Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
-Aagiza kukamilishwa kwa uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
Alhamisi, Aprili 17, 2014, alifanya mazungumzo na majadiliano ya kina na
viongozi wa vyama vyote vya wafanyakazi nchini yenye nia ya kutafuta
njia za kuboresha maslahi na ustawi wa wafanyakazi nchini.
Mazungumzo
hayo ya muda mrefu yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam yalihudhuriwa pia
na Waziri wa Kazi na Ajira Mheshimiwa Gaudensia M. Kabaka, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi) Mheshimiwa Celina Kombani, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Fedha
Mheshimiwa Saada Mkuya na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue.
Aidha,
mazungumzo hayo yalihudhuriwa na maofisa waandamizi wa Serikali wakiwemo
Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo zinahusika moja kwa moja na maslahi na
ustawi wa wafanyakazi na uongozi wa vyama vya wafanyakazi uliongozwa na
uongozi wa juu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania – TUCTA.
Rais
Kikwete na viongozi hao wa vyama vya wafanyakazi nchini kwa zaidi ya saa
10 walijadili hali ya utekelezaji wa masuala na mambo yaliyokubaliwa
katika kikao chao cha namna hiyo kilichofanyika Februari 27, Mwaka jana
wa 2013.
Vile vile,
Rais Kikwete na viongozi hao wakiwemo wale wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT) walichambua kwa kina hoja za wafanyakazi zilizowasilishwa kwa Rais
Kikwete na vyama hivyo.
Hoja hizo
zilijadiliwa katika kikao hicho. Miongoni mwa hoja hizo ni ajira kwa
wageni na athari zake kwa ajira ya Watanzania, athari za kuzuka kwa
mawakala wa ajira nchini, watumishi waandamizi wa Serikali kushikilia
nafasi za uongozi katika vyama vya wafanyakazi na athari zake,
ushirikishwaji wa wafanyakazi katika bodi za taasisi za umma na
Serikali na uhamisho wa maofisa kazi ambao Rais Kikwete aliuagiza miaka
mitatu iliyopita.
Hoja
nyingine zilizojadiliwa ni hali ya afya ya wafanyakazi katika migodi
mbali mbali nchini, bei ya umeme majumbani na athari yake kwa
wafanyakazi, uwezekano wa kupunguza tena kodi kwenye mishahara ya
wafanyakazi jambo ambalo Serikali ililifanya Mwaka 2013, madai ya
malimbikizo ya mapato ya wafanyakazi, madeni ya walimu na uwezekano wa
nyongeza ya mishahara kwa walimu.
Katika
kikao hicho, Rais Kikwete ameagiza wizara, idara na taasisi zote za
Serikali na umma ambazo hazijatekeleza hitaji la kisheria ya kuundwa kwa
mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma kufanya hivyo mara moja
bila kuchelewa.
Rais
Kikwete ametoa muda hadi Mei Mosi, mwaka huu, kwa wizara, idara na
taasisi hizo kuwa tayari zimeunda mabaraza hayo na amemwagiza Balozi
Sefue kutuma barua za maagizi hayo ya Rais kwa wizara, idara na taasisi
husika.
Aidha, Rais
amesema kuwa mwishoni mwa mwaka huu atapenda kupata taarifa kuhusu hali
ya uanzishwaji na utendaji wa mabaraza hayo ambayo ni muhimu kwa
uwakilishi wa wafanyakazi katika uendeshaji wa taasisi za umma ambazo
wanazifanyia kazi.
Rais Kikwete amekiambia kikao hicho: “Wafanyakazi
lazima washirikishwe kikamilifu katika uendeshaji wa taasisi
wanazozifanyika kazi na hasa katika vikao vyote vya bajeti za wizara,
idara na taasisi za umma ambako wameajiriwa.”
Post a Comment