Mapumziko Siku ya Mapinduzi yakanganya wengi


Na Ibrahim Yamola na Christopher Maregesi, Mwananchi
Bunda na Dar. Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kutangaza Watanzania Bara kuungana na wenzao wa Zanzibar kupumzika kusherehekea Sikukuu ya Mapinduzi, kumezua mkanganyiko kwa wafanyakazi na watu wa kada mbalimbali.
Mara kadhaa, chumba cha habari cha gazeti hili kilikuwa kikipokea simu kutoka kwa wananchi kutaka kuhakikisha kama kweli leo ni siku ya mapumziko.
Katika kuadhimisha siku hiyo juzi, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alitangaza kuwa kesho (jana) itakuwa ni mapumziko na kutumia nafasi hiyo kusema kuwa alinong’onezwa na Rais Kikwete kuwa na Bara itakuwa mapumziko.
Baadaye, Rais Kikwete kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, alitoa taarifa kutangaza rasmi kuwa ni mapumziko kuungana na Wazanzibari kuadhimisha siku hiyo.
Mwandishi alimtafuta Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka ili kuzungumzia athari za mapumziko hayo na ajira za watu hususan wasio katika sekta rasmi ambapo alisema: “Naomba usiniulize swali kama hilo mimi.”
Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema mapumziko hayo yana athari kubwa kwa makundi mbalimbali.
Profesa Ngowi alisema, kuna watu ambao walihitaji kupata huduma za kibenki, kusaini mikataba na mambo mbalimbali ya kijamii, lakini kutokana na mapumziko ya ghafla shughuli hizo zimekwama.
“Mapumziko haya yameathiri makundi mengi, sisi tulikuwa na mkutano leo (jana) na tumewaleta wageni kutoka nchi mbalimbali, lakini kutokana na gharama tumeamua kuendelea na ratiba licha ya kuwa ni mapumziko,” alisema Profesa Ngowi.
Aliongeza: “Lakini surprise (mshangao) ya Rais Kikwete ina uzuri wake na ubaya wake, hivyo kama alijua hilo ni bora angetoa taarifa wiki mbili kabla ili watu wakajipanga kwa mapumziko na shughuli zao..”
Naye Mtaalamu wa Uchumi wa Kimataifa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema athari za mapumziko hayo yapo hususan kwa sekta isiyo rasmi kwa wafanyakazi kuhatarisha ajira zao.
Alisema waajiri wa viwandani wanaweza wasiyatambue mapumziko hayo.

Post a Comment

أحدث أقدم