
Wiki
hii Bunge Maalumu la Katiba limeahirishwa, kupisha Bunge la Bajeti
kuanza vikao vyake vya bajeti kwa mwaka mpya wa fedha wa 2014/15.
Hata hivyo, Bunge hilo limeahirishwa
likiwa limegawanyika vipande, baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge hilo Aprili 16, wakipinga
kejeli, matusi na mambo mengine ya ukiukwaji wa taratibu yaliyokuwa
yakifanywa na baadhi ya mawaziri nje ya Bunge.
Kutoka kwa Ukawa nje unaojumuisha vyama
vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, DP na wajumbe 25 kutoka kundi la 201
hakukuzuia Bunge hilo kuendelea na vikao vyake. Bunge hilo limeahirishwa
Agosti 5, litakapokutana tena mjini Dodoma kuendelea na majadala wa
kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Kundi la Tanzania Kwanza linalojumuisha
wajumbe wengi wa CCM, wamekuwa wakiwapiga vijembe kuwa warudi bungeni
kuendelea na mjadala huo kwani Katiba haitengenezwi nje ya Bunge.
Jukata yasaka suluhu
Kutokana na mgawanyiko huo kuonyesha
kuligawa taifa na kuwaacha wananchi wakiwa njiapanda juu ya hatima ya
kupata Katiba Mpya, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) linajipambanua
kutaka kusaka suluhu ya mvutano huo.
Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba
anasema, Jukwaa hilo linajitolea kusaka suluhu kwa kuratibu maridhiano
ya makundi yanayovutana ya Ukawa na la Tanzania Kwanza.
Anasema lengo la kusaka maridhiano hayo
ni kuhakikisha kabla ya Bunge hilo kuanza Agosti 5, kunakuwapo
maridhiano, yatakayowezesha wajumbe wote wanakuwa kitu kimoja katika
kujadili maudhui ya rasimu, licha ya tofauti zao za kiitikadi na
kimisimamo.
Kibamba anasema wameamua kuwaalika
wataalamu ambao wana uzoefu wa siku nyingi katika masuala ya sheria
kusimamia maridhiano hayo, yatakayojenga umoja na mshikamano katika
taifa.
Wataalamu hao kwa mujibu wa Kibamba ni
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Barnabas Samatta anayekuwa mwenyekiti,
Profesa Patrice Lumumba kutoka nchini Kenya ambaye atakuwa msuluhishi
mwenza sambamba na uwepo wa makundi ya viongozi kutoka Ukawa, Tanzania
Kwanza, vyama vya siasa, asasi za wananchi na taasisi zote muhimu
zilizoguswa na mchakato huu.
“Katika kujenga Katiba yenye kuwajali
wananchi, tunaomba kila upande kuridhia kukutana na kutokuwa na misimamo
mikali ili kuhakikisha tunawaunganisha na kuendelea na mchakato huo
kama kawaida,” anasema Kimbamba.
Kuhusu uhalali wa Bunge hilo kuendelea na
mijadala licha ya Ukawa kutoka nje, anasema sheria za Jumuiya ya Madola
kwa mabunge ya Katiba kundi moja linapotoka nje kwa tamko, Bunge hilo
hutakiwa kusitishwa.
“Ukawa wametoka nje tena wakiwa zaidi ya
190, Bunge lilitakiwa kusitishwa na kupata maridhiano kwanza si kama
wanavyotumia akidi vibaya kuliendesha Bunge hilo,” anasema Kibamba.
Aliongeza: “Jukata bado inaamini kwamba
mwaka 2014 Katiba Mpya haitapatikana, hivyo kunahitajika kufanyiwa
marekebisho makubwa Katiba ya sasa hasa vifungu vinavyohusu uchaguzi ili
kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa amani.”
Maoni ya wadau
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Watu wenye Ulemavu Tanzania, Felician Mkude anasema, maridhiano
yanahitajika ili kuweza kupata uwakilishi ndani ya Bunge hilo kwa
ufasaha.
Anasema, kuendelea na mvutano kuhusu aina
gani ya Muungano, si jambo la maana na kinachotakiwa kufanyika ni
wananchi kupiga kura ya muundo gani unaostahili.
“Huwezi kuwalazimisha watu kuamua jambo
ambalo hawalitaki kama ni muundo wa Muungano tunaomba wananchi ndiyo
waamue, lakini yote hayo Katiba yetu inatakiwa kubainisha mambo
mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu na haki zao zote,” anasema
Mkude.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Idd
Makombe anasema mvutano uliokuwa ukiendelea bungeni kuhusu muundo wa
Muungano haukuuimarisha bali unauvuruga.
Dk Makombe anasema, uwazi na maridhiano ndio utakaowezesha kuipata Katiba Mpya yenye kuwajali Watanzania wote.
“Kunahitajika kufanyika kwa kura ya maoni
kuhusiana aina gani ya Muungano wananchi wanataka, kwani hivi sasa watu
hatuaminiani na huwezi kumlazimisha mtu jambo ambalo halitaki, hivyo
pande zote mbili zifikie maridhiano kwa amani,” anasema Dk Makombe.
Mhadhiri wa Chuo Kiuu cha Dar es Salaam,
Idara ya Sayansi na Utawala, Richard Mbunda anasema nchi inapitia katika
kipindi kigumu kutokana na kauli na mienendo mbalimbali inayoendelea
kujitokeza.
Mbunda anasema viongozi wa kidini na
Serikali wanapotoa kauli wanatakiwa kuwa makini, kwani zinaweza
kuliingiza taifa katika vurugu za kidini au za kisiasa.
Kauli ya Rais Kikwete
Akizungumza na Vijana na Wazee wa Chama
Cha Mapinduzi kutoka Tanzania Bara na Visiwani juzi kwenye Ukumbi wa PTA
Sabasaba, Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete amewataka Ukawa kurejea
bungeni kuendelea na mjadala wa kutunga Katiba.
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
limeingilia kati mpasuko uliojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba kwa
kusaka wasuluhishi watakaorejesha maridhiano ya pande mbili
zinazokinzana.
Rais Kikwete anasema, katika kuandika
Katiba ya Watanzania kunahitajika kufanya maridhiano ili kuhakikisha
mchakato huo unamalizika salama kwa wananchi kupata Katiba yenye kujali
masilahi yao.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment