Rais Kikwete, TUCTA wajadili jinsi ya kuboresha maslahi na ustawi wa wafanyakazi.

kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
-Aagiza kukamilishwa kwa uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi, Aprili 17, 2014, alifanya mazungumzo na majadiliano ya kina na viongozi wa vyama vyote vya wafanyakazi nchini yenye nia ya kutafuta njia za kuboresha maslahi na ustawi wa wafanyakazi nchini.
Mazungumzo hayo ya muda mrefu yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kazi na Ajira Mheshimiwa Gaudensia M. Kabaka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi) Mheshimiwa Celina Kombani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Mkuya na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue.
Aidha, mazungumzo hayo yalihudhuriwa na maofisa waandamizi wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo zinahusika moja kwa moja na maslahi na ustawi wa wafanyakazi na uongozi wa vyama vya wafanyakazi uliongozwa na uongozi wa juu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania – TUCTA.
Rais Kikwete na viongozi hao wa vyama vya wafanyakazi nchini kwa zaidi ya saa 10 walijadili hali ya utekelezaji wa masuala na mambo yaliyokubaliwa katika kikao chao cha namna hiyo kilichofanyika Februari 27, Mwaka jana wa 2013.
Vile vile, Rais Kikwete na viongozi hao wakiwemo wale wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) walichambua kwa kina hoja za wafanyakazi zilizowasilishwa kwa Rais Kikwete na vyama hivyo.
Hoja hizo zilijadiliwa katika kikao hicho. Miongoni mwa hoja hizo ni ajira kwa wageni na athari zake kwa ajira ya Watanzania, athari za kuzuka kwa mawakala wa ajira nchini, watumishi waandamizi wa Serikali kushikilia nafasi za uongozi katika vyama vya wafanyakazi na athari zake, ushirikishwaji wa  wafanyakazi katika bodi za taasisi za umma na Serikali na uhamisho wa maofisa kazi ambao Rais Kikwete aliuagiza miaka mitatu iliyopita.
Hoja nyingine zilizojadiliwa ni hali ya afya ya wafanyakazi katika migodi mbali mbali nchini, bei ya umeme majumbani na athari yake kwa wafanyakazi, uwezekano wa kupunguza tena kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi jambo ambalo Serikali ililifanya Mwaka 2013, madai ya malimbikizo ya mapato ya wafanyakazi, madeni ya walimu na uwezekano wa nyongeza ya mishahara kwa walimu.
Katika kikao hicho, Rais Kikwete ameagiza wizara, idara na taasisi zote za Serikali na umma ambazo hazijatekeleza hitaji la kisheria ya kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma kufanya hivyo mara moja bila kuchelewa.
Rais Kikwete ametoa muda hadi Mei Mosi, mwaka huu, kwa wizara, idara na taasisi hizo kuwa tayari zimeunda mabaraza hayo na amemwagiza Balozi Sefue kutuma barua za maagizi hayo ya Rais kwa wizara, idara na taasisi husika.
Aidha, Rais amesema kuwa mwishoni mwa mwaka huu atapenda kupata taarifa kuhusu hali ya uanzishwaji na utendaji wa mabaraza hayo ambayo ni muhimu kwa uwakilishi wa wafanyakazi katika uendeshaji wa taasisi za umma ambazo wanazifanyia kazi.
Rais Kikwete amekiambia kikao hicho: “Wafanyakazi lazima washirikishwe kikamilifu katika uendeshaji wa taasisi wanazozifanyika kazi na hasa katika vikao vyote vya bajeti za wizara, idara na taasisi za umma ambako wameajiriwa.”

Post a Comment

أحدث أقدم