WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likikutana
kesho kwa ajili ya kupokea taarifa za kamati na kuanza mjadala wa jumla
kwa wajumbe wote, Rais Jakaya Kikwete ameridhia ombi la kulisitisha
kuanzia Aprili 28 hadi Agosti mwaka huu, ili kupisha Bunge la Bajeti
liendelee na vikao vyake.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo Februari 18,
mwaka huu, wajumbe wameweza kujadili sura mbili pekee za rasimu ya
katiba ambazo hata hivyo uamuzi wake utategemea majadiliano
yatayofanyika baada ya kamati zote kuwasilisha taarifa zao kuanzia
kesho.
Bunge hili limetumia takribani wiki tatu
kujadili kanuni zake, na hivyo kupunguza muda wake wa siku 70 uliowekwa
kisheria bila kuanza kujadili sura na ibara za rasimu hiyo.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta
alizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kukutana na viongozi
wawili wakuu wa dini, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam,
Mwadhama
Sitta alisema kuwa juzi alipokutana na
Rais Kikwete alimueleza umuhimu wa kuongeza muda kwa Bunge hilo ambapo
alionyesha nia ya kulisogeza hadi Agosti mwaka huu.
Alisema kwa sasa wapo katika hatua za
mwisho za kumalizia kuipitia sura ya kwanza na ya sita ya rasimu
inayozungumzia muundo wa serikali ambapo kesho wenyeviti wa kamati 12 za
Bunge hilo watawasilisha taarifa zao kwa mtiririko bila majadiliano.
“Wakishawasilisha tunatarajia wiki ijayo
wajumbe wote kupata fursa ya kuchangia kwa uwiano, lakini niseme kuwa
sina hakika kama kwa muda uliosalia tutakuwa tumemaliza maana sheria
namba 83 ya mabadiliko ya katiba inasema ni siku 70 tu, hivyo itakuwa ni
aibu rasimu ipitiwe sura mbili pekee kati ya sura 17 zilizopo,”
alisema.
Alieleza kuwa baada ya Bunge la Katiba
kuahirishwa, litaanza Bunge la Jamhuri kwa ajili ya bajeti hadi Juni, na
Julai wataitumia kwa kuwapa wabunge nafasi ya kutembelea majimbo yao
ili Agosti Bunge la Katiba liweze kurejea tena kuendelea kupitia sura
nyingine.
Sitta alifafanua kuwa baada ya Bunge
Maalumu kuhitimisha kazi yao, watakabidhi kwa Rais Kikwete na mwenzake
wa Zanzibar rasimu ya katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kuiwasilisha
kwa wananchi waweze kuipigia kura ya ama kuikubali au kuikataa.
“Unajua licha ya kuwepo purukushani
nyingi za hapa na pale nia ya wabunge wengi ni kupata katiba bora na
nzuri hivyo mchakato utakamilika tu,” alisema.
Akizungumzia sababu ya kuwatembelea
viongozi hao, Sitta alisema kuwa katiba inamgusa kila raia na ndiyo
sababu kama mwenyekiti wa Bunge Maalumu aliamua kukutana nao ili
kuwafahamisha wametoka wapi, wako wapi na nini kinaendelea.
Sitta aliongeza kuwa kwa kutambua nafasi
ya viongozi hao katika jamii hasa kwa kuongoza kundi kubwa la
Watanzania, amekutana nao ili kuwasihi na kuelimisha wananchi wengi
wanaowaongoza ikiwemo kuliombea Bunge hilo litoke salama.
Sitta atia shaka
Katika hatua nyingine, ziara ya Sitta kwa
viongozi wakuu wawili wa dini imeacha maswali mengi ambapo baadhi ya
watu wameitafsiri kama kampeni ya Chama Cha Mapinduzi kutafuta uungwaji
mkono katika kutetea mfumo wake wa muundo wa serikali mbili.
Hatua hiyo inatokana na msimamo wa
viongozi hao wawili kuwa sambamba na ule wa CCM katika suala la muundo
wa Muungano ambapo wote wanataka serikali mbili.
Vyanzo vyetu vya ndani vimedokeza kuwa
kwa muda mrefu CCM ilikuwa ikitafuta namna ya kupenyeza karata yake ili
kupata uungwaji mkono wa Kanisa Katoliki ambalo lina wafuasi wengi
nchini.
Hivi karibuni, Kardinali Pengo
alilazimika kukutana na vyombo vya habari ili kuweka sawa taarifa
iliyokuwa imetolewa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu wa
kanisa hilo kupitia kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paul Ruzoka
akitaka mapendekezo ya wananchi kwenye rasimu kuhusu serikali tatu
yaheshimiwe.
Alisema maoni hayo ni yake binafsi wala
si msimamo wa kanisa hilo huku akiweka bayana kuwa yeye ni muumini wa
serikali mbili, lakini pia akasisitiza kwamba hayo ni maoni yake.
Wapinzani wajipanga
Kutoka mjini Dodoma, taarifa zinaeleza
kuwa wajumbe wa kambi ya upinzani wamejipanga ipasavyo kutengeneza
taarifa ya maoni kinzani kwa ajili ya kukata ngebe za CCM, wakidai
inatumia wingi wake kutaka kubadili maudhui ya vifungu vya rasimu kutoka
mapendekezo ya serikali tatu kwenda mbili.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa
wajumbe hao kupitia maoni yao kinzani ya wachache, wameandaa hoja kadhaa
za kulishawishi Bunge zima ili kuhakikisha mapendekezo ya muundo wa
serikali tatu unaopendekezwa na wananchi kupitia rasimu ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba yanapitishwa yalivyo.
“CCM walitegemea kutumia kamati kuburuza
wajumbe ili kupata theluthi mbili ya kura kwa pande zote waweze kubadili
rasimu watakavyo kutoka serikali tatu kwenda mbili, lakini
imeshindikana baada ya kukosa kura hizo kwenye takribani kamati zote.
“Sasa wameandaa taarifa za kuleta bungeni
wakionyesha wajumbe wengi kwenye kamati wamependekeza serikali mbili,
na hivyo wamebadili vifungu vya rasimu vionyeshe hivyo, hatutakuwa
tayari kwa hili, nakuhakikishia moto utawaka, sisi tumejipanga kwa hoja
wao wanatumia wingi wao bila hoja… tutaona,” alisema mtoa taarifa.
Chanzo: Tanzania Daima
إرسال تعليق