RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya Mrisho Kikwete ameipa klabu
ya Simba Sh 30 milioni kwa ajili ya kukomboa hati yao ya kiwanja cha
Bunju B, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliwaambia wanachama wa klabu
hiyo jana Jumapili katika mkutano wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika
Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Rage alisema kwamba Rais Kikwete ametoa fedha hizo baada ya
kufurahishwa na umoja ulionyeshwa na baadhi ya wanachama wa Simba
waliojitolea kwenda katika uwanja huo kwa siku za karibuni na kufyeka
majani na kuonyesha kuwa wanauhitaji.
Rage alisema alikutana na Rais Kikwete saa 2 asubuhi jana Jumapili
kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Simba na kumtakia heri katika
mkutano huo huku pia akitoa hundi ya Sh 30 milioni kwa ajili ya uwanja
huo.
“Asubuhi leo saa 2 nilipata bahati ya kukutana na Rais Kikwete na
kututakia heri katika mkutano wetu na kama unavyojua kulikuwa na
matatizo ya kupata hati ya ardhi kule Bunju, tulikuwa tunadaiwa Sh 85
milioni, tulitoa milioni 50 hivyo nikamuomba Rais aingilie kati jambo
hili ili kuweza kupata hati mapema na kuanza ujenzi.”
“Rais akanikabidhi hundi ya milioni 30 kama mchango wake kwetu,
amedhihirisha ni mwanamichezo na mpenzi wa timu zote, kutokana na jambo
hilo naamini mambo yatakwenda vizuri na zile siku 100 alizotoa katibu wa
Simba kuwa baadhi ya vitu vitakuwa vimekamilika basi vitakamilika
kweli maana hadi kufikia siku hizo tutakuwa hata na sehemu ya kufanyia
mazoezi timu yetu,” alisema Rage.
Aliongeza: “Kikubwa alichofurahishwa ni juhudi za wanachama kwenda
kule na kuonyesha uhitaji wa uwanja na ndio maana akaamua kutoa fedha
hizo ili kuhakikisha tunapata hati ya ardhi na kuanza ujenzi mara moja.”
SOURCE: MWANASPOTI
Post a Comment