Baadhi ya nchi zinataka Sudan mbili ziungane tena”

Rais Omar al Bashir wa Sudan amesema baadhi ya madola makubwa duniani yanataka Sudan mbili ziungane tena. 
Akihutubia wajumbe wa chama tawala cha Kongresi ya Taifa ya Sudan, Al Bashir amesema madola kadhaa duniani yameomba radhi kwa sababu ya kuunga mkono kutengana kwa Sudan mbili. 
Rais wa Sudan amebainisha kuwa baada ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan, maadui wa Khartoum walishangazwa na muqawama ulioonyeshwa na Sudan baada ya utengano huo, na leo hii wanaonyesha kujuta na kuitaka Sudan ikubali suala la kuungana tena Sudan mbili. 
Amesema kuungana sehemu nyengine na ardhi ya Sudan, mbali na kuhitajia ridhaa ya serikali kutalazimu pia kuitishiwa kura ya maoni ili kupata msimamo wa wananchi. 
Itakumbukwa kuwa asilimia 99 ya wakaazi wa Sudan Kusini waliunga mkono kujitenga eneo hilo na Sudan katika kura ya maoni iliyoitishwa mwezi Januari mwaka 2011, na mnamo tarehe 9 Julai mwaka huo huo Sudan Kusini ikajitangazia uhuru na kujitenga rasmi na Sudan. 
Baadhi ya duru za habari zimefichua kuwa viongozi wa Marekani na Umoja wa Ulaya wanahisi kwamba katika hali iliyopo hivi sasa ni muhali kwa nchi mbili za Sudan na Sudan Kusini kuishi kwa amani na masikilizano na hivyo wanazitaka nchi hizo zikubali kuanzisha shirikisho la mkataba mkabala na kupatiwa msaada mkubwa wa fedha na madola makubwa duniani.

Source: kiswahili.irib.ir

Post a Comment

أحدث أقدم