
MCL
Nikiwa kanisani jana na wakati mwingine wowote, natoa maombi yangu mengi, lakini kubwa kuliko yote natamani Yesu arudi.
Ni kwa nini nataka Bwana Yesu arudi hasa wakati huu ambao tunaambiwa kuwa tusubiri kwani nyakati zake hazijatimia?
Hili ni swali zito na kubwa ambalo nimekuwa
nikijiuliza hata Jumatatu ya leo ninapoiangalia, ninapoitizama nchi
yangu Tanzania na mustakabali wake katika Jumuiya ya sasa ya Afrika
Mashariki (EAC), chini ya marais wa kizazi hiki cha vijana na wazee.
Kabla ya kwenda mbali, niseme kuwa matamanio yangu
ya kutaka Yesu arudi hata leo, ni ili ayafumbue macho yetu sisi
Watanzania vipofu, atuzibue masikio yetu sisi ambao ni viziwi.
Ninatamani Yesu aje duniani ili atulishe sisi kwa
maajabu yake, atulishe mikate michache na vijisamaki bila kujali wingi
wetu ili nasi tushibe na kisha makombo yake yakusanywe kwenye makapu
zaidi ya 120, kulingana na idadi ya makabila yetu.
Muujiza huu wa Yesu ufanyike kwetu Watanzania
kwani inaelekea tumechoka, kazi hatutaki kufanya, ndiyo maana tunahitaji
maajabu yafanyike, ili tuamini.
Usishangae, nchi ambayo inaitwa ya kilimo, ambayo
zaidi ya asilimia 70 ya watu wake ni wakulima, lakini ni nini tija ya
kilimo hiki cha jembe la mkono au trekta hizi za power tillers, ambazo
zimeingizwa nchini kupitia Mpango wa Kilimo Kwanza, ubunifu ambao ni
miongoni mwa mingi ambayo haitekelezeki?
Ni fikra hizi na nyinginezo kuhusu nchi yangu
ambazo kwa hakika zinaisumbua nafsi yangu na roho yangu kila
ninapojaribu kufanya tafakuri ya kina kuhusu mustakabali wa nchi yangu
inayojinadi kwamba kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano na ambayo
watu wake hawataki kubadilika, hawafanyi kazi, wanashinda vijiweni
wanajadili siasa na umbea.
Kama nilivyoeleza wiki chache zilizopita, Tanzania
yetu ya sasa inapita kwenye kipindi kigumu. Kwa hakika ni kipindi
kigumu kweli ambacho sisi kwa umoja wetu bila kujali itikadi na tofauti
zetu za kisiasa, rika, dini, jinsia wala bila kusubiri mchakato wa
Katiba Mpya ukamilike, hatuna budi kusimamia jambo moja.
Nilidhani wanasiasa wetu wa vyama vikubwa na
vidogo, viongozi wa dini wa madhehebu yote wangepiga kelele tayari
kuhusu kitu hiki kinachoendelea katika uhusiano baina ya nchi yetu na
majirani zake.
Kama wananchi au wazalendo kwa umoja wetu, naamini
kuwa hatuna budi kukaa chini, kufanya tafakuri ya kina na ikibidi
tuangalie nini kinatokea ili tuweze kujirekebisha.
Inafaa, kama nchi tuongozwe zaidi na masilahi yetu
mengi kama nchi, hasa wakati huu ambao tumezungukwa na majirani,
marafiki ambao wanaonyesha kila dalili, hawatuamini au wametuchoka.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق