HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA
RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIFA HAMAD SIKU YA UPANDAJI MITI KITAIFA
KATIKA ENEO LA BARABARA YA JENDELE - CHEJU - UNGUJA UKUU, MKOA WA KUSINI UNGUJA
TAREHE 20 APRIL, 2014
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa
Kusini Unguja;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama
na Serikali
Waheshimiwa Wananchi, Mabibi na
Mabwana
Assalm Alaykum.
Kwanza
kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye wingi wa rehema kwa
kutujaalia neema ya uhai tukaweza kukutana hapa wakati huu tukiwa wazima.
Pia
napeda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyote mlioshiriki katika kuandaa kampeni
ya Upandaji Miti Kitaifa na kuamua kunialika mimi nije kujumuika nanyi katika
tukio hili muhimu. Vile vile nawashukuru wananchi nyote mlioweza kufika hapa
kwa wingi. Kuhudhuria kwenu katika shughuli hii ya upandaji wa miti kunaonesha
ni jinsi gani mnavyo thamini juhudi za kuistawisha nchi yetu, ili iwe na
mazingira mazuri, jambo ambalo ni muhimu sana kwa maisha yetu, vizazi vyetu na
kwa maendeleo ya nchi yetu kwa jumla.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Tunasema
kuwa siku ya leo ni muhimu sana kwa sababu ina lenga kutukumbusha hostoria ya
visiwa vyetu vya Unguja na Pemba. Historia ya utajiri mkubwa wa miti ya asili
na matunda ya aina mbali mbali. Lakini kutokana na tabia zetu mbaya sisi binaadamu
zimepelekea matumizi mabaya ya rasilimali hizo na matokeo yake ni kupotea kwa
miti mingi hapa nchini.
Wazee
wetu nadhani bado mnakumbuka kwamba visiwa hivi vilikuwa vikijuilikana kama Visiwa vya Kijani. Hali hii ilitokana
na ukweli kwamba visiwa vilikuwa vimepambwa kwa mandhari nzuri ya miti ya aina
mbali mbali. Hivyo basi kila mgeni alitamani kutembelea na wakati mwengine
kuamua kuishi hapa hapa, kutokana na utajiri huo mkubwa wa aina mbali mbali za miti
na wanyama.
Hata
hivyo, nadhani tunakubalina sote kwamba hivi sasa hali hiyo imeanza kubadilika
kwa kasi, kuna maeneo mengi ya visiwa vyetu miti imeadimika sana na mengine
kutishiwa kuwa jangwa, kutokana na ukataji wa miti uliokithiri ambao unafanywa
bila ya kuzingatia taratibu zozote.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Kuongezeka
kwa mahitaji muhimu ya nishati kama vile makaa na kuni, majengo, ardhi kwa
ajili ya makaazi na kilimo na shughuli nyengine za maendeleo kunazidisha kuongezeka
kwa kasi ya ukataji wa miti na uharibifu wa misitu hapa nchini.
Takwimu
za hivi karibuni za sensa ya miti zinaonesha wazi kwamba idadi ya miti
inapungua sana. Zimeonesha kwamba maeneo mengi ya misitu pamoja na mashamba
yamegeuzwa kuwa makaazi ya watu na hivyo kuendelea kukatwa kwa kasi. Miongoni
mwa miti inayokatwa sana ni miti mikubwa, miti ya matunda na ya viungo. Ardhi zenye rutba ambazo zimetengwa kwa
kilimo hivi sasa ndizo zinazovamiwa kwa ujenzi na hivyo kupunguza zaidi idadi
ya miti na uzalishaji wa matunda na chakula.
Takwimu
hizo zimeonesha kwamba juzi tu, yaani mwaka 1997 visiwa vya Unguja na Pemba
vilikuwa na miti yenye mita za ujazo wa 10.3 milioni, lakini kima hicho
kilipungua hadi kufikia mita za ujazo 8.6 milioni mwaka jana wa 2013.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Hali
halisi ni kwamba uwezo wa misitu na miti yetu ya kuzalisha rasilimali ambao ni
mita za ujazo 485,532 (cm3) kwa mwaka, wakati ambapo mahitaji yetu
mita za ujazo 1,340,067 (cm3) kwa mwaka. Hivyo basi kutokana na
taarifa hizo, nchi yetu ina upungufu wa mahitaji ya rasilimali zitokanazo na
miti, yaani kuni, makaa, mbao na majengo, za kiasi cha mita za ujazo 854,537
(cm3) ambazo zinabidi zifidiwe kutoka nje ya nchi. Hali hii
haioneshi picha nzuri hata kidogo kwa mustakabali wa nchi, hasa ikizingatiwa
kuwa mahitaji makubwa tuliyonayo ya miti kwa ajili ya nishati.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Siku
ya upandaji miti Kitaifa imeteuliwa rasmi na Serikali ili kuwatanabahisha na
kutoa changamoto kwa wananchi wa visiwa hivi kuhusu jukumu letu la kupanda na
kuitunza miti na uhifadhi wa mazingira ya nchi yetu. Athari za mabadiliko ya
tabia ya nchi si tatizo la Kiulimwengu pekee, bali hata nasi hapa Zanzibar
tunaathirika sana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa. Taathira tunazokabiliana
nazo ni pamoja na kubadilika kwa miongo, mvua zisizo za uhakika, mafuriko,
vimbunga, ukame, kuzuka kwa mioto, maradhi na athari nyenginezo. Matokeo yake
ni pamoja na kupungua kwa mazao ya kilimo, nishati, kuni, miti ya kujengea na
kuongezeka kwa maradhi ya binaadamu, wanyama na mimea.
Waheshimiwa Wananchi
Miti
husaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na vyanzo vya
maji, chemchem, mito, kujikinga na upepo mkali na kusaidia upatikanani wa mvua
ambayo ni muhimu kwa shughuli zetu za kilimo na ustawi wa maisha yetu binaadamu
na wanyama.
Aidha,
miti ni chanzo cha pato la wananchi na Taifa kwa jumla, kwa mfano karafuu ni
miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni kwa nchi yetu na pia inachangia
nishati kuu ya kuni na makaa tunayotumia. Pia inatumika kwa shughuli za ujenzi
wa nyumba, mbao, chakula na hata madawa ya asili. Tukumbuke kuwa misitu ndio
makaazi na mazalia muhimu ya wanyama, ndege na samaki, hususan katika maeneo ya
miti ya mikoko.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Inabidi tuzidi kukumbuka kwamba maisha yetu
kwa kiasi kikubwa yanategemea kuwepo kwa miti kwa ajili ya mahitaji yetu muhimu
ya kila siku. Kuimarika kwa ardhi ya kilimo, yaani kuwa na rutba kunahitaji
sana kuwepo kwa miti ambayo hutoa virutubisho ambavyo ndio chakula cha mimea tunayoipanda. Chemchem za maji
haziwezi kuimarika bila ya kuwepo kwa miti. Hivyo basi ni wajibu wetu kuendelea
kuihifadhi, kuitunza na kuipanda kwa wingi, ili tuweze kuyanusuru maisha na
mazingira yetu hivi sasa na siku zijazo.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Ulimwengu
hivi sasa umehamanika kutokana na matatizo makubwa yanayosababishwa na
mabadiliko ya hali ya hewa. Uhifadhi wa mazingira yetu ni sehemu ya suluhisho
la kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira ambazo zinasababisha mabadiliko ya
hali ya hewa tusivyotarajia. Pale tutakapomudu kutunza vyema miti yetu ya asili
na tunayoipanda, ikiwemo ya matunda na viungo basi ni dhahiri kwamba tutakuwa
tumepiga hatua kubwa za kukabiliana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa.
Juhudi
kubwa hazina budi kuchukuliwa katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu na
thamani ya miti yetu kijamii, kiuchumi na kimazingira. Ni lazima tufahamu
kwamba majanga mengi ya kimazingira yataendelea kutokea ikiwa tutaendelea
kuikata miti hiyo ovyo na bila ya utaratibu.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Kwa
upande wa Serikali mkazo mkubwa tumeuweka katika suala zima la upandaji wa miti
nchini. Mkazo huu umewekwa katika upandaji wa miti aina mbali mbali kwani miti
yote ina faida nyingi kama ambavyo niliwaeleza hapo awali. Hata hivyo suala
zima la upandaji wa miti ya misitu, matunda, viungo na mikarafuu, Serikali nayo
imelipa msukumo zaidi katika kipindi hichi.
Hakuna
asiyefahamu umuhimu wa zao la Karafuu kwa uchumi wetu. Zao hili kwa kipindi
kirefu limekuwa likikabiliwa na matatizo makubwa katika uendelezaji wake. Hali
hii imechangiwa sana na kuporomoka kwa bei yake katika soko la Dunia.
Uzalishaji mdogo pia umesababishwa na maradhi, kuzeeka kwa miti hiyo pamoja na
matunzo hafifu, hali iliyopelekea miti ya mikarafuu kukatwa kwa wingi, na hata
ile iliyosalia iliachwa hadi kufa bila ya kupata huduma zozote. Hali hii
ilipelekea visiwa vya Zanzibar kuanza kupoteza sifa yake ya kuwa ni miongoni
mwa wazalishaji wakubwa wa karafuu zenye ubora unaosifika hapa Ulimwenguni.
Mbali
na matatizo hayo katika uzalishaji wake, zao la karafuu linakabiliwa na tatizo
jengine kubwa la kusafirishwa kwa magendo. Lakini pia jambo baya zaidi hivi
karibuni kumezuka tabia ya baadhi ya watu kuitorosha kwa magendo miche ya
mikarafuu na kuipeleka nje ya nchi. Kwa kweli hili ni janga kubwa ambalo halina
budi kupigwa vita kwa nguvu zote. Serikali imeendelea kuwapa motisha wakulima
wa mikarafuu ili kuinua uchumi na maisha yao na kuinua pato la Taifa kwa jumla.
Pia Serikali inaendelea kutoa miche bure na vivutio vyengine, ili kuhakikisha
wakulima wetu wanafaidika na jasho la kazi yao.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Tupandeni
kwa wingi mikarafuu pamoja na mazao mengine yakiwemo ya viungo na matunda.
Haiba na mandhari njema ya nchi hii yataendeela kuwa mazuri iwapo upatikanaji
wa matunda mbali mbali na viungo utaendelea kushamiri. Hata Miji, Vijiji pamoja
na barabara zetu zitazidi kupendeza ikiwa zitaendeela kutunzwa kwa kupandwa
miti ya vivuli na ya matunda.
Uzinduzi
tunaoufanya leo katika barabara hii ya Jendele hadi Unguja Ukuu ni muendelezo
wa kampeni hii ya upandaji miti katika barabra na maeneo mengine ya jamii.
Lengo letu kuu ni kuhakikisha tunapanda miti katika barabara zote za Unguja na
Pemba na kuhakikisha kwamba tunaendeleza mandhari nzuri za barabara zetu, kama
ilivyo katika baadhi ya maeneo kama vile Bungi, ambako kila mmoja wetu
anafurahia kupita.
Napenda
kutoa wito kuwa skuli zetu na hata vyuo vyetu vipangiwe program maalum ya
kupanda na kutunza miti kwa wingi. Pengine kila mwanafunzi akipewa jukumu la
kupanda, kulea na kutunza mti mmoja tu kwa mwaka, basi tutaibadili nchi yetu
katika kipindi kifupi.
Pia
wananchi washajiishwe kuacha tabia ya kukata miti katika viwanja wanavyokusudia
kujenga nyumba zao. Badala yake wahakikishe kuwa nyumba wanazojenga
zinazunguukwa na miti kwa kuihifadhi iliyopo na kupanda mingine.
Wakati
mzuri wa kupanda miti ili istawi na kukua ni nyakati za misimu ya mvua. Hivyo
tuzitumie mvua hizi kupanda miti kwa wingi kama itakavyo wezekana.
Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Katika
msimu huu wa mvua, Serikali kwa kushirikiana na wana jamii pamoja na vikundi
vya kuhifadhi mazingira imedhamiria kupanda miti katika maeneo mbali mbali
ikiwemo hayo ya barabara. Jumla ya kilomita 50 za barabara tayari zimepandwa
miti katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Uongozi
wa Wilaya hizo pamoja na Masheha kwa kushirikiana na wananchi wote wana jukumu
la kushiriki kikamilifu katika kupanda miti, lakini pia kuihudumia miti hiyo.
Uzoefu unaonesha mara nyingi huwa tunapanda miti mingi hasa katika kampeni kama
hizi, lakini tatizo linakuja kwenye matunzo ya miti hiyo, ambapo mingi
hushindwa kustawi.
Waheshimiwa Viongozi na
Wananchi
Kwa
vile tumeshafanya kazi kubwa na muhimu ya kupanda miti katika barabara hii,
nisingependa kutumia muda wenu zaidi, hivyo basi nachukua fursa hii
kukushukuruni nyote kwa kushiriki katika Uzinduzi huu. Pia nakushukuruni sana
kwa utulivu na uvumilivu wenu kwa muda wote nilipokuwa nikizungumza.
إرسال تعليق