Na Emmanuel Richard Makundi
Upinzani nchini Zimbabwe umekosoa baraza jipya la mawaziri
lililotangazwa na rais Robert Mugabe, ukisema kiongozi huyo ameteua watu
walewale ambao wameshindwa kuleta mabadiliko nchini humo.
Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha MDC-T kimesema kuwa mawaziri
walioteuliwa kuunda baraza jipya la mawaziri toka chama tawala cha
ZANU-PF lina sura zilezile za wazee na viongozi ambao wameshindwa kuleta
mabadiliko nchini Zimbabwe.
Kwenye mahojiano maalumu na rfikiswahili msemaji wa MDC, Douglas
Mwanzora amesema hakuna mabadiliko ambayo yanatarajiwa kwenye Serikali
ya sasa na kwamba uteuzi wa mawaziri haukuzingatia vigezo na uwezo wa
watu katika kuleta mabadiliko nchini humo.
Mwonzora ameongeza kuwa wengi wa mawaziri wanaounda baraza jipya la
mawaziri walikuwepo kwenye Serikali ya umoja wa kitaifa iliyomaliza muda
wake na wengi walishindwa kuleta mabadiliko ambayo wananchi wa Zimbabwe
wanayataka.
Wakati wa sherehe za kuapishwa kwa mawaziri hao, rais Mugabe ameahidi
kuleta mabadiliko kwenye Serikali yake na kudai kuwa atayashughulikia
makampuni ya kigeni yaliyoko nchini humo kukubali uwekezaji wa asilimia
51 kubaki kwa Zimbabwe na wao kuchukua asilimia 49.
Rais Mugabe amesema anataka kuona mabadiliko nchini mwake na kumtaka
kila waziri aliyemchagua kutekeleza kile ambacho wananchi waliwapa
dhamana wakati wa kempeni za urais.
Baraza jipya la mawaziri limejaa nyuso za viongozi waliopigania uhuru wa
Zimbabwe na watu ambao ni wafuasi wa damu wa chama tawala cha ZANU-PF.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa waziri wa sheria, Patrick Chinamasa
ameteuliwa kuongoza wizara ya uchumi na biashara akiwa na jukumu la
kuhakikisha uchumi wa Zimbabwe unaimarika.
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, Morgan Tsvangirai ameendelea
kusisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka huu uligubikwa na mizengwe na ushindi
wa rais Mugabe haukuwa halali.
Via kiswahili.rfi.fr
إرسال تعليق