
Pia ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii na Uongozi wa Muhimbili, kuandaa utaratibu na kuhakikisha kituo
hicho kinafanya kazi kwa kujitegemea ili kiwe na ufanisi zaidi, kama
ilivyo Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa
Ubongo (MOI).
Alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa kituo hicho, Dar es Salaam jana.
Rais
Kikwete alisema Serikali haitavumilia kuona wodi hizo zikitumika vibaya
kwa wagonjwa wasiokuwa wa moyo, huku wagonjwa wa moyo wakikosa mahali
pa kulazwa.
"Haitakuwa na maana ya kuwepo na kituo hiki, jiepusheni
na ushawishi wa kugeuza wodi za kituo hiki kuwa cha watu maarufu na
wenye fedha ambao si wagonjwa wa moyo," alisema.
Alisema kutokana na
ubora wa wodi hizo, watu hao wana uwezo wa kulipa kiasi chochote cha
fedha ilimradi walazwe, bila kujali wagonjwa wahusika wa moyo.
Kutokana
na umuhimu wa kituo hicho nchini, hasa katika maendeleo ya sekta ya
afya, Rais alitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na uongozi wa
Muhimbili, kuweka utaratibu wa kuhakikisha kinajitegemea kama ilivyo
MOI ili kijiendeshe kwa ufanisi.
"Kwa umuhimu wa kituo hiki,
kikitegemea bajeti moja ya Muhimbili ndipo na chenyewe kipate mgawo,
kuna uwezekano wa huduma muhimu kukosekana ni bora uwekwe utaratibu
mapema, kwani Moi kama ingetegemea Muhimbili, ingekuwa katika hali mbaya
kutokana na uhaba wa fedha," alisisitiza.
Pamoja na hayo, aliitaka
Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) kutambua umuhimu wa kituo hicho cha Moyo
na kuhakikisha dawa na vifaa vya tiba vinapatikana wakati wote.
"Hapa
napenda nisisitize kuwa Serikali haitakuwa tayari kusikia eti kituo
hiki hakina dawa za kutosha wala vifaa, maana umuhimu wake kwa
Watanzania hautakuwepo, MSD tambueni kituo hiki, ili lengo la kupambana
na ugonjwa huu lifikiwe," alisema.
Alisema pamoja na Shirika la Afya
Duniani (WHO) kutoa takwimu zinazoonesha kuwa kila mwaka watu milioni 12
hufariki kwa ugonjwa wa moyo duniani, Tanzania kasi ya ongezeko la
wagonjwa wa moyo ni kubwa, ambapo asilimia 26 ya wagonjwa hao, hufariki
kila mwaka.
Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ilitafuta msaada
kwa Serikali ya China kupitia Rais Xi Jinping aliyekuwepo nchini hivi
karibuni, ambapo alikubali China kuchangia ujenzi wa kituo hicho, kwa
kutoa Sh bilioni 16.6 na Tanzania ilichangia Sh bilioni 10.
Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, alisema uwepo kwa kituo
hicho, utapunguza gharama za Serikali kusafirisha wagonjwa wa moyo nje
ya nchi na kupunguza idadi kubwa ya vifo vya wagonjwa wa moyo, kutokana
na ukosefu wa tiba hiyo nchini.
Alisema kituo hicho, ambacho tangu
kianze mwaka jana kimeshafanya upasuaji wa wagonjwa 33, kitatoa huduma
za upasuaji mkubwa wa moyo, vipimo vya moyo kwa kutumia vifaa vya kisasa
na uchunguzi wa mishipa ya damu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya
Muhimbili, Profesa Joseph Kuzilwa, alisema licha ya ukosefu wa kitengo
maalumu cha tiba ya moyo nchini, hospitali hiyo ilishaanza kufanya
upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 362 tangu mwaka 2008.
"Lakini ni jambo
la kujivunia kuwa sasa kuna kitengo maalumu cha tiba ya ugonjwa huu
hatari, ambapo idadi ya wagonjwa itaongezeka kwa kuwa jengo hili lina
vyumba vya upasuaji vitano, wodi 32 za uangalizi maalumu na vitanda 96
vya kulazia wagonjwa, pia kituo kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 400 kwa
wiki," alisema.
Mjumbe Maalumu na Mwakilishi wa Rais wa China
nchini, Xi Jinping ambaye pia ni Naibu Spika wa China, Chen Changzhi,
alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya ishara ya urafiki na undugu
baina ya China na Tanzania, ambao umedumu kwa miaka 50 sasa.
Katika
hafla hiyo, viongozi kadhaa waanzilishi wa ujenzi wa kituo hicho,
walitunukiwa vyeti, akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Wizara hiyo,
Dk Deo Mtasiwa.
إرسال تعليق