Na Ibrahim Yamola na Christopher Maregesi, Mwananchi
Bunda na Dar. Uamuzi wa Rais
Jakaya Kikwete kutangaza Watanzania Bara kuungana na wenzao wa Zanzibar
kupumzika kusherehekea Sikukuu ya Mapinduzi, kumezua mkanganyiko kwa
wafanyakazi na watu wa kada mbalimbali.
Mara kadhaa, chumba cha habari cha gazeti hili
kilikuwa kikipokea simu kutoka kwa wananchi kutaka kuhakikisha kama
kweli leo ni siku ya mapumziko.
Katika kuadhimisha siku hiyo juzi, Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alitangaza kuwa kesho (jana) itakuwa ni
mapumziko na kutumia nafasi hiyo kusema kuwa alinong’onezwa na Rais
Kikwete kuwa na Bara itakuwa mapumziko.
Baadaye, Rais Kikwete kupitia Kurugenzi ya
Mawasiliano Ikulu, alitoa taarifa kutangaza rasmi kuwa ni mapumziko
kuungana na Wazanzibari kuadhimisha siku hiyo.
Mwandishi alimtafuta Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudentia Kabaka ili kuzungumzia athari za mapumziko hayo na ajira za
watu hususan wasio katika sekta rasmi ambapo alisema: “Naomba usiniulize
swali kama hilo mimi.”
Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema mapumziko hayo yana athari kubwa
kwa makundi mbalimbali.
Profesa Ngowi alisema, kuna watu ambao walihitaji
kupata huduma za kibenki, kusaini mikataba na mambo mbalimbali ya
kijamii, lakini kutokana na mapumziko ya ghafla shughuli hizo zimekwama.
“Mapumziko haya yameathiri makundi mengi, sisi
tulikuwa na mkutano leo (jana) na tumewaleta wageni kutoka nchi
mbalimbali, lakini kutokana na gharama tumeamua kuendelea na ratiba
licha ya kuwa ni mapumziko,” alisema Profesa Ngowi.
Aliongeza: “Lakini surprise (mshangao) ya Rais
Kikwete ina uzuri wake na ubaya wake, hivyo kama alijua hilo ni bora
angetoa taarifa wiki mbili kabla ili watu wakajipanga kwa mapumziko na
shughuli zao..”
Naye Mtaalamu wa Uchumi wa Kimataifa na Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema athari za mapumziko hayo yapo
hususan kwa sekta isiyo rasmi kwa wafanyakazi kuhatarisha ajira zao.
Alisema waajiri wa viwandani wanaweza wasiyatambue mapumziko hayo.
Post a Comment