
Licha ya wito wa Rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wa kutaka
kufanya mazungumzo na makundi ya wanamgambo na wito wake wa kurejeshwa
amani katika nchi hiyo, habari kutoka mji mkuu Bangui zinasema kuwa,
hali bado si shwari kutokana na kuendelea kushuhudiwa machafuko.
Jana mapigano makali yalishuhudiwa katika mji mkuu Bangui ambapo watu
wasiopungua 9 walipoteza maisha yao na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Mapigano hayo yalijiri huku Rais Catherine Samba-Panza akianza maisha
mapya katika Ikulu ya Rais baada ya kuapishwa kuwa Rais wa muda wa nchi
hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, hali ya ukosefu wa amani ingali inashuhudiwa katika mji mkuu Bangui.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki
za Binadamu la Amnesty International limeripoti kwamba, kwa akali
Waislamu 50 wameuawa baada ya wanamgambo wa Anti Balaka kushambulia
vijiji viwili kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wiki iliyopita pia, wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka waliwaua
Waislamu 22, wakiwemo watoto watatu na kuwajeruhi makumi ya wengine.
Mapigano ya ndani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza mwezi Machi
mwaka jana baada ya kung'olewa madarakani serikali ya aliyekuwa Rais wa
nchi hiyo François Bozizé.
Post a Comment