Askari Polisi, viongozi wa tarafa watakiwa kushirikiana

GEDSC DIGITAL CAMERA
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambaye ni Polisi Tarafa wa Muklati Elibariki Kileo akitoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas wakati wa makabidhiano ya kikosi kazi cha askari 15 watakaofanya kazi pamoja na wananchi wa Tarafa ya Muklati wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
GEDSC DIGITAL CAMERA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas akitoa elimu ya Polisi Jamii kwa viongozi, vikundi vya ulinzi shirikishi na wananchi wa Tarafa za Muklati na Enaboishu wilayani Arumeru. Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Askari wa Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa Tarafa za Muklati, Enaboishu, Poli, Mbuguni  Moshono na King’ori zilizopo katika wilaya ya Arumeru wametakiwa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kufanikisha dhana nzima ya Ulinzi Shirikishi.
Akiongea katika vikao tofauti vilivyofanyika mwishoni mwa wiki hii wakati wa kusambaza askari 15 kwa kila Tarafa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema ushirikiano huo utafanikiwa endapo tu askari Polisi watakuwa wanatumia lugha nzuri na kufanya kazi kwa maadili huku viongozi wa Tarafa, Kata, Mitaa au vijiji watakuwa tayari kuwapa ushirikiano.
“Kama kutakuwa na ushirikiano wa dhati ambao utawezesha kufanya kazi kama timu moja basi kutakuwa na kuelezana ukweli na hivyo kuondoa majungu badala ya kila kundi kufanya kazi kwa kujitenga”. Alisema Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema serikali wanayoitumikia ni moja hivyo ili kukidhi malengo ya kuimarisha Ulinzi na Usalama katika maeneo yao makundi hayo yanatakiwa kuungana na kufanya kazi kama familia moja hali ambayo itasaidia kuongeza vikundi vya ulinzi shirikishi, kupata taarifa za uhalifu na wahalifu na hatimaye kupunguza vitendo vya uhalifu kama si kuutokomeza kabisa.
Alisema siku zote wahalifu wanafanikiwa sehemu ambazo ni dhaifu na zile sehemu ambazo zimeungana wanashindwa kupenya kwani uhalifu wowote ambao unahusisha watu wa mbali unaanzia toka kwa mwenyeji hivyo kama kila mwenyeji ataungana na wenzake kwa kuukataa uhalifu basi daima maeneo yao yatakuwa salama.
Kamishna huyo Msaidizi Mwandamizi wa Polisi pia aliwaomba wananchi hao kujitokeza mahakamani pindi wanapotakiwa kutoa ushahidi hali ambayo itasaidia kuwatia hatiani watuhumiwa watakaowakamata kinyume cha hapo jamii itaendelea kuvivyooshea vidole jeshi la Polisi pamoja na Mahakama.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngaramtoni iliyopo katika Tarafa ya Muklati Bw. David Kimisi (CCM) alimpongeza Kamanda Sabas kwa hatua yake ya kuamua kutembelea Tarafa zote za Mkoa huu kwa nia ya kutoa elimu ya Polisi Jamii kwa viongozi, vikundi vya Ulinzi Shirikishi pamoja na wananchi na pia hatua yake ya kusambaza askari hao 15 kila tarafa ili waweze kutoa huduma karibu na jamii.
Diwani huyo alisema katika Tarafa yake kuna ushirikiano mkubwa kati ya Viongozi, wananchi ambao wanashirikiana vema na Mkaguzi wa Polisi wa Tarafa hiyo Elibariki Kileo pamoja na askari wa Tarafa hiyo hali ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Alimalizia kwa kusema maneno ya Kamanda Sabas yameongeza chachu ya kuimarisha ulinzi katika eneo hilo huku viongozi na wananchi wa eneo hilo wakiwa na mipango dhabiti ya kukikarabati kama si kujenga kituo cha Polisi  kingine ili kiweze kuhudumia idadi kubwa ya watu wa eneo hilo kwa wakati mmoja.

Post a Comment

Previous Post Next Post