Halmashauri
ya Jiji la Dar es Salaam ilikiuka taratibu za utoaji wa zabuni ya
kubomoa jengo lililokuwa ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo
mikoani kilichopo Ubungo (UBT), ambalo lilianguka mwanzoni mwa mwaka huu
na kusababisha madhara kwa watu na mali. Januari 21 mwaka huu, watu
wanne walijeruhiwa baada ya magari yao waliyokuwa wameyaegesha katika
eneo la UBT kuangukiwa na ukuta, huku magari 24 na bajaji nne
zikiharibika vibaya.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Kampuni ya Makalla Contractors
Ltd ndiyo iliyofanya kazi ya ubomoaji huo, lakini hakukuwa na mkataba wa
kazi hiyo baina yake na Jiji la Dar es Salaam.
Uchunguzi
zaidi unaonyesha kuwa, licha ya kutokuwa na mkataba, Makalla Contractors
Co. Ltd wamepeleka kwa uongozi wa jiji hilo madai ya Sh59, 615, 252
wakitaka walipwe kutokana na kazi hiyo.
“Makubaliano
yalifanyika kwa mdomo na kazi ikaanza, hakukuwa na uitishwaji wa zabuni
wala kufanyika taratibu zozote za kisheria, walipeana kazi hiyo
kirafiki na baada ya jengo kubomoka ndipo walianza kuhaha jinsi ya
kuwezesha kulipa fedha hizo,” kilisema chanzo chetu.
Katika
moja ya nyaraka za kampuni hiyo kwenda Halmashauri ya Jiji, Kampuni
hiyo ya Makalla inasema ilipewa kazi hiyo kutokana na gharama zake kuwa
za chini na kwamba iliombwa kuanza kuitekeleza haraka kutokana na
udharura wake kwa ahadi kuwa taratibu nyingine za kupewa LPO na mkataba
zingefuata. Hata hivyo, taratibu za zabuni zinataka kazi itangazwe na
hata kama kungekuwa na dharura ilipaswa kufuata utaratibu wa ‘single
sourcing’ ambao ungewezesha kuchagua kampuni ya kutekeleza jukumu bila
kuchelewa. Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi ambaye ndiye
mwenye dhamana ya kusaini mikataba kwa niaba ya jiji hilo alisema:
“Sijawahi kusaini mkataba unaohusu kampuni hiyo unayoitaja (Makalla) na
wala sijawahi kusaini mkataba kuhusu ubomoaji wa pale Ubungo.”
Alipobanwa akitakiwa aeleze sababu za ubomoaji kufanywa bila yeye
kuhusishwa alijibu: “Waulize watendaji wa Jiji, muulize mkurugenzi maana
huo ni wajibu wa watendaji na siyo wajibu wa Meya, nilichokwambia ni
kwamba mimi sijasaini mkataba wowote kuhusu suala hilo.”
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alipoulizwa
alisema hawezi kutoa taarifa kuhusu suala hilo kwenye vyombo vya habari.
“Wewe hizo
taarifa umezipata wapi?... Mimi siwezi kukwambia mkandarasi gani
aliyehusika, sitoi taarifa hizo kwenye vyombo vya habari… unazitaka za
nini? Wananchi ndio wamekutuma uwatafutie taarifa? Wao wanatakiwa
wasubiri huduma ikamilike, lakini siyo kumjua mkandarasi, kalipwa au
hakulipwa,” alisema Kabwe.
Malipo kwa Mkandarasi
Wakati Kabwe
akihoji maswali lukuki, habari zaidi zinasema ofisi yake imekuwa katika
harakati za kuwezesha Kampuni ya Makalla kulipwa, na kwamba
kinachokwamisha malipo hayo ni kutokuwapo kwa mkataba wa kazi. Fedha za
ubomoaji kiasi cha Sh63 milioni zilitolewa na Ofisi ya Mradi wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART) na kuhamishiwa kwenye akaunti za Halmashauri ya
Jiji la Dar es Salaam, lakini imebainika kuwa kumekuwapo na harakati za
fedha hizo kurejeshwa DART.
“Ofisi ya
mkurugenzi inaendelea na mchakato wa kurejesha fedha hizo DART ili
Kampuni ya Makalla ikalipwe huko maana ni ngumu malipo kufanyika hapa
kwetu kwa sababu hakuna documents (nyaraka) za mkataba wa kazi, huwezi
kulipa, sasa huko DART nao sijui watafanyaje,”kilidokeza chanzo chetu
katika ofisi za Jiji. Hata hivyo, Ofisa Mwandamizi wa DART, Jack Meena
alisema suala hilo linawahusu Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) na
Halmashauri ya Jiji ambao ndiyo wamiliki wa kituo hicho.
“Sisi kazi
yetu ni kuhakikisha eneo la mradi linakuwa tayari kwa ajili ya ujenzi.
Kwa hiyo tulifanya tathmini na kulipa fidia na kumwachia mkandarasi,”
alisema Meena.
Msimamizi wa
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Tanroads, Barakaeli Mmari
alisema suala hilo linashughulikiwa na Halmashauri ya Jiji, hivyo
waulizwe wenyewe.
“Ni kweli
tunasimamia mradi wa mabasi yaendayo haraka, lakini suala la ubomoaji ni
la Halmashauri ya Jiji. Wao ndio wanafahamu mkandarasi na kama alilipwa
au hakulipwa,” alisema Mmari.
Sheria za Ubomoaji
Uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa Kampuni ya Makalla iliandikiwa barua na Bodi
ya Usajili wa Makadarasi (CRB), ikitakiwa kutoa maelezo ya kuhusika
kwake katika kazi hiyo, pia vielelezo vilivyoonyesha jinsi kazi
ilivyofanywa. CRB katika barua yake ya Mei 9, 2013 kwenda kwa Mkurugenzi
wa Makalla Contractors Co. Ltd ambayo gazeti hili limeiona, ilitaka
kampuni hiyo kuwasilisha mkataba wa kazi, majina ya wataalamu
walioshiriki katika kubomoa jengo hilo na nyaraka za uthibitisho wa
malipo yao.
Msajili wa
CRB, Boniface Muhegi alikiri kwamba Kampuni ya Makalla imesajiliwa.
“Halmashauri ya Jiji ndiyo waliomwajiri, ila kulipotokea malalamiko
ndiyo tukawauliza (Jiji) wakakiri kwamba ndiye aliyefanya kazi hiyo,”
alisema Muhegi na kuongeza:
“Mwanzoni
kulikuwa na ubabaishaji. Tulipouliza tuliambiwa wenye magari waliambiwa
wayaondoe kwanza… hilo ni tatizo la Jiji, lakini tutaichukulia hatua
Kampuni ya Makalla kwa sababu imesababisha uharibifu wa mali za watu na
kwa kutokuzingatia vigezo vya usalama kazini.” “Katika tathmini zetu
tuna alama, kama zikifikia 60 au 70 tunatoa adhabu kulingana na kosa.
Inaweza ikawa onyo, kusimamishwa kwa muda au kufutwa kabisa. Kwa kuwa
hili ni kosa la kwanza tutaangalia vigezo vyetu,”alisema Muhegi.
Septemba 4,
mwaka huu gazeti hili liliwasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
hiyo, Makalla Moseka ambaye awali alisema taarifa zote kuhusu suala hilo
zinapaswa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini
baadaye alimtaka mwandishi afike ofisini kwake kesho yake kwa maelezo
zaidi.
Gazeti hili
lilifika katika ofisi hizo, chumba namba tisa cha ghorofa ya 10 katika
Jengo la Ushirika, Lumumba, lakini ofisi hizo zilikuwa zimefungwa, huku
majirani zake wakisema kuwa ofisi hiyo imefungwa muda mrefu.
Baada ya
kumkosa, mwandishi alimpigia simu siku hiyo ya Septemba 5 ambapo Makalla
alikanusha kwamba kampuni yake iliwahi kufanya kazi ya aina hiyo.
“Sikiliza
bwana, mimi sikuhusika na kazi hiyo, inawezekana kuna watu walishafanya
kazi kwenye kampuni hii, halafu wakaenda kufanya kazi kwa jina la
kampuni yangu,” alisema Makalla.
Baada ya
kubanwa zaidi, Septemba 7, Makalla aligeuka na kukiri kuhusika na kazi
hiyo, huku akitaka mwandishi aonane naye Septemba 8. Alipotafutwa siku
hiyo, alisema kwamba yuko msibani, hivyo kuahidi kwamba angekuwa tayari
kuzungumza Septemba 10.
Gazeti hili lilimtafuta juzi na jana, lakini mara zote alipopigiwa simu alikuwa akikata baada ya mwandishi kujitambulisha.
Chanzo - Mwananchi
إرسال تعليق