Rais wa Msumbiji Armando Guebuza na Chama cha Renamo kutafuta suluhu ya haraka

Raisi wa Msumbiji Armando Guebuza kufanya mazungumzo na chama cha Renamo ili kunusuru amani ya Msumbiji/bbc.co.uk

Na Martha Saranga Amini

Rais wa Msumbiji Armando Guebuza ameomba nafasi ya kufanya mazungumzo na lililokuwa kundi la waasi la Renamo ambalo sasa linatambuliwa kama chama cha siasa.


Rais Guebuza amesema wanahitaji kutafuta suluhu la haraka ili kulinda amani ya nchi hiyo ambayo kwa sasa imetetereka.

Ombi hilo linakuja baada ya ghasia za hivi karibuni baina ya vikosi vya serikali na Renamo, walitangaza kusitisha kuutambua mkataba wa amani wa mwaka 1992 uliotamatisha machafuko yaliyodumu kwa miaka 16.

Uhusiano baina ya chama tawala cha Frelimo na wapinzani wa Renamo umekuwa tete katika siku za hivi karibuni, huku mataifa mbalimbali na jumuiya ya kimataifa ikitoa wito kwa pande hizo mbili kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo ili kuepusha umwagaji damu.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki-moon alitoa wito alhamisi kwa serikali ya Msumbiji pamoja na lililokuwa kundi la waasi nchini humo Renamo kufanya mazungumzo sambamba na kuepuka ghasia zinazohatarisha amani na usalama nchini humo.

Siku kadhaa baada ya Renamo kusitisha kuutambua mkataba wa amani wa mwaka 1992 uliomaliza machafuko ya miaka 16, hofu ya kutumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe imezidi kutanda nchini humo.

Shule zimeripotiwa kufungwa katika maeneo yanayoizunguka kambi ya Renamo kutokana na hofu ya usalama, huku mataifa kama Marekani yakizidi kuhimiza pande zote kumaliza tofauti zao.

Nao Ubalozi wa Ufaransa mjini Maputo umeonya dhidi ya raia wake waishio nchini humo kutosafiri kuelekea katika jimbo la Sofala ambalo ni kitovu cha machafuko baina ya Renamo na vikosi vya serikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post