Chanzo cha bunge kuahirishwa!

BARUA YA UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI (UKAWA) KWA
MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM, MHESHIMIWA SAMWEL J. SITTA,
KUHUSU UKIUKWAJI WA KANUNI ZA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sisi ambao majina yetu yameorodheshwa hapa chini ni Wajumbe
wa Bunge Maalum ambao tunatokana na vyama vya CHADEMA,
CUF, NCCR Mageuzi, DP, UDP, CHAUSTA, CHAUMA, NRA, NLD na
CCK pamoja na Wajumbe walioteuliwa kutokana na makundi
yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba, Sura ya 83. Tumeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(‘UKAWA’) wenye lengo la kuhakikisha kwamba mchakato wa
sasa wa Katiba katika Mkutano huu wa Bunge Maalum
unapelekea nchi yetu kupata Katiba Mpya na bora kwa ajili ya
nchi yetu.
Kwa sababu ya mwendelezo wa matukio ya ukiukwaji wa
makusudi wa Kanuni za Bunge Maalum, 2014, ambao umefanyika
tangu ulipoapishwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum, kama
tunavyoonyesha hapa, tunapenda kukufahamisha kwamba
hatuko tayari kuendelea kukaa kimya wakati unaendelea kuvunja
Kanuni za Bunge Maalum na kupelekea Mkutano wa Bunge
Maalum kuwa hatarini kuvunjika. Katika kipindi cha siku nne tangu
umeapishwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum umefanya
maamuzi yafuatayo yanayodhihirisha ukiukwaji wa Kanuni:
1. Tarehe 14 Machi, 2014, mara tu baada ya kuapishwa
ulitangaza kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba atawasilisha Rasimu ya Katiba siku ya Jumatatu,
yaani leo. Aidha, ulitangaza kwamba baada ya Mwenyekiti
wa Tume kuwasilisha Rasimu, kutakuwa na kipindi cha siku
tatu kwa Wajumbe wa Bunge Maalum kufanya mjadala wa
jumla juu ya Rasimu kwa lengo la ‘kufungua vifua vyao.’ Vile
vile, ulilitaarifu Bunge Maalum kwamba baada ya hapo
Mheshimiwa Rais atakuja kulihutubia Bunge Maalum kati ya
siku ya Jumanne au Jumatano.
2. Licha ya Wajumbe kadhaa wa Bunge Maalum kukuomba
ubadilishe msimamo wako juu ya masuala haya, tarehe 15
Machi uliendeleza msimamo huo na ukaongeza kwamba
Mwenyekiti wa Tume atawasilisha Rasimu ya Katiba kwa
muda usiozidi dakika sitini na baada ya hapo kutakuwa na
siku tatu za semina itakayoongozwa na wataalamu kutoka
nje ya nchi yetu na baadaye ndiyo Mgeni Rasmi atakuja
kulihutubia Bunge Maalum.
3. Leo tarehe 17 Machi baada ya malalamiko ya Wajumbe
kadhaa umesema kwamba umeshauriana na Mwenyekiti
wa Tume jana tarehe 16 Machi na mmekubaliana kwamba
muda wa saa mbili (dakika mia moja ishirini) zitamtosha
Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba. Hii
inathibitisha kwamba ulipopanga muda wa dakika sitini kwa
ajili hiyo siku ya tarehe 15 Machi ulikuwa hujashauriana na
Mwenyekiti wa Tume kama inavyotakiwa na Kanuni za
Bunge Maalum. Aidha, kwa taarifa tulizo nazo, inaelekea
Mwenyekiti wa Tume analazimishwa kukubaliana na muda
ambao wewe mwenyewe na nguvu nyingine zilizo ndani na
nje ya Bunge Maalum mmempangia.
Kwa maoni yetu, yote haya ni ukiukwaji wa makusudi wa
Kanuni:
(a) Kanuni ya 7(1)(g) na (h) ya Kanuni za Bunge Maalum
imeweka mpangilio wa shughuli zote za Bunge Maalum
ambapo ‘hotuba ya ufunguzi ya Mgeni Rasmi’, i.e., Rais
wa Jamhuri ya Muungano au Rais wa Zanzibar,
itafuatiwa na ‘uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba.’ Kwa
jinsi ya mpangilio wa shughuli uliowekwa na Kanuni ya
7(1), uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba kabla ya hotuba
ya ufunguzi ya Mgeni Rasmi ni ukiukwaji wa Kanuni za
Bunge Maalum na, kwa vyovyote vile, kunatoa picha
kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuja
Bungeni kama mchangiaji wa hoja badala ya kuja
kama Mkuu wa Nchi kwa lengo la kufungua Bunge
Maalum;
(b) Kanuni ya 47(a) inaelekeza kwamba “Mwenyekiti
baada ya kushauriana na Mwenyekiti wa Tume
watapanga muda unaofaa kwa ajili ya Mwenyekiti wa
Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge
Maalum.” Pamoja na kwamba kanuni hiyo imeanza
kwa maneno ‘isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo
kwenye Kanuni hizi au Mwenyekiti ameelekeza
vinginevyo’, ufahamu wetu wa Kanuni za Bunge
Maalum unatuelekeza kwamba Mwenyekiti wa Bunge
Maalum hana uwezo kikanuni wa kujipangia yeye
mwenyewe muda ambao Mwenyekiti wa Tume
atahitaji kwa ajili ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba.
Muda huo unatakiwa kupangwa kwa pamoja baada
ya mashauriano baina yao.
(c) Kwa mujibu wa kanuni ya 31(3), “baada ya Rasimu
kuwasilishwa … Mwenyekiti atatangaza majina ya
wajumbe wa kila Kamati … na kila Kamati itatekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa
na Kanuni hizi.” Aidha, kwa mujibu wa mpangilio wa
kanuni ya 32, baada ya Kamati kuundwa, Rasimu
itajadiliwa katika Kamati na baadaye katika Bunge
Maalum. Kwa mtiririko wa Kanuni ulivyo, hakuna namna
yoyote halali kwa Bunge Maalum kufanya semina ya
wataalamu wa ndani au nje ya nchi kwa lengo la
wajumbe kufungua vifua vyao au kwa lengo lingine
lolote.
(d) Matumizi mabaya ya kanuni ya 85 inayohusu mamlaka
ya kutengua kanuni. Ijapokuwa kanuni ya 85(1)
inatamka kwamba “… kanuni yoyote inaweza
kutenguliwa kwa madhumuni mahsusi …”, kanuni hiyo
imefungwa na masharti ya kanuni ya 85(4) inayoelezea
mazingira yanayoweza kusababisha kanuni itenguliwe.
Kwa kifupi, kanuni inaweza kutenguliwa kwa ajili ya
kuahirisha kikao au kuongeza muda wa shughuli au
kuongeza orodha ya shughuli yoyote ambayo
haikuwepo kwenye mpangilio wa shughuli za siku hiyo.
Nje ya mazingira hayo, Bunge Maalum haliwezi
kutengua kanuni zake.
Kwa sababu ya ukiukwaji huu wa Kanuni za Bunge Maalum
tunapenda kukujulisha kwamba sisi wanachama wa UKAWA
hatuko tayari kuunga mkono, na tutapinga kwa kadri ya
uwezo wetu mambo yafuatayo kufanyika ndani ya Ukumbi
wa Bunge Maalum:
(i) Uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba na Mwenyekiti wa
Tume kabla ya hotuba ya ufunguzi wa Bunge
Maalum na Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais
wa Zanzibar;
(ii) Semina yoyote itakayoongozwa na wataalamu wa
ndani au nje ya nchi yetu kama ulivyolitangazia
Bunge Maalum;
(iii) Hotuba ya Mgeni Rasmi endapo itafuatia uwasilishaji
wa Rasimu ya Katiba;
(iv) Jambo lingine lolote linalokiuka Kanuni za Bunge
Maalum.
Tunatarajia kwamba utayapa masuala haya tafakuri ya kutosha ili
uweze kufanya maamuzi kwa kutumia Kanuni za Bunge Maalum.
Tunaamini utatumia busara na hekima ili kuliepusha Taifa letu na
fedheha ya vurugu zisizokuwa na sababu ndani ya Bunge
Maalum.
Tunatanguliza shukrani zetu za dhati.
Chanzo JF

Post a Comment

Previous Post Next Post