WEZI WAVUNJA GHALA LA KUHIFADHIA DAWA HOSPITALI YA WILAYA YA MAKETE NA KUIBA DAWA ZILIZOKWISHA MUDA WAKE WA MATUMIZI

Watu wasiojulikana wamevunja ghala la kuhifadhia dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi katika hospitali ya wilaya ya Makete mkoani Njombe na kuiba dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi na kutokomea nazo kusikojulikana

Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa kuamkia jana januari 21, 2014 na kuzua sintofahamu na hali ya taharuki kwa wakazi wa Makete mkoani Njombe baada ya kusikia taarifa hiyo

Akizungumzia tukio hilo Mganga mfawidhi hospitali ya wilaya ya Makete Dkt. Michael Gulaka amesema tayari wameshatoa taarifa kwenye kituo cha polisi wilayani hapo na kuwataka wananchi kuwa makini wanapokwenda kununua dawa kwenye maduka ama kwa watu kuangalia tarehe ya matumizi ya dawa hiyo ili kuepuka kuuziwa dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi

Dkt. Gulaka amesema kwa mujibu wa taratibu za kiafya, dawa hizo zilizoibiwa ni sumu kwa kuwa muda wake wa matumizi umekwisha na hivyo zilikuwa zikisubiri kwenda kuteketezwa lakini kabla ya zoezi hilo kufanyika ndipo wizi huo umetokea

Ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa polisi ama hospitali ya wilaya ya Makete pindi watakapoona dawa zikiwa zimezagaa mitaani ama kuwa na mashaka na dawa watakazoziona mahali popote na kuzitilia shaka ili watuhumiwa hao wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria

Post a Comment

أحدث أقدم