Ligi ya
Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2013/2014 itakayochezwa kwa mkondo
mmoja inaanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vya
timu tisa kila kimoja.
Timu
itakayoongoza katika kila kituo cha ligi hiyo itakayomalizika Juni 2
mwaka huu ndiyo itakayopata tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) kwa msimu ujao wa 2014/2015. Vituo hivyo ni Mbeya, Morogoro na
Shinyanga.
Kituo cha
Morogoro ambapo mechi zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kitakuwa na timu za
Abajalo FC ya Dar es Salaam, African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC
(Shinyanga), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Mji Mkuu FC
(Dodoma) Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na
Pachoto FC (Mtwara).
Uwanja wa
Sokoine ndiyo utakaotumika katika kituo cha Mbeya chenye timu za AFC ya
Arusha, Magereza FC (Iringa), Mpanda United SC (Katavi), Njombe Mji FC
(Njombe), Panone FC (Kilimanjaro), Tanzanite SC (Manyara), Town Small
Boys (Ruvuma), Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC (Morogoro).
Timu za
Eleven Stars ya Kagera, Geita Veterans (Geita), JKT Rwamkoma FC (Mara),
Mbao FC (Mwanza), Milambo SC (Tabora), Mvuvumwa FC (Kigoma), Simiyu
United (Simiyu), Singida United (Singida) na Wenda FC (Mbeya) zitacheza
katika kituo cha Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage.
Orodha ya
usajili wa wachezaji wa timu zote kwa ajili ya RCL imetumwa kwa vyama
vya mpira wa miguu vya mikoa na klabu zote za RCL, FDL na Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kwa ajili ya kipindi cha pingamizi ambacho kinamalizika
Mei 4 mwaka huu.
Hata
hivyo, katika usajili uliowasilishwa na baadhi ya klabu imebainika kuwa
kuna wachezaji walioshiriki VPL, FDL na wale U20 za VPL waliocheza ligi
msimu wa 2013/2014.
Kiongozi
yeyote atakayebainika katika udanganyifu kwenye usajili huo, awe wa
klabu au chama cha mpira wa miguu cha mkoa atachukuliwa hatua kwa mujibu
wa kanuni ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya kimaadili vya TFF kwa
hatua zaidi.
Ligi ya Mabingwa haina mdhamini, hivyo timu shiriki zitajitegemea kwa kila kitu, na zinakumbushwa kuwahi vituoni.
MALAWI KUWASILI MEI 1 KUIVAA STARS
Timu ya
Taifa ya Malawi (Flames) inatarajiwa kuwasili nchini Mei 1 mwaka huu kwa
ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Mei 4
mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Flames
yenye msafara wa 31 utakaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Chama cha Mpira wa Miguu cha Malawi (FAM) utaingia Mbeya kwa usafiri wa
barabara. Wachezaji katika msafara huo ni 20.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha
mpya, Mart Nooij tayari ipo jijini Mbeya kujiwinda kwa mechi hiyo ikiwa
ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Zimbabwe
itakayochezwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.
إرسال تعليق