Tukae chonjo, urafiki huu wa pacha watatu unaiangamiza Tanzania

  MCL

Nikiwa kanisani jana na wakati mwingine wowote, natoa maombi yangu mengi, lakini kubwa kuliko yote natamani Yesu arudi. 
Ni kwa nini nataka Bwana Yesu arudi hasa wakati huu ambao tunaambiwa kuwa tusubiri kwani nyakati zake hazijatimia?
Hili ni swali zito na kubwa ambalo nimekuwa nikijiuliza hata Jumatatu ya leo ninapoiangalia, ninapoitizama nchi yangu Tanzania na mustakabali wake katika Jumuiya ya sasa ya Afrika Mashariki (EAC), chini ya marais wa kizazi hiki cha vijana na wazee.
Kabla ya kwenda mbali, niseme kuwa matamanio yangu ya kutaka Yesu arudi hata leo, ni ili ayafumbue macho yetu sisi Watanzania vipofu, atuzibue masikio yetu sisi ambao ni viziwi.
Ninatamani Yesu aje duniani ili atulishe sisi kwa maajabu yake, atulishe mikate michache na vijisamaki bila kujali wingi wetu ili nasi tushibe na kisha makombo yake yakusanywe kwenye makapu zaidi ya 120, kulingana na idadi ya makabila yetu.
Muujiza huu wa Yesu ufanyike kwetu Watanzania kwani inaelekea tumechoka, kazi hatutaki kufanya, ndiyo maana tunahitaji maajabu yafanyike, ili tuamini.
Usishangae, nchi ambayo inaitwa ya kilimo, ambayo zaidi ya asilimia 70 ya watu wake ni wakulima, lakini ni nini tija ya kilimo hiki cha jembe la mkono au trekta hizi za power tillers, ambazo zimeingizwa nchini kupitia Mpango wa Kilimo Kwanza, ubunifu ambao ni miongoni mwa mingi ambayo haitekelezeki?
Ni fikra hizi na nyinginezo kuhusu nchi yangu ambazo kwa hakika zinaisumbua nafsi yangu na roho yangu kila ninapojaribu kufanya tafakuri ya kina kuhusu mustakabali wa nchi yangu inayojinadi kwamba kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano na ambayo watu wake hawataki kubadilika, hawafanyi kazi, wanashinda vijiweni wanajadili siasa na umbea.
Kama nilivyoeleza wiki chache zilizopita, Tanzania yetu ya sasa inapita kwenye kipindi kigumu. Kwa hakika ni kipindi kigumu kweli ambacho sisi kwa umoja wetu bila kujali itikadi na tofauti zetu za kisiasa, rika, dini,  jinsia wala bila kusubiri mchakato wa Katiba Mpya ukamilike, hatuna budi kusimamia jambo moja.
Nilidhani wanasiasa wetu wa vyama vikubwa na vidogo, viongozi wa dini wa madhehebu yote wangepiga kelele tayari kuhusu kitu hiki kinachoendelea katika uhusiano baina ya nchi yetu na majirani zake.
Kama wananchi au wazalendo kwa umoja wetu, naamini kuwa hatuna budi kukaa chini, kufanya tafakuri ya kina na ikibidi tuangalie nini kinatokea ili tuweze kujirekebisha.
Inafaa, kama nchi tuongozwe zaidi na masilahi yetu mengi kama nchi, hasa wakati huu ambao tumezungukwa na majirani, marafiki ambao wanaonyesha kila dalili, hawatuamini au wametuchoka.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post