FLASHBACK, HOTUBA YA MWALIMUY NYERERE MWAKA 1995 KUHUSU MUUNGANO,NI HOTUBA YA KIHISTORIA


Hotuba ya Mwalimu Nyerere kwa waandishi wa habari mwaka 1995 hasa kuhusu mustakabali wa muungano

“Watu wamezungumza Uzanzibari, baadhi ni viongozi wetu wanajivunia Uzanzibari. Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga, sio wengi, lakini wapo.

Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi, kusiwe na nchi moja bali mbili. Hili ni jambo linazungumzwa.

Tunataka viongozi, kiongozi wanaoelewa hilo. Kuzungumza Uzanzibari si jambo la fahari. Hatima yake utavunja nchi. Mtu mwenye akili, Mzanzibari ana akili hawezi akautuza Uzanzibari wa kujiita sisi Wazanzibari na wao Watanganyika.
Na adhani ile ina usalama ndani yake. Kufanya hivyo, hatima yake Zanzibar itajitenga.

Zanzibar ikijitenga, kutokana na ulevi tu…sisi Wazanzibari wao Watanganyika…sisi si wamoja. Ulevi tu…ulevi hasa ulevi wa madaraka.

Ikitokea hivyo, sisi Wazanzibari wao Watangayika. Wakumbuke kwamba muungano ndio unaowafanya waseme sisi Wazanzibari wao Watanganyika.

Nje ya muungano hawawezi kusema hivyo, nje ya muungano hakuna Wazanzibari. Nje ya muungano kuna wao Wapemba sisi Waunguja. Nataka mjue hivyo… nataka mjue hivyo.

Nje ya muungano hakuna sisi Wazanzibari wao Watanganyika. Hakuna… hakuna. Kinachowafanya sasa wajiite sisi ni ubaguzi wa kuwabagua Watanganyika.

Wakishakuwabagua Watanganyika, ile dhambi ya ubaguzi haifi, inaendelea. Dhambi ya ubaguzi ukishakuitenda inaendelea, ni sawa na kula nyama ya mtu, ukila nyama ya mtu utaendelea tu. Mtamaliza, mtatengana na Watanganyika halafu mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari…kuna Wapemba na kuna Waunguja.

Wapemba watapata msukosuko kidogo au aaah. Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama… hamtakaa salama.

Hamuwezi kukaa salama baada ya kutenda dhambi ya kubagua watu wa nchi yenu ile ile moja, mkawaita wale wao na hawa sisi. Dhambi ile haishii hapo, ndiyo historia ilivyo, ni sheria ya historia sio sheria ya Mwalimu Nyerere.

Huwezi kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache hapo hapo. Hapana, itakuandama. Ninalolisema kwa Wazanzibari nalisema kwa Watanganyika.

Zanzibar wanaweza kujitenga kwa ujinga, kwa ulevi na hasa ujinga wa viongozi wao na Watanganyika wakabaki wameduwaa.

Wazanzibari hawa wanafanyaje? Wanatuacha hawa wenzetu jamani wanakwenda zao wenzetu!

Watanganyika walioachwa wameduwaa kwa kitendo cha Wazanzibari kuwakimbia, watabaki wamoja, hawataparaganyika.

Narudia…Wazanzibari wanaweza wakatoka, wakajitenga wenyewe tu…sasa wengine wana bendera sisi hatuna kwanini, wengine wana wimbo wa taifa sisi hatuna wimbo wa taifa kwanini?

Basi wakajitenga, si wote wanaosema hivyo ni viongozi wanaosema… basi wakajitenga, wakawaacha Watanagnyika wameduwaa…hivi wenzetu kweli wanatuacha!

Wakiwaacha Watanganyika walio katika hali hiyo, Watanganyika wanaowashanga Wazanzibari katika kuwaacha, Watanganyika hawa watakuwa salama.

Watanganyika wakiwakataa Wazanzibari kwa tendo la dhambi ile ile, sisi Watanganyika wao Wazanzibari… wakautukuza usisi Tanganyika na kwa ajili hiyo wakawafukuza Wazanzibari, hawabaki salama.

Hapatakuwa na Tanganyika… wakishakujitenga tu Wazanzibari wale wako kando hivi… mmewafukuza mnajidai wakubwa ninyi… hawa nani hawa… wao wana rais sisi hatuna rais kwanini… watimue.

Mkawatimua, mkapata rais wenu hapa akawatimua. Hambaki… hambaki. Kwani mtasemaje, mtakuwa mmeishasema sababu ya kuwafanya wale wao na ninyi ni ninyi… wao vipi?

Wazanzibari… halafu mbaki ninyi? Maana wako watakaosema Wazanzibari tu… Wazanzibari kana kwamba kuna kabila Wazanzibari, mmewabagua.

Mtaanza nyumba za Wapemba, mtaziingilia pale sasa hivi. Viko vijumba vya Wapemba humu baadhi yao walikimbia wakati uleeee, vijumba vya kwanza vitapitiwa… Wapemba… Wapemba, mtamaliza vya Wapemba.

Halafu mtakuta ninyi mliokuwa mnajiita sisi… sisi Watanganyika, mtakapoanza kuchoma nyumba za Wapemba zile mtakuta aah si sisi… sisi hawa wote si wamoja.

Mbona za Wapemba tunachoma za Wachaga hatuchomi kwanini. Kwani Wachaga si wazawa bwana, hapa kuna wazawa hapa, sasa mnachoma za Wachaga mnaacha?

Mtakuta hakuna watu wanaitwa Watanganyika, mtakuta mlijidanganya mnadhani kuna watu wanaitwa Watanganyika, hakuna.

Kuna Wagogo, kuna Wanyamwezi, kuna Wasukuma, kuna Wazanaki, kuna Wakurya, kuna Wamwera… wengi sana, siwezi kuwataja wote.

Mtakuta hakuna kitu kizima hivi kinaitwa sisi Watanganyika… hata kidogo. Na madhali mmefanya dhambi ya kusema wao Wazanzibari si wenzetu… dhambi ile ile itawatafuna nyinyi.

Na mimi nasema Mwenyezi Mungu anisamehe, mnastahili iwatafune. Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na dhambi nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”

Post a Comment

Previous Post Next Post