } Tarehe 1 machi 1995 na kutunukiwa heshima ya kamisheni tarehe 17
mei 1997.
Katika utumishi wake Meja Khatib Shaaban Mshindo alibahatika kuhudhuria
mafunzo ya afisa mwanafunzi chuoni Monduli, kozi ya uongozi wa platuni,
uongozi wa kombania pamoja na mafunzo ya operesheni Nchini Canada mwaka
2008.
Kamanda Khatib kutokana na ukakamavu wake alipandishwa vyeo kuanzia
nafasi ya Luteni mwaka 1998, kepteni mwaka 2004 na kufikia cheo cha meja
mwaka 2010 wadhifa aliokuwa nao hadi kufariki kwake.
Marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo aliwahi kushika madaraka ya
Kamanda wa Kikosi mwaka 1997, Mkufunzi kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka
2006 pamoja na kuwa kamanda wa kombania Mkoani Kibaha.
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Serikali ya Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua na
kuthamini mchango wa Meja Khatibu Shaaban Mshindo alimtunuku nishani ya
Miaka 40 ya JWTZ.
Umoja wa Mataifa katika mazishi hayo uliwakilishwa na Kamanda wa Vikosi
vya Umoja huo Mjini Goma Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Meja
D.B Samujeli .
Kamanda Khatibu Shaaban Mshindo aliyelitumikia jeshi la Wananchi wa
Tanzania katika kipindi cha miaka 18 miezi saba na siku 28 ameacha
kizuka mmoja na watoto watatu.
Mwenyezi Muungu alilaze roho ya marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo mahali peMa peponi. Amin.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/9/2013.
Post a Comment