
Kwa mujibu
wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, tathmini
hiyo ilifanywa kwa baraka za wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la
Misaada la Marekani (USAID), ili kupata taarifa kuhusu hali halisi
ilivyo kwa wanafunzi wa Tanzania, kumudu stadi za KKK wanapofika Darasa
la Pili.
Akizungumza hivi karibuni katika Kongamano la Wazi Kuhusu
Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu jijini Dar es Salaam, Dk Kawambwa
alisema tathmini hiyo ilifanywa na asasi ya Research Triangle Institute
(RTI) ili kupima kitaifa stadi za KKK.
"Upimaji huu ulifanyika
katika halmashauri 20, shule 200 kwa wanafunzi 2,214 wa Darasa la Pili
na ulitumia zana zilizojaribiwa na kuthibitishwa kimataifa za Tathimini
ya Awali ya Kusoma (EGRA), Tathimini ya Awali ya Kuhesabu (EGMA) na
Halihalisi ya Menejimenti ya Shule na Uwezo wake Kutoa Matokeo
Yanayohitajika (SSME).
"Upimaji huo umetuwezesha kupata taarifa
kuhusu hali halisi ilivyo kwa wanafunzi wetu kumudu stadi za KKK
wanapofika Darasa la Pili. Nimefurahi kuona kwamba shirika hili la RTI
ni sehemu ya kongamano la leo na washiriki mtaweza kusikia watoto wetu
wako wapi katika stadi za KKK," alisema Dk Kawambwa.
Tathmini hiyo
ilipofanywa ili kufahamu uwezo wa kusoma na kuelewa kwa lugha ya
Kiswahili, matokeo yameonesha kuwa ni asilimia nane tu ya wanafunzi wa
Darasa la Pili walioweza kusoma na kuelewa, kwa kuwa asilimia 92
hawakuweza kusoma na kuelewa.
Asilimia 40 waliopewa kazi ya kusoma, hawakuweza kujibu angalau swali moja kwa ufasaha, linalotokana na walichosoma.
Kwa
mujibu wa tathmini hiyo, wanafunzi hao wa Darasa la Pili walipimwa
welewa wao katika stadi za msingi za hisabati, kwa kuzingatia mambo
kadhaa.
Miongoni mwa mambo yaliyotumika kupima wanafunzi ni
kujumlisha na kupunguza, maarifa ya maana (kutumia maswali),
kulinganisha namba na mafumbo ya hisabati.
"Wanafunzi walifanya vizuri zaidi katika maarifa ya akili
(wanakumbuka) vitu, na hawafanyi vizuri katika maswali
ya kuelewa zaidi kwa kutumia maarifa yao ya kiakili.
"Matokeo ya tathmini ya EGMA nchini Tanzania,
yanabainisha kwamba ufundishaji wa hisabati unazama zaidi katika kukariri kwa vipengele, kanuni, na fomula.
"Licha
ya kuwa ukariri wa vipengele, unaweza kuchangia kutoa mwelekeo kwa
watoto kufahamu hisabati yao katika hatua za mwanzo kabisa za awali (kwa
mfano Darasa la 1 na la 2), EGMA nchini Tanzania ilibainisha kwamba
wanafunzi hawakuweza
kutumia maarifa yao waliyoyakariri, kujifunza hisabati tete zaidi na za muhimu katika hatua za juu," ilieleza tathmini hiyo.
Tathmini
hiyo ilibainisha kuwa asilimia 92 ya wanafunzi, hawakuwa na kitabu cha
kujisomea darasani cha Kiswahili, asilimia 97 ya wanafunzi hawakuwa na
kitabu cha kujisomea darasani cha Kiingereza, na asilimia 90 ya shule
hazikuwa na maktaba, ambazo wanafunzi wangetumia.
Asilimia 51 ya
wanafunzi hao, walikiri kuwa na vitabu vya ziada vya kujisomea nyumbani,
mbali na vitabu vya shuleni. Lakini ni asilimia 19 tu walikiri kutumia
vitabu hivyo, kumsomea mtu kwa sauti kila siku.
Wakati suala la
kujifunza kusoma linahitaji mazoezi na wanafunzi wanatakiwa kuwa na muda
na kuwa vifaa vya kujisomea, tathmini hiyo ilibainisha kuwa katika
kipindi kimoja cha dakika 30 cha somo la Kiswahili, wanafunzi walitumia
dakika saba tu kusoma.
Kuhusu mafunzo kwa walimu, ni asilimia 25 tu
ya walimu waliohojiwa, waliwahi kupata mafunzo maalumu ya awali au
wakiwa kazini ya jinsi ya kufundisha kusoma, kuandika na hisabati kwa
wanafunzi wa shule ya awali.
Walimu waliripoti kwamba walichunguza ustadi wa wanafunzi, kwa kupitia mitihani ya majaribio ya kuandika na mitihani kwa jumla.
Hata
hivyo, ni walimu wachache walioripoti, kutathmini ustadi wa wanafunzi
kwa kutumia matokeo yanayojenga (continuous assessment) ili kuchunguza
welewa wa wanafunzi katika kung'amua maudhui ya maagizo, kurekebisha
ufundishaji wao ili ukidhi mahitaji ya wanafunzi, au kupanga mafunzo ya
siku za usoni na shughuli za kujifunza.
Wakati Tanzania ikipiga vita
tangu Uhuru dhana yoyote ya ubaguzi, inaonekana pengo kati ya walionacho
na wasionacho, limeanza kuchangia ubaguzi hadi katika elimu.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, wanafunzi waliotoka katika familia tajiri, walionekana kufanya vizuri mara 15 zaidi ya wengine.
Hata
walimu wakuu wa wanafunzi waishio katika maeneo ya kipato cha chini,
walikuwa na matarajio ya chini kuhusu ustadi wa wanafunzi wao.
Asilimia
67 ya wanafunzi waishio katika maeneo tajiri, walikuwa na vitabu vya
kujisomea nyumbani, jambo ambalo lilichangia katika ufanisi na mafanikio
yao, huku kwa wanaoishi katika kipato cha chini, asilimia 39 tu ya
wanafunzi hao waliripotiwa kuwa na vitabu hivyo.
Wanafunzi wanaoishi
katika maeneo tajiri, ilibainika kuwa walikuwa na nafasi ya kufanya
mazoezi ya kusoma kwa nguvu nyumbani na kumsomea mtu nyumbani, jambo
lililochangia kuwa na mafanikio.
Akitoa maelezo ufundishaji wa KKK,
changamoto zake na nini kinafaa kuwa suluhisho, Dk Leonard Akwilapo
kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), alisema masomo ya lugha na
hisabati, ndio msingi wa kujenga stadi za KKK.
Alisema stadi hizo, husaidia ujifunzaji na welewa wa masomo mengine na hivyo masomo mengine hukazia tu ujuzi wa KKK.
Alionya kuwa udhaifu wa KKK kwa mwanafunzi ni chanzo cha kuchukia masomo, kufanya vibaya katika mitihani na hata kuacha shule.
Kwa
mujibu wa Dk Akwilapo, umuhimu wa ufundishaji wa KKK ulitiliwa mkazo
tangu enzi za Ukoloni na lengo la elimu wakati huo, lilikuwa ni kupata
wafanyakazi wachache kama makarani katika maofisi, viwanda na mashamba.
Mfumo wa elimu wakati huo wa Ukoloni, kwa Darasa la Kwanza
mwanafunzi alikuwa na masomo sita tu na ufundishaji wake ulikuwa kama
ifuatavyo.
Kwanza somo la Hesabu kwa wiki, lilikuwa na vipindi
vitano, pili kulikuwa na somo la Kusoma lililokuwa pia na vipindi vitano
na tatu somo la Kuandika, lililokuwa pia na vipindi vinne.
Somo la
Hadithi lilikuwepo na lilipewa vipindi vitano na somo la tano, lilikuwa
Kazi za Mikono, ambalo lilikuwa na vipindi vitano pia na somo la mwisho
likiwa Dini, lililopewa kipindi kimoja kwa wiki. Imeelezwa mafanikio
yalipatikana ya kukidhi mahitaji ya Mkoloni.
Baada ya Uhuru, Serikali
ilibainisha matatizo makubwa matatu ya Ujinga, Maradhi na Umasikini
ambapo katika kupambana na Ujinga, ilitilia mkazo programu mbili; moja
ufundishaji wa KKK shuleni na pili kuanzisha Kisomo cha Watu Wazima.
Kwa
mujibu wa Dk Akwilapo, mafanikio yalipatikana na yalitokana na mambo
makuu mawili, ambayo yalikuwa moja; utoaji wa mafunzo kwa walimu kazini
na pili uimarishaji wa mazingira ya kufundishia.
Programu hizo,
zimeelezwa kwamba zilikamilisha kazi yake mwaka 1980 ambapo idadi ya
masomo wakati huo kwa darasa la I Ð III, yalikuwa masomo saba na darasa
la IV Ð VII, masomo 13.
Kwa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, masomo
yalikuwa Kiswahili, Hisabati, Sanaa na Uchoraji, Kazi za Mikono, Sayansi
Kimu na Afya, Elimu kwa Michoro na Dini.
Kwa darasa la Nne mpaka
Saba, masomo yalikuwa masomo yalikuwa Kiswahili, Hisabati, English,
Historia, Jiografia, Michezo, Sanaa, Kilimo, Sayansi, Dini, Sayansi Kimu
na Afya, Kazi za Mikono na Siasa.
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo
mafanikio hayo yalianza kufifia baada ya kutokea kwa uandikishaji mkubwa
wa watoto wa darasa la kwanza.
Changamoto zilianza kujitokeza kwa
kutokea uhaba wa walimu na madarasa, kupungua kwa walimu waliopata
mafunzo na hapo kukajitokeza tatizo la stadi za KKK kwa wahitimu wa
darasa la VII.
Kujitokeza kwa changamoto hizo na zingine,
kulisababisha Serikali iunde tume ikiwemo Tume ya Makweta (1980) na Tume
ya Taifa ya Elimu (1990).
Mapendekezo ya tume hizo pamoja na mambo
mengine, yalitaka masomo ya msingi yapunguzwe kutoka masomo 13 hadi 7.
Masomo mapya yaliyopendekezwa ni Hisabati, Kiswahili, English, Sayansi,
Stadi za Kazi, Maarifa ya Jamii na Dini.
Hata hivyo, Dk Akwilapo
alibainisha kuwa idadi ya masomo, si sababu ya kuporomoka kwa elimu kwa
kuwa katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania wanafunzi wana masomo
machache zaidi.
Kwa sasa imeelezwa kuwa mwanafunzi wa darasa la
Kwanza na la Pili, anasoma kwa wastani wa juu masomo tisa tu ambayo ni
Hisabati, Kiswahili, English, Sayansi, Tehama, Stadi za Kazi, Haiba na
Michezo, French (Chaguzi), Dini.
Kwa Burundi, darasa la Kwanza na la
Pili, ni masomo 11, ambayo ni Mathematics, Kirundi, English, Kiswahili,
French, Environment, Physical Education, Religious Education, Musical
Expression, Human Training Education na Civics.
Nchini Kenya,
mwanafunzi wa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, masomo pia ni 11, ambayo
ni Math, English, Kiswahili, Creative Arts , Science, Social Studies,
Physical Education, Mother Tongue, Life Skills Education, Kenyan Sign
Language, Religious Education (CRE, IRE, Hindu Religious Education).
Nchini
Rwanda, wanafunzi wa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, anasoma masomo
kumi ambayo ni Kinyarwanda, Mathematics, English, Social Studies,
Sports, Religious Education, Music, Fine Art, Cultural Activities na
Practical Work.
Uganda wao ni masomo tisa kwa mwanafunzi wa darasa la
Kwanza mpaka la Tatu, ambayo ni Mathematics, Literacy I, Literacy II,
English, Creative, Performing Arts (Music, Art and Crafts), Physical
Education, Religious Education, Free Activity na Oral Literature.
Dk
Akwilapo alishauri ili kupata suluhisho la kinachotokea, mafunzo ya
walimu vyuoni yaimarishwe katika ufundishaji wa KKK na matumizi ya zana
anuai.
Pia, alipendekeza mafunzo ya walimu kazini, yanayotilia mkazo ufundishaji wa KKK yapewe kipaumbele.
Pendekezo
lingine ni kupunguza idadi ya wanafunzi darasani, wasizidi 35 kwa
darasa, ili walimu watoe msaada kwa kila mwanafunzi.
Viwango vya
vyumba vya madarasa imependekezwa view na ukubwa unaoruhusu kufanyika
kwa ufasaha kwa vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji.
Msomi huyo
kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, alipendekeza vitabu bora vya
kufundishia KKK, vipatikane na vitabu vya kiada, viwepo pia vitabu vya
ziada vyenye mvuto kwa wanafunzi (hadithi za kusisimua).
Mazingira ya
kujifunza na kufundishia yamependekezwa kuwa rafiki kwa wanafunzi ili
kupunguza utoro wa wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za
madawati na viti, chakula cha mchana, maji safi na salama, vyoo safi na
salama vitendea kazi vingine wezeshi.
Upatikanaji wa zana anuai za
kufundishia KKK umetajwa kuwa wa muhimu, zikiwemo kadi na chati za
herufi za alfabeti, kadi za namba, picha, kadi za maneno na sentensi.
Viongozi
wameshauriwa kuhamasisha walimu kutengeneza vifaa hivyo kwa kutumia
malighafi rahisi na zinazopatikana katika mazingira yao.
Jamii pia imetakiwa kushiriki katika elimu, hasa wazazi na walezi ili watambue wajibu wao katika elimu za watoto.
Kwa
mujibu wa Dk Akwilapo, tafiti zimeonesha kuwa wazazi/walezi
wanaofuatilia na kuwasaidia watoto wao kujifunza, huwasaidia kupata
matokeo chanya.
Pia, shule zimetakiwa kuwa na viwanja vya michezo na walimu wa michezo, ili kuimarisha mazingira ya shule na kupunguza utoro.
إرسال تعليق