Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Wazazi
na walezi wameshauriwa kuwapa watoto uji na ugali wa unga wa dona na
siyo sembe kwakuwa unga wa dona una kiini cha mahindi ambacho
kinakirutubisho kinachosaidia ukuaji na uwezo wa akili ya binadamu.
Ushauri
huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati
akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya
Chama hicho katika matawi ya Mnazi Mmoja, Amani na Muungano yaliyopo
katika kata ya Mingoyo wilaya ya Lindi mjini.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema siku
hizi watu wengi wanapenda kutumia unga wa sembe ambao hauna virutubisho
vyovyote katika mwili kwani unapokoboa mahindi kiini kinabaki katika
pumba ambazo wanapewa wanyama na binadamu kukosa virutubisho vya muhimu
katika miili yao.
“Watoto
wetu wanatakiwa kupata lishe bora ambayo itawajenga akili zao, wasiwe
na mambo mengi na kufanya zaidi ya kwenda shule na kusoma . Wakiwa
shuleni watahitaji kunywa uji au kula chakula cha mchana hivyo basi ni
muhimu kwa walezi kuchangia chakula cha mtoto kwakuwa mwanafunzi
akishiba ataweza kusoma vizuri na kufaulu masomo yake .
Katika
suala la kuchangia chakula cha mtoto si lazima upeleke fedha lakini
kama utajuwa mtoto wako anakula chakula kiasi gani kwa wiki au mwezi
unaweza kupeleka chakula shuleni kama ni mchele, mahindi au maharage
hii inategemea na aina ya chakula kinachopikwa shuleni hapo kwa kufanya
hivyo mwanafunzi atasoma akiwa ameshiba”, alisema Mama Kikwete.
Mama
Kikwete alimalizia kwa kuwaomba viongozi hao kukaa na watoto wao na
kuwaeleza historia ya nchi yao na umuhimu wa kutunza amani, umoja na
mshikamano kwani vitu hivi vikitoweka wao ndiyo watakaopata tabu lakini
kama jamii itaishi maisha ya upendo amani itatawala.
Naye
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi Mzee Ally Mtopa aliwataka viongozi hao
kuwahimiza wananchi kujenga nyumba bora za matofali ya kuchoma na siyo
nyumba za miti katika hilo wao wawe ni mfano wa kuigwa kwani moja ya
sera ya CCM ni kutunza mazingira hii ikiwa ni pamoja na kutokata miti
hovyo.
Kwa
upande wake Katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Lindi Haji Tajiri
aliwataka viongozi hao kuzingatia viapo wanavyoapa hii ikiwa ni pamoja
na kutokupokea wala kutoa rushwa, kuwa waaminifu na watiifu na kusema
ukweli daima kwani katiba ya CCM ndiyo imewaweka hapo walipo
waiheshimu.
Wakati
huo huo Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye alikuwa
safarini akitokea kijijini kwao Mtama alikatiza safari yake na kwenda
kuwasalimia wanachama wa tawi la Mnazi Mmoja, alimpongeza Mama Kikwete
kwa kazi nzuri anayoifanya ya kufanya mikutano na viongozi wa
Halmashauri kuu ya tawi hii ikiwa ni kazi mojawapo ya kukijenga chama
hicho.
“Kama
WANEC wote wangefanya hivi hakika chama chetu kingefika mbali na kupata
ushindi mkubwa katika chaguzi mbalimbali kwani wajumbe wa Halmashauri
Kuu Taifa wanatakiwa kupita kwenye matawi yote katika wilaya zao,
kukutana na wanachana na kusikiliza kero zao na siyo kukaa mbali nao kwa
kuwa waliomba nafasi hii ili waweze kuwatumikia watu”, alisema
Nnauye.
Alisema
Mama Kikwete anastahili pongezi kwa kuwa anafanya kazi kubwa ya
kutekeleza ilani za CCM katika mambo ya afya, elimu na kuwainua
wanawake kiuchumi .
Mama
Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini
alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya
kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na
viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
إرسال تعليق