
Wachezaji wa timu ya Mbeya City wakipasha kabla ya mechi. Leo wanatupa
karata yao katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wakiwakabili wekundu
wa Msimbazi Simba ya Jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Wakati vinara wa Ligi Kuu, Azam
na Yanga wakiwa katika michezo ya kimataifa nje ya nchi, macho na
masikio ya mashabiki wa soka leo yatakuwa jijini Mbeya wakati Mbeya
City watakapoikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Sokoine.
Vinara wa ligi Azam wenye pointi 36, wapo Maputo
wakiikabili Ferroviano katika Kombe la Shirikisho kesho, mabingwa
watetezi Yanga (35) leo watashuka uwanjani Comoro kuikabili Komorozine
katika Ligi ya Mabingwa.
Mbeya City, ipo katika nafasi ya tatu katika
msimamo ikiwa na pointi 34, wanajua ushindi wa leo dhidi ya Simba
inayoshika nafasi nne na pointi 31 utawapeleka kileleni kwa kwa mara ya
kwanza mwaka huu.
Simba wanashuka kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya
wakiwa na kumbukumbu ya kunyukwa bao 1-0 na Mgambo Shooting katika mechi
yao iliyopita, hivyo wanautazama mchezo dhidi ya Mbeya City kama fursa
ya kurekebisha makosa yao.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ambaye tayari
ametangaza kunawa mikono katika vita ya kusaka ubingwa amekiri kwamba
shughuli itakuwa pevu leo.
“Tukutana na timu yenye rekodi nzuri katika ligi
kwani imepoteza mchezo mmoja tu hivyo ni dhahiri tunatakiwa kupambana
kufa na kupona ili kupata ushindi,”alisema Logarusic.
Kocha wa Mbeya City Juma Mwambusi akizungumzia
mchezo huo alisema, utakuwa mkali na wenye upinzani wa ajabu, lakini
kikosi chake kimejiandaa kuitoa machozi Simba.
“Simba ni timu kubwa na tunaiheshimu, lakini
mwisho wa siku soka inachezwa sehemu ya wazi na idadi ya wachezaji ni 11
kwa kila timu hivyo sina shaka kwamba kikosi changu kipo tayari kuvuna
pointi tatu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Prisons.
Pia, utamu wa ligi hiyo utashuhudiwa katika
viwanja vingine vitano Kwenye Uwanja wa Manungu, Mtibwa Sugar
itapepetana na Prisons, Mgambo Shooting itakung’utana na Rhino Rangers
kwenye Uwanja wa Ali Hasani Mwinyi, Ruvu Shooting itapimana ubavu na
Coastal Union kwenye Uwanja wa Mabatini.
Wakati JKT Oljoro itavutana mashati na JKT Ruvu
kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kadhalika Ashanti United itakuwa
kwenye Uwanja wa Azam Complex kumenyana na Kagera Sugar
إرسال تعليق