
Taarifa zilizotufikia na kuthibitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama
vya siasa nchini, zinakitaja chama hicho kuwa ni African Alliance for
Change and Transparence (AACT) na kwamba mipango ya usajili wa muda wa
chama hicho inadaiwa kuanza kuratibiwa kwa takribani mwezi mmoja sasa.
Chama hicho kimekamilisha baadhi ya taratibu na kinatarajiwa kupewa
usajili wa muda na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siku ya Jumanne,
wiki ijayo.
Upo uwezekano wa wanachama waliofukuzwa uanachama kutoka Chadema hivi karibuni kujiunga na chama hicho.
Wanasiasa wengine wanaotajwa ama kuwa nyuma ya kuanzishwa kwa chama
hicho au wanatarajia kujiunga, ni wale waliofukuzwa kutoka CUF, nia
ikiwa ni kuendeleza harakati zao za kisiasa.
Mmoja wa watu wanaounda chama hicho alilidokeza gazeti hili kuwa
endapo chama hicho kitapata usajili baada ya hapo, taratibu na harakati
za kuanza kukitangaza zitafanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema pia wamepanga kuendesha siasa zenye upinzani, ikiwa ni
pamoja na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi
Mkuu wa 2015 iwapo kitakuwa tayari kimejiimarisha.
Hivi karibuni Kamati Kuu Chadema, iliwavua uanachama aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa
Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe, akikimbilia Mahakamani kuomba zuio la kutojadiliwa uanachama wake
na kikao hicho.
Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba walituhumiwa na uongozi wa juu wa
Chadema kuandaa waraka wa siri wenye lengo la kufanya mabadiliko ya
uongozi ndani ya chama, hali iliyoibua mgogoro mzito hadi kufikia uamuzi
wa kuwavua uanachama baadhi yao.
Alipoulizwa Dk. Kitila kama ameshiriki na wenzake kuanzisha chama
cha siasa, alishindwa kukataa wala kukubali, kwa kusema kuwa ukweli ama
uongo wa habari hiyo utajulikana.
Alipotajiwa chama hicho na kwamba kinatarajia kupata usajili wa muda, alisema hafahamu hilo na hawezi kuzungumzia.
“Sina cha kuzungumza juu ya swali lako, kuwapo kwa chama kipya au
la, nadhani ukweli utajiweka wazi nanyi mtabaini tu, hata hilo jina la
chama kipya kuitwa AACT sijui,” alisema Dk. Kitila.
Mpaka sasa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu nchini ni 23,
ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, UMD, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, Tadea.
Vingine ni TLP, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP,
APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau na AFP, UMD, FORD, CCK, ADC na
Chaumma. Chama:
Mtanzania
إرسال تعليق