BAADHI YA VIPANDE VYA RAIS KIKWETE VILIVYOTAWANYA VIKUNDI MITAANI KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Bungeni mjini Dodoma akihutubia Bunge maalum la Katiba

Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. 

Wapo wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. 

Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. 

Wanasema kuwa   taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664.  Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia.  Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.  Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!

Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2  ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja.  Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?

Mheshimiwa Mwenyekiti; 
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211.  Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. 

Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. 

Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote.  Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”

Post a Comment

Previous Post Next Post