MAMA KIKWETE AWAHIMIZA WALEZI NA WAZAZI KUWAPATIA WATOTO UJI NA UGALI WA DONA

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

Wazazi na walezi wameshauriwa kuwapa watoto uji na ugali wa unga wa dona na siyo sembe kwakuwa unga wa dona una kiini cha mahindi ambacho kinakirutubisho kinachosaidia ukuaji na uwezo wa akili ya binadamu.

Ushauri huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea  kwa nyakati tofauti  na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho  katika matawi ya Mnazi Mmoja, Amani na  Muungano yaliyopo katika kata  ya  Mingoyo wilaya ya Lindi mjini.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete  alisema siku hizi watu wengi wanapenda kutumia unga wa sembe ambao hauna virutubisho vyovyote katika mwili kwani unapokoboa mahindi kiini kinabaki katika pumba ambazo wanapewa wanyama na binadamu kukosa virutubisho vya muhimu katika miili yao.

“Watoto wetu wanatakiwa kupata lishe bora ambayo itawajenga akili zao, wasiwe na mambo mengi na kufanya zaidi ya kwenda shule na kusoma . Wakiwa shuleni watahitaji kunywa uji au kula chakula cha mchana hivyo basi ni muhimu kwa walezi kuchangia  chakula cha mtoto kwakuwa mwanafunzi akishiba ataweza kusoma vizuri na kufaulu masomo yake .

Katika suala la kuchangia chakula cha mtoto si lazima upeleke fedha lakini kama utajuwa  mtoto wako anakula chakula kiasi gani kwa wiki au mwezi unaweza kupeleka  chakula shuleni  kama ni mchele, mahindi au maharage hii  inategemea na aina ya chakula kinachopikwa shuleni hapo kwa kufanya hivyo mwanafunzi atasoma akiwa ameshiba”, alisema Mama Kikwete. 

Mama Kikwete alimalizia kwa kuwaomba viongozi hao kukaa na watoto wao na kuwaeleza historia ya nchi yao na umuhimu wa kutunza amani, umoja na mshikamano kwani vitu hivi vikitoweka wao ndiyo watakaopata tabu lakini kama jamii itaishi maisha ya upendo amani itatawala.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi Mzee Ally  Mtopa aliwataka viongozi hao kuwahimiza wananchi kujenga nyumba bora za matofali ya kuchoma na siyo nyumba za miti katika hilo wao wawe ni mfano wa kuigwa  kwani moja ya sera ya CCM ni kutunza mazingira  hii ikiwa ni pamoja na kutokata miti hovyo.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Lindi Haji Tajiri aliwataka viongozi hao kuzingatia viapo wanavyoapa hii ikiwa ni pamoja na kutokupokea wala kutoa  rushwa, kuwa waaminifu na watiifu  na kusema ukweli daima kwani katiba ya CCM ndiyo imewaweka hapo walipo waiheshimu. 

Wakati huo huo  Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye alikuwa safarini akitokea kijijini kwao Mtama  alikatiza  safari yake na kwenda kuwasalimia wanachama wa tawi la Mnazi Mmoja,   alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi nzuri anayoifanya ya kufanya mikutano na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi hii ikiwa ni kazi mojawapo ya kukijenga chama hicho.

“Kama WANEC wote wangefanya hivi hakika chama chetu kingefika mbali na kupata ushindi mkubwa katika chaguzi mbalimbali kwani wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa  wanatakiwa kupita kwenye matawi yote katika wilaya zao, kukutana na wanachana na kusikiliza kero zao na siyo kukaa mbali nao kwa kuwa waliomba  nafasi hii ili waweze kuwatumikia  watu”, alisema Nnauye.

Alisema  Mama Kikwete anastahili pongezi kwa kuwa  anafanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani za CCM katika mambo ya afya, elimu na  kuwainua wanawake kiuchumi . 

Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Post a Comment

Previous Post Next Post