
Baadhi
ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Komnyang’anyo wilaya ya
Handeni wakitembea barabarani kuelekea kwenye makazi yao vijiji
mbalimbali vinavyoizunguka shule hiyo.
UJENZI
wa Sekondari za Kata katika mikoa mbalimbali umesogeza huduma za elimu
kwa baadhi ya maeneo. Ipo mikoa ambayo awali ilikuwa na shule chache za
sekondari hali ambayo ilifanya wanafunzi wachache kupata fursa ya
kujiunga na sekondari. Kwa sasa hali si hivyo tena, mikoa mingi
imeongeza idadi ya shule hizo licha ya changamoto kibao inazozikabili
shule hizi.
Zipo
baadhi ya shule za sekondari zimejengwa mbali kidogo na makazi ya
wahitaji kitendo ambacho huwalazimu wanafunzi kutembea muda mrefu
asubuhi wakielekea shuleni na baadaye jioni wakirejea nyumbani, hali
ambayo ni changamoto kwa wengi wao.
Hata
hivyo baadhi ya maeneo shule hizo zimejengwa mbali zaidi na makazi ya
watu kutokana na kile kuhudumia vijiji ama vitatu hadi vinne, na hazina
mabweni jambo ambalo wanafunzi wanashindwa kuvumilia umbali uliopo
kutoka kijiji kimoja hadi kingine hivyo kutafuta mbinu mbadala ya
kusogea jirani na shule wanazokuwa wamepangiwa.
Wanafunzi
wanaamua kutafuta vyumba vilivyopo jirani na maeneo ya shule
walizopangiwa na hivyo kupanga (kukodi chumba). Wenyewe vyumba hivi
huviita mageto. Vyumba hivi huwa vidogo na vingine mithili ya vibanda,
ambapo bei huwa ya chini zaidi kwa mwezi. Wanafunzi wengine huamua
kujikusanya wawili ama zaidi na kuishi pamoja kwenye geto ili kupunguza
gharama.

Mageto mbili.
Mkoa
wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto baadhi ya maeneo aina hii ya maisha
ya wanafunzi ni kitu cha kawaida. Wanafunzi wameamua kupanga kwenye
mageto (vyumba mitaani) na kuishi kwa makundi huku wakikabiliwa na
changamoto lukuki zinazohatarisha safari yao ya elimu ya sekondari.
Mbwambo
Conrad ni Mkazi wa Kata ya Bungu wilayani Lushoto, eneo ambalo lina
idadi kubwa ya wanafunzi waliopanga kutoka vijiji vya mbali huku
wakihudhuria masomo yao ya sekondari. Anasema eneo hilo kuna wanafunzi
wengi ambao wametoka vijiji vya mbali na wamepanga jirsni na shule
kwenye kata hiyo kuhudhuria masomo.
Anasema
wanafunzi hao wamepangiwa na wazazi wao ili waweze kuhudhuria masomo
yao kuepuka umbali wanaotoka kwenye vijiji vyao. “Wanafunzi hawa
wamepanga katika baadi ya vyumba na wanaishi kwa tabu sana…wengi
wanaingia katika majaribu kutokana na aina ya maisha wanayoishi,”
anasema Mzee Conrad.
Anasema
wavulana wengi huishia kuwa wahuni maana uangalizi wa wazazi hawana,
mara nyingi utawakuta wamekaa vikundi kwa vikundi nyakati za jioni hadi
usiku unaweza kufikiri sio wanafunzi. Wanachelewa kulala muda mwingi
wanazunguka kwenye majumba ya sinema (vibanda vinavyo onesha picha za
video) hivyo wanaishi kwa kujitawala utazani si wanafunzi.
Willson
N’gwamizi ni Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Muungui wilayani Lushoto,
anasema licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali katika shule hiyo suala
la wanafunzi kuishi kwenye mageto ni changamoto kubwa kwa shule kwani
linaathiri maendeleo ya shule kitaaluma. Anasema wanafunzi hulazimika
kuishi katika vyumba hivyo vya kupanga kutokana na shule nyingi za kata
zilizojengwa kutokuwa na mabweni huku zikichukua wanafunzi kutoka vijiji
vya mbali.
“…Kifupi
suala la wanafunzi kuishi katika mageto linaathiri maendeleo ya shule
kitaaluma…wanafunzi hawa wanapoishi huko hukosa usimamizi wa wazazi na
wengine hata hela ya kumudu maisha hayo huwa ni tatizo maana wanatoka
vijiji vya mbali na uwezo wa familia zao wakati mwingine hushindwa
kuwatimizia mahitaji yote,” anasema N’gwamizi.
Anasema
kutokana na uhuru huo wa kukaa kwenye mageto wanafunzi wengine hutoroka
na kwenda kufanya vibarua kwenye mashamba ya chai na sehemu nyingine
wasichana nao huwa huru zaidi kitendo ambacho hushindwa kukabiliana na
changamoto za vishawishi mitaani.

Mageto moja.
“Ukizunguka
katika baadhi ya kata unaweza kukuta wanafunzi wa kidato cha pili
wamepanga kwenye chumba kimoja, ndani ya chumba hicho wapo wawili hadi
watatu…wengine wanatoka katika familia duni hawapewi mahitaji ya
kutosha, wengine hujikuta wanashawishika na kuingia mitaani na kujikuta
wanakatizwa masomo kwa kutiwa ujauzito,” anasema.
“Kwa
kweli mageto ni tatizo, wapo baadhi ya walimu hujitahidi kuwafuatilia
huko wanakoishi ili kuhakikisha wanajenga nidhamu ya kiuanafunzi, hata
hivyo zoezi hili bado ni changamoto maana na walimu wamejikuta wakikaa
mbali na shule kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu jambo ambalo ni
tatizo pia…,” anasema mwalimu huyo.
Suala
la ukosefu wa mabweni kwa shule za kata na kuwalazimu wanafunzi kupanga
mitaani (mageto) halipo kwa wilaya ya Lushoto pekee. Wilaya ya Handeni
nayo inakabiliwa na changamoto hiyo ya wanafunzi kupanga uswahilini
wenyewe karibu na shule walizopangiwa.
Ester
Frank ni mmoja wa wanafunzi wa sekondari za kata wilayani Handeni
anasema changamoto kwa wanafunzi kukaa kwenye mageto ni kubwa hasa wa
kike. Anasema wengi wanakosa uangalizi na usimamizi hivyo kujikuta
wanajiingiza kwenye vishawishi hivyo kuishia kupata mimba na kukatizwa
masomo yao. “…Usema kweli mageto yanatuathiri wanafunzi hapa wilayani
Lushoto,” anasema mwanafunzi huyo.
Afidha
Said ni mkazi wa Kijiji cha Kidereko, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.
Said anasema katika mahojiano na mwandishi wa makala haya kijijini
Kidereko wilayani Handeni, aliyekuwa akifuatilia vitendo vya ukatili wa
kijinsia ambavyo hufanyiwa baadhi ya wanafunzi na wanawake eneo hilo kwa
ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa). Anasema
matukio ya mimba kwa wanafunzi eneo hilo si kwamba hulazimishwa
kimahusiano, bali huingia wenyewe katika mahusiano kingono kutokana na
mazingira halisi.
Anasema
ukiachilia mbali uduni wa kipato kwa familia nyingi eneo hilo, ambao
wengi ndio wazazi/walezi wa wanafunzi, shule nyingi za kata Wilaya ya
Handeni zipo mbali na makazi ya wanafunzi. Zimejengwa hivyo ili kuweza
kuhudumia vijiji vingi, ambavyo pia kuna umbali mkubwa kutoka kijiji
kimoja hadi kingine.
Wapo
wanafunzi ambao hulazimika kutembea kilometa 12 hadi 20 kwenda na
kurudi shuleni kila siku jambo ambalo linawaumiza wengi, hivyo
kulazimika ama kutafuta urahisi wa kupata usafiri hasa kwa wanafunzi
wanaotoka vijiji vya mbali au kulazimika kupanga katika mageto jirani na
shule walizopangiwa. kwa usafiri maarufu ambao hutumika na jamii maeneo
mengi ya vijiji hivi ni pikipiki (bodaboda), ambao wazazi hawawezi
kuumudu kwa wanafunzi wao kutokana na gharama za juu.

Mmoja
wa walimu katika moja ya shule za kata wilaya ya Handeni (jina
tunalihifadhi kwa kuwa si msemaji) anasema shule yao inawanafunzi
wanatoka katika vijiji kama Kidereko ambacho ni takribani kilomita 6
kwenda na Kijiji cha Bangu ambacho ni karibu kilomita 10 kwenda tu.
Anasema umbali kama huu ukiuunganisha mwanafunzi analazimika kwenda na
kurudi kila siku unakuta ni tatizo.
Anasema
na wengi wanatoka katika familia duni unakuta hawapewi chochote
wanapotoka nyumbani kama matumizi ya siku (kula), sasa katika hali kama
hii inakuwa tabu. Wapo ambao wanaamua kukata tamaa ya kuendelea na shule
hivyo kujiingiza katika mambo ambayo yanawaharibu kitabia kabisa.
Rais
Jakaya Kikwete akihutubia wananchi Januari 7, 2013 mjini Igunga aliwahi
kusema kuwa serikali inajitahidi kukabiliana na changamoto za elimu.
“Kwa upande wa elimu tumeendelea kupata mafanikio katika kupunguza
tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu
(2013) tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu ni
57,755 kati yao 20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za
Sekondari.
Rais
Kikwete anasema kwa mwaka 2014 Serikali itaajiri walimu wapya 36,100
kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari. Kufanya hivyo
kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi. Kwa upande wa shule za
sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia kulimaliza.
Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi.
Rais
Kikwete anasema upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vya ualimu
nchini ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka. Anaongeza kuwa mapema
mwaka 2014 Serikali itakutana na wadau wa elimu nchini kujadiliana juu
ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hilo.
Hata
hivyo licha ya juhudi hizi kwa upande wa changamoto ya walimu hasa kwa
shule za kata kuna haja ya Serikali kuangali namna ya kulipa kipaumbele
suala la kupambana na changamoto za umbali wa shule za kata na makazi ya
wananchi na kuhakikisha ujenzi wa mabweni ili kupunguza adha wanazopata
wanafunzi wa kike na kiume kutokana na changamoto hiyo inamalizima kama
si kupungua kwa kiasi fulani. Tukiamua tunaweza kukabiliana na
changamoto hizi.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TAMWA
إرسال تعليق