JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja, linamshikilia Ali Abrahmani Ali (49) mkaazi wa Kwamtipura kwa madai ya
kumwagia maji ya moto mfanyakazi wake wa ndani, alitambuliwa kwa jina la Tausi
James Mmirija (18) na kumsababishia maumivu makali.
Kamanda wa Polisi mkoa huo, Kamishna
Msaidizi,Mkadam Khamis Mkadam, alisema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti
hili ofisini kwake Muembe Madema.
Alisema tukio hilo limetokea tarehe 15 mwezi
uliopita ambapo mfanyakazi huyo akiwa katika matayarisho ya kumchemshia maji
bosi wake alikosana nae lugha na bosi huyo kuamua kumwagia maji ya moto binti
huyo.
Alisema tukio hilo limetokea baada ya Tausi
kuambiwa maneno asiyoyapenda na bosi wake hali iliyomfanya atoke nje ya nyumba
na bosi wake kuamua kumwagia maji yaliyokuwa yakichemka.
"Tukio limetokea baada ya Tausi
kuwambia maneno asiyoyapenda na bosi wake na wakati anatoka nje bosi wake
alimfuata akiwa na sufuria la maji ya moto na kummwagia,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo binti huyo
alifungiwa ndani ya nyumba licha ya kuwa na maumivu makali aliyopata.
Alisema polisi walipata taarifa ya tukio
hilo Machi 21 na baada ya kufuatilia waligundua binti huyo akiwa amefungiwa
ndani na kuamua kumchukua kumpeleka hospitali.
Kwa upande wa binti aliyetendewa unyama huo,
akizungumza na gazeti hili alisema, yeye anachotaka ni haki zake kwani tokea
alipofika Unguja Januari 4 ya mwaka huu amekuwa akinyanyasika kutoka kwa mabosi
wake wa kazi.
Binti huyo ambae ni mwenyeji wa Kahama,
alisema aliamua kufanya kazi za ndani ili kumsaidia bibi yake kwani wazazi wake
wote wamefariki lakini alipofika kwa bosi wake aliemtaja kwa jina la mama Chubi
alikuwa anamnyanyasa kwa kukumshambulia kwa maneno mabaya na alipomwambia
amlipe pesa zake za mshahara ili aweze kurudi kwao alikataa.
Alisema alivumilia mateso lakini
aliposhindwa aliamua kutafuta kazi sehemu nyengine na kuamua kumtoroka dada
huyo na kwenda kufanya kazi Darajabovu kwa mtuhumiwa ambapo alifika hapo Machi
6 na ilipofika Machi 15 ndipo alipokutwa na unyama huo baada ya kumkatalia ombi
lake la kutaka kufanya nae mapenzi.
"Niliamka asubuhi nikamtelekea maji ya
moto baba na yeye aliamka akanita ukumbini akanambia tufanye mapenzi nilikataa
kwa sababu sicho kilichonileta na kuanza kulia ndipo baba akataka kunibaka mimi
nikakimbilia uwani na yeye alitoka na kuchukua maji ya moto yaliyopo jikoni
ambayo yalikuwa yamechemka na kunimwagia," alifahamisha.
Alisema kuwa baada ya kufanyiwa tukio hilo
alijimwagia maji ya baridi na huyo mzee alimpaka asali alafu alimuacha ndani
bila ya kumpeleka hospitali na kumwambia kuwa akiulizwa na mtu asiseme kama
amemwagiwa maji ya moto na yeye.
Alisema ilipofika jioni alimpigia simu mama
mwenyenyumba na alipokuja alimwambia kaanguka na kumwagikiwa na maji ya moto.
"Baba alinambia nikiulizwa na mtu
yeyote nisiseme kama nimemwagiwa maji moto na yeye na nikisema ataniuwa na mama
alipomwambia wanipeleke hospitali alimkatalia akamwambia wewe sio uliemleta
hapa,"alisema.
Tausi alitumia nafasi hiyo kuitaka serikali
imsaidie ili aweze kupata haki zake na aweze kurudi kwao kwa usalama.
Kwa upande wa Mratibu wa nyumba salama,
Aisha Ali Ibrahim, ambako mtoto huyo anatunzwa, alisema lengo la kumuhifadhi
mtoto huyo katika nyumba hiyo ni kusubiri kesi iendelee na asije kupoteza
ushahidi.
Alisema wao wapo kwa lengo la kumsaidia
mtoto huyo aweze kupata haki zake na wakimaliza watamrudisha kwao kwani na yeye
mwenyewe hayupo tayari kuendelea kuishi tena Unguja.
Mratibu huyo alifahamisha kuwa nyumba salama
imefunguliwa kwa lengo la kutoa huduma kwa jamii ili kutokomeza vitendo vya
udhalilishaji na unyanyasaji vinavyoendelea kufanywa kila siku.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kujibu shitaka linalomkabili.
Post a Comment